January 29, 2013

SOKA AFCON; CAPE VERDE, WANAJIAMINI WANAJUA SOKA


Na Markus Mpangala, Dar es salaam

Angola imechapwa magoli 2-1 na Cape Verde, taifa ambalo taifa linalokadiriwa kuwa na idadi ya watu 500,000 tu kulingana na sense zao. Cape Verde imeingia robo fainali huku kocha wake, Lucio Antunes akiongeza sifa katika kazi yake ya ukocha. Ingawa nahodha wake Fernando Neves alijifunga bao la kwanza, lakini aliongoza vema kikosi chao kuishinda Angola kisha kutinga robo fainali. Ni mafanikio makubwa kwao.

Cape Verde inashiriki michuano ya mataifa ya afrika yanayoendelea nchini Afrika Kusini. Kama tujuavyo michuano hii ilitakiwa kufanyika nchini Libya, lakini kutokana na matatizo ya kisiasa yaliyotokea nchini humo yalisababisha majadiliano baina ya chama cha soka cha Afrika kusini na kile cha Libya hivyo kubadilisha michuano.
Kocha wa Cape Verde, Lucio Antunes
Kimsingi Afrika Kusini ilitakiwa kuwa mwenyeji wa michuano ya mwaka 2015, hivyo basi kwakuwa imekuwa mwenyeji mwaka huu basi michuano ijayo itafanyika nchini Libya. Tukiitazama Cape Verde inayoshiriki michuano hiyo ikiwa na wachezaji wengi vijana wameonyesha soka safi ambalo liliwafanya waweze kufuzu kwa michuano hiyo.

Cape Verde imetinga fainali hizo ikiwa na kumbukumbu ya kuisambaratisha Cameroon kwa mabao 4-0 wakati wa kuwania kufuzu kwa AFCON. Kwa sasa wengi wanaitazama Cape Verde kama somo la kuendeleza soka. Idadi ndogo ya watu, kujiamini, kujua soka, lakini imejikuta ikikosa jambo moja tu uzoefu wa mashindano ya kimataifa kama AFCON. Pambalo la kwanza la Cape Verde lilikuwa baina yao na wenyeji Bafana Bafana. Pambano hilo lilimalizika kwa suluhu ya kutofungana hali ambayo iliibua maswali kwa wadau wa soka wa kote afrika hususani wenyeji waafrika kusini.

Matokeo ya pambano hilo ilimlazimu kocha wa Afrika kusini, Gordon Ingesund kufanya mabadiliko katika kikosi chake. Awali alimweka benchi mshambuliaji hatari Katlego Mphela na kumwanzisha Majoro hali ambayo iliwakuta wakishindwa kufurukuta mbele ya ngome ya Cape Verde inayoongozwa na nahodha Neves na T. Varela.

Pambano la kwanza kwa Cape Verde lilionyesha ushahidi kuwa ilijiandaa kwa AFCON mwaka huu na ilipania kufanya vema. mpaka sasa Cape Verde wamejikusanyia pointi mbili, wakiwa nyuma kwa pointi mbili kutoka kwa vinara Afrika kusini. Cape Verde ilitoka sare ya mabao 1-1 dhidi ya Morocco, hivyo kushika nafasi ya pili. Huku Morocco ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi mbili na bao moja baada ya kutoka suluhu na Angola.

Aidha, pambano la pili Afrika Kusini iliichapa Angola kwa mabao 2-0, huku mshambuliaji Siyabongwa Sangweni wa Afrika Kusini akiibuka shujaa kutokana na mchezo mzuri uliomfanya apachike bao la kwanza. Afrika kusini iliingia pambano la pili ikimwanizhs beki wake hodari Tsepo Masilela ambaye alikosekana kwenye pambano la kwanza. Hali hii ilimsaidia sana nahodha wao Khumalo kucheza kwa kujiamini na kuongoza jahazi la nchi hiyo kwa ufanisi.

Lakini kwa Cape Verde ni wazi imeingia kwenye michuano hii ikielewa kuwa ni sehemu ya kujifunza licha ya kushindana kwa dhati. Washambuliaji wake Platini, Ryan Mendes wamekuwa kivutio kwa mashabiki wa soka wanaoifuatilia timu hiyo. Ryan Mendes akicheza kama shambuliaji wa pili katika mfumo 4-3-3, ameng’ara sana kutokanana kujaliwa kipaji kikubwa cha soka. Platini licha ya kuwa mshambuliaji mwenye kipaji anakabiliwa na ukosefu wa stamina ambayo ingelimwezesha kufanya maajabu mbele ya lango la adui.

Kwa upande wa kushoto beki Nivaldo anaonekana kucheza kwa utulivu lakini anaoksa kasi ya mchezo. Yeye ni beki aina ya Timothee Atouba, wanaocheza soka la taratibu sio kasi kasi kama Essou Ekotto. Lakini moja ya mabeki wanavutia kuwatazama jinsi wanavyoshughulikia washambuliaji ni nahodha wa Cape Verde, Neves  na Gege ambaye ni beki wa kulia wa timu hiyo.
wachezaji wa Cape Verde wakishangilia
Wanacheza soka la nguvu na vipaji. Wanajua namna ya kukabiliana na washambuliaji hatari kama Belhanda wa Morocco, mawinga hatari kama Siphiwe Tshabalala  wa Afrika kusini. Kila unapoitazama Cape Verde ikitandaza soka, utaona kwua inao vijana wanaojiamini sana, na wanajua kucheza soka. Mpangalio wao wa mashambulizi mara nyingi hutegemea kasi ya Ryan Mendes, ambaye amekuwa mchezaji kivutio zaidi na mwenye kilifahamu lango la adui kwa ufasaha.
Pia Cape Vaerde inayo bahati moja kubwa, viungo Soares na Mendes wake wanajua kupiga mashuti makali wakiwa na lengo la kujaribu kufunga. Mashuti hayo yanaweza kulenga goli (on target) au kutoka nje ya goli(off target) lakini jambo la msingi wanajaribu kutuonyesha kile walichonacho katika soka. Kwenye safu ya ushambuliaji Platini na Tavares wamekuwa tishio kwa kiwango cha kuridhisha, lakini wanaosa uzeofu tu. 

Tavares anatumika kama mshambuliaji wa kupambana na mabeki, huku Platini akiwa mshambuliaji wa pili maalumu wa kupachika mabao. Ni sababu hii inaonekana timu pinzani zinamfanya rafu mbaya sana Platini kuliko mchezaji mwingine yeyote wa Cape Verde. Kila dakika wanayocheza dimbani wanavutia, wanaburudisha na kujenga taswira mpya ya soka baada ya vigogo kama Cameroon na Senegal kukosekana kwenye michuano hii. Kwa watanzania wanaikumbuka Cape Verde iliyotuchapa mabao 2-1 wakati Taifa Stars ilipokuwa ikinolewa na Marcio Maximo.

Ni wazi wakati ule Cape Verde nayo ilikuwa kwenye kipindi cha mpito cha kujitengenezea njia ya mafanikio kisoka. Hatimaye mwaka huu wanashiriki AFCON, na wametuonyesha kuwa vipaji, kujiamini na kupangilia mambo ni msingi mkubwa wa mafanikio. Jambo lililo wazi na kufurahisha ni kwamba mfumo wa Cape Verde wa 4-3-3 uko wazi sana na unaonekana kwa uwazi ambao timu pinzani zinaweza kuichapa mabao mengi. Lakini Cape Verde wana nidhamu sana katika mchezo. Wanajua soka, wanajiamini lakini safu ya ulinzi inahitaji uzoefu zaidi. Platini anahitaji stamina, Mendes atakuwa bonge la kiungo siku za mbele. Tujifunze, na ku-graduate.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako