September 25, 2009

JE UNASADIKI KUNA UCHAWI?


Ndugu zetu wa Globalpublishers wametuwekea picha hii tangu habari hiyo ilipovumbuliwa na Knaisa la mama Lwakatare. Tunawashukuru kwalo.
Jambo moja la msingi ninaloongelea leo ni suala la UCHAWI/USHIRIKINA. Baadhi yetu tuliozaliwa ukanda wa nyasa siyo jambo geni wala halitishi kama ambavyo wengi wanavyotishika. Nakiri kwamba katika makuzi yangu nimekuwa nikisikia habari hizi na siyo mara moja nimezijua, nazielewa napengine nimeshuhudia matukio kadhaa.
Kwetu nyasa hapa, mambo ya uchawi yanasikika na unaweza kuambiwa familia ya fulani ni wachawi sana kwahiyo usioe wala kuolewa nao. Ni jambo la kawaida jamii kufikia kuamini kile kinachowazunguka. Kwani ndicho wanachokiona kila leo. Uchawi hapa nyasa ni suala ambalo limetamalaki na familia zinaweza kuogopana kwasababu ya uchawi. Hili utalikuta katika ngoma za utamaduni, soka, sherehe, uvuvi na mambo mengine. Siyo ajabu kukuta nyavu zinafungwa mafundo kadhaa yenye kila dalili za ndumba au kuona namna jambo fulani linavyohususishwa na wachawi.
TUKIO LA KUKUMBUKWA. Mwaka 1994 kulikuwa na kundi kubwa sana la watalii hapa kijijini kwetu LUNDU, kundi hilo ilikuwa ni kawaida katika miezi kama hii ya septemba na oktoba. Wazuungu wale walishangaza sana, walipokuwa ziwani pale walivalia vikaptura vya jeans, na wengine walikuwa wamevaa kawaida tu. Lakini tumezoea kuwa ifikapo saa 12 jioni wengi wao huondoka na kurejea pale Misheni yaani kama Monesteri za mapdre na masista kwa wanawake.
Wao hawakuondoka, wakatulia hapo hadi usiku wa manane, na kwakuwa ufukwe ule upo karibu makaburi basi wakaanza kufunga taa(umeme) kwa kutumia betri za gari. Wakafunga katika msalaba mkubwa uliopo katika ya makaburi yale na misalaba mingine. Baadhi yetu tuliokuwa karibu wamisionari tulijua kuwa hawa wageni wanataka kupiga picha za video ili wawanase wachawi. Ndivyo walivyofanya na inasadikika ilikuwa hivyo. Baadhi ya wafanyakazi wa wamisionari wale waliofanikiwa kuona video hizo wakataja baadhi ya watu wa familia fulani kuwapo katika mkanda huo. Je walikuwa wachawi kweli?
Dhana nyingine ikadaiwa kuwa wazungu wale nao ni wachawi, lakini hatukuweza kuthibitisha hilo. Lengo la kupiga picha zile ilikuwa kutaka kuwaonyesha wakazi wa kijiji chetu adhimu cha LUNDU. lakini kwa hekima za mwenyeji wao Padre Rainer alikataa jambo hilo na kuwaamuru kuwa wasionyeshe hapo bali wakafanye huko waendako. Ikawa hivyo...sijui kilichoendelea.
Vilevile katika kijiji chetu hiki eneo hilohilo la makaburi kuna miti mikubwa miwili ya mibuyu. Cha ajabu kuna mti mmojawapo kila ukiangua mabuyu yale wakati mwingine unaweza kukuta nywele ndani yake ay damu. Hilo linashangaza na linaendelea kushangaza sikusimuliwa nimeshuhudia mwenyewe hapa kwetu. Unaweza kuchuma mabuyu hayo lakini ukakinai kuyala. Tukirudi kwa wazungu wale walichofanya baada ya kuzuiliwa kuonyesha picha zile usiku uliofuata wakapiga kambi tena pale makaburini na kuanza kung'oa misalaba kadhaa na kuitupa. Wakaishia zao na kurejea kwao Bavaria-Ujerumani.(mji ambao baadhi ya wakazi wake ni wahudhuriaji sana hapa LUNDU) . Nikomee kwa hapa leo, kuna mengi ya kusimulia katika mjadala wa uchawi. Je wewe unasadiki kuna uchawi?

6 comments:

  1. Mie siamini haya mamba hata kama nimezaliwa sehemu hizo:-)

    ReplyDelete
  2. Naanza na story ya hoyo picha. huo ulikuwa UWONGO. niwiwa na mawazo kuwa pengine hi ilikuwa deal ya kuvutia waumini wengi zaidi kuwa kanisa la mama yetu lina upako. si kweli kabisa. haina tofauti na yule bibi harusi mtarajiwa aliyekamatwa tabata kumbe alikuwa kaandaliwa na mmiliki wa kanisa kuuonyesha uma kanisa 'lake' limesheheni UPAKO. hamna lolote ni upuuzi tu. watu wengi siku hizi wamekata tamaa ya maisha kwa namna anuai. hivyo wanatafuta ufumbuzi wa maisha yao. sasa yanapotokeza makanisa ya 'upako' (sina uhakika upako wa MUNGU au wa MIUNGU)watu waliopoteza matumaini wanamiminika huko wakiwa na matumaini ya kutatua matatizo yao.

    Kwenye hoja ya msingi sasa. uchawi upo. halafu uchawi sio kitu kibaya. uchawi ni kama aina fulani ya madawa ambayo yakitumiwa vyema huponya, yakitumiwa vibaya huua. uchawi ulikuwa kwa madhumuni na kurekebisha tabia katika jamii. ulitumika katika kuonya ama kutoa adhabu kwa mtu aliyepogoka katika msari wa maadili ya jamii husika. siku hizi wameutumia vibaya kama ambavyo dawa ukizitumia vibaya zaweza kuleta kizungumkuti katika jamii. nasikia hata baadhi ya madaya ya kulevya yana vipimo mahsusi kwa wagonjwa fulani fulani. lakini tunaona jinsi gani wanaotumia vibaya wanavyoadhirika mitaani. huu ni mfano tu.

    katika jamii za leo ndugu wa sumbawanga bado wanamatumizi mazuri ya uchawi. ukienda kwao uliza taratibu zao na ukizifuata utaishi miaka tisini na kenda. ukipora mke wa mtu utakiona, ukiiba mahindi ya mtu utakiona, ukijimegea shamba la mtu utakiona. usipofanya mabaya haya yote utaishi vema huko kwao. sehemu nyingine mathalani kwetu kyela (mbeya) uchawi unatumiwa vibaya. mtu anakuona tu umenunua shati jipya anakuweka mshipa. this is really a serious misuse of the natural gift that was for punishing and warning wrong doers.

    ReplyDelete
  3. Jamaa alivyokodoa macho kwenye hiyo picha ni changamoto tosha ya kunifanya nisadiki kuna uchawi :-)

    ReplyDelete
  4. Prof mbele lakini hii ni ya kutengeneza. wanawalipa pesa kidogo wanawatrain on how to pose, wanawaambia wasitamke neno lolote, waact kama wehu na kadhalika

    ReplyDelete
  5. Ndugu Mwaipopo, shukrani kwa kunibonyeza hayo. Nashawishika kupiga mehesabu upya :-)

    ReplyDelete
  6. Jamaa hendisamu na anamitalenti lukuki halafu eti kwenye movie za kibongo hayupo!:-(

    ReplyDelete

Maoni yako