January 28, 2013

CHOMBEZO: AMUA SASA NI MAISHA YAKO


Markus Mpangala

Na Markus Mpangala
Usinitazame kwa huzuni. Nitazame kwa furaha kwakuwa sijui namna ya kufirikia matatizo. Sijui namna ya kuwaza kwamba vikwazo vitaniandama. Bali nawaza namna bora na namna ninavyoweza kuishi kwa njia bora. Huwa siwezi kufikiria vikwazo kwakuwa najua vitanirejesha nyuma ili nitaabike. Ninasonga mbele. Usikae ukajuta. Fikiria njia zako. Tafakari kile unachokifanya ili kufanye jambo moja tu la kuamua maisha yako. 
Amua leo usisubirie kesho. Amua kitu kimoja tu ili uweke misingi maishani au kutoweka misingi. Amua moja kama unadhani kkimbia matatizo ni suluhisho. Amua tu kama unadhani mapenzi bora  anapatikana nyumba ndogo kuliko kwa njiwa wako ulimwahidi kuimba naye nyimbo zenye marashi ya huba milele. 
Iko wapi ile ahadi ulimwahidi mwenzio kuwa mtaimba nyote nyimbo tamu za mapenzi yaliyojaa huba. Iko wapi ahadi ulimwahidi binti wa wenzio kwamba utamvika pete ya ndoa. Kwani umgeuze mtoto wa wenzio kuwa kitoweo kisha ukishiba unatanga na njia?
Kwanini iwe hivi kwake na si wewe kutendewa. Ni vizuri kufanya uamuzi mapema kuliko kumwingiza kwenye matatizo huku ukijua unaweza kuyakwepa. Amua sasa maana siku utakayoamua utakuwa umechelewa, basi nakuhimiza sasa. 
Endapo njia zako hazina misingi basi unakaribisha tatizo kubwa. Endapo huna falsafa basi  nakaribisha kasoro maishani mwako. Acha kuwarubuni watoto wa wenzio, acha kuwafanya wao ni kitoweo chako pale udhaniapo unahitaji kula daima. Nakutaka uamue leo na si kesho ambayo hujui itakuwa na sura gani siku hiyo. 
Amua sasa kama unaona hakuna haja ya kusoma au kufanya kazi. Maana wapo watu wanadhani wanaakili kuliko akili zao zilivyo. 
Amua sasa kwamba hutawasumbua watoto wa wenzio. 
Amua sasa kwamba unahitaji kufanya kazi kwa bidii. 
Amua sasa kwamba ofisi yako inahitaji uwajibikaji wa pamoja. 
Taswira ya Mungu
Amua sasa kama unaona mkataba wako haukunufaishi, basi achana nao kwa nia njema kabisa kuliko kuwaghilibu wenye kampuni kuwa u mfanyakazi mwenye hamu ya kuendelea kufanya nao kazi. 
Kuna mambo maishani ni lazima yafanyiwe uamuzi. 
Ni muhimu kuyaangalia kila leo maana ya kesho huwezi kuyaona kwakuwa mshale wa saa unakuwa na mambo mengine zaidi ya hayo. Najua wapo wengine wenye matatizo ya kiafya,mali na mengineyo. Lakini hakuna jambo zuri kwenye maisha kama kufanya uamuzi juu ya hali uliyonayo.
Endapo wewe huna kazi, amua kuwa unahitaji kazi inayoweza kukufanya ukafanya mambo mazuri zaidi. Au unaweza kuamua kwa kuwa mchuuzi maana kushindwa yule si kushindwa kwa wewe. 
Jukumu lako ni kuamua namna ya kuishi kwenye hii sayari yetu ya dunia. Ni muhimu kuyafanya maisha yako kuwa bora kwakuwa hakuna kizuizi chochote. 
Hakuna awezaye kukuzuia ikiwa unafuata taratibu halali za maisha yako. Ni mwenyezi Mungu pekee anaweza kukuzuia lakini mafanikio yako yapo mikononi mwako. Juhudi zako ndizo zitakufanya uwe bora kila siku. 
Amua moja kusuka ama kunyoa, kufunga pingu za maisha au kukaa kuoa. Kuishi vizuri au kuishi kipuuzi. Ni wewe unaweza kuamua namna ya kuishi kwenye hii dunia. Amua moja tu ndugu yangu. Amua ukijua kuwa uamuzi wako unastahili kuheshimiwa na watu wote. 
Usifanye jambo ambalo linaumiza nafsi yako. Amini uamuzi wako unastahili kukufanya uishi vizuri zaidi ya leo. Ni wakati wako wa kufanya uamuzi ili uweze kujua unakokwenda na namna gani unaweza kuishi kwa amani. Amua sasa. 
Misingi ambayo itakufanya uwe na nyumba bora, familia bora na yenye amani ila siku. Familia yenye heshima na wingi wa upendo. Lakini muhimu ni kuamua namna ya kuwa familia hiyo.  Huwezi kupanga kuwa na familia yenye upendo ikiwa hujawa sehemu ya upendo huo. 
Huwezi kuota kuwa na mke mwema/mume ikiwa matendo yako hayaambatani na wema/upendo. Unatakiwa kujiuliza sana kila unavyoishi. Jaribu kujenga picha ambayo mbele yako unajiona na kujisemea kuwa unajipenda. 
Basi vivyo hivyo unatakiwa kuwapenda wengine ama famili yako. Yote haya yanakujia ikiwa tu umeamua kupenda na kutazama njia zenye mustakabali mwema maishani. Hebu  jiulize kwanini wewe huwi mfano wa kuigwa bali unabaki kusema kwamba unataka kumuiga fulani? Kwanini usiamue kuwa wewe unayeigwa badala ya kuwatazama wengine? 
Amua sasa kuwa maisha yako yatakuwa mfano wa kuigwa zaidi kadiri unavyokwenda maana ni wewe tu uwezaye kusuka taswira ya maisha yako. Uwe mfano zaidi kila siku ili utambue thamani ya kuigwa. Sasa ili kuweza kuamua maisha yako basi ni lazima utambue kuna kanuni zinazoongoza maisha ya wale unaowaiga kwa maisha yao mazuri na mema. 
Ni misingi 6 tu ya kuamua namna ya kuishi kutenda mema ama mabaya. Bila shaka utanielewa vema. Na uichunge misingi 6 hii iwe dira yako maishani mwako ili ufanikiwe.
1.Usimchukie yeyote hata kama atakukosea vipi.
2.Ishi maisha ya kawaiada hata kama upo juu kwa kiasi kikubwa.
3. Tarajia heri hata kama mitihani inakusakama.
4. Toa kwa wingi hata kama wewe umenyimwa.
5. Onesha tabasamu hata kama moyo  unavuja damu
6. Usiache kumuabudu mungu.
Nakutakia siku njema na afya nje. Usisahau kuwa yaliyotokea jana yanakufahamisha kwamba aidha ujirekebishe au unapaswa kusonga mbele kutokana na hali ilivyo sasa. Ichunge misingi hiyo muhimu maishani. AMUA SASA.

2 comments:

  1. KUAMUA, KUWA NA MSIMAMO NDIO MSINGI WA MAISHA ..NIMEPENDA SOMO LA LEO....

    ReplyDelete
  2. julieth mushi29 January, 2013

    Asante kwa somo lako linatufundisha mambo mengi linatutia moyo tuwaze mafanikio mbele katika maisha na pia Kamwe tusikumbuke matatizo yaliyopita sababu yanaumiza na tusiwaze yajayo sababu yanatia hofu,ila maisha ni hapo ulipo maamuzi ni kielelezo cha maisha bora yajayo. unatazama mbele kwa kujiamini nyuma kwa taadhari na ulipo kwa matumaini hapo tutajenga maisha bora na si bora maisha...

    ReplyDelete

Maoni yako