February 19, 2013

UCHAGUZI MKUU: HOFU YA MACHAFUKO YAREJEA KENYA

Dorine Otinga

Na Dorine Otinga, Eldoret, Kenya

MDAHALO ulimalizika vizuri mapema Jumatatu wiki iliyopita hapa Kenya, huku wagombea wote wakionyesha uwezo mkubwa.
Martha Karua, Raila Odinga, Peter Kenneth, Uhuru Kenyatta ni wagombea waliovuta hisia za wananchi wa Kenya kutokana na uwezo wao wa kujibu hoja na kuelezea sera zao iwapo watafanikiwa kushika madaraka.

Takribani wananchi 328 waliotazama mdahalo huo kwa njia ya runinga wanakubali kuwa ushindani wa wagombea umekuwa mkubwa. Pia mdahalo umeboresha uelewa wananchi wa Kenya kujua ni mgombea gani anafaa kuwa rais badala ya Mwai Kibaki.Siku chache zilizopita baada ya mdahalo, Taasisi mbalimbali za utafiti ziliendesha zoezi la kura za maoni juu ya uamuzi wa wakenya kuchagua rais Machi 4, mwaka huu.
Watu 92% wamekubali kuwa mdahalo kwa njia ya runinga ulisaidia kujua mbinu na uwezo wa kujieleza wa wagombea wao. Wengine 24% walilazimika kubadili mawazo yao kwaajili ya wagombea waliodhani watawachagua. Kwahiyo, mdahalo umeleta changamoto kwa wagombea kuweza kuwapata wapigakura sahihi ili kuibuka na ushindi. Wapigakura hawa 34% ina maana wamebadili mawazo kutoka kwa mgombea mmoja kwenda kwa mwingine.

Uhuru Kenyatta
Pengine wapo waliopanga kumchagua Musalia Mudavadi au Raila Odinga na Uhuru Kenyatta, lakini kutokana na kuwatazama na kuwasikiliza kupitia mdahalo, ni wazi wananchi wamebadili mitazamo juu ya wagombea hao. Profesa James Kiyiapi alitangaza mageuzi ya elimu ya hapa Kenya. Raila Odinga alitangaza mageuzi 18 ya kimaendeleo ambayo atayafanyia kazi ipindi akingia madarakani kuongoza wakenya; elimu bure, afya, na uwajibikaji sekta ya umma. Naye Martha Karua amekusudia kupambana na ufisadi unaolitafuta taifa letu kwa miaka mingi sasa. Kwenye mdahalo huo wagombea ambao hawakufua dafu ni Musalia Mudavadi, Paul Muite na Mohamed Abduba Diba.

Mvuto wao kwa wapigakura bado dhaifu, haitegemewi kama wataweza kumudu ushindani wa Uhuru na Odinga. Wakenya 27% wanadhani Uhuru Kenyatta atashinda uchaguzi. Wakenya 26% wanaamini Peter Kenneth atashinda kutokana na kufanya vizuri kwenye mdahalo. Vilevile 22% ya wakenya wanaamini Raila Odinga atashinda uchaguzi na yeye ndiye bingwa wa ushawishi hadi sasa akiwa na mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka.

Halafu kuna 12% wanapenda kuona Martha Karua akishinda kuchukua uongozi. Sasa baada ya kuona hiyo, na sasa tuone suala nyeti ambalo linagusa sana wagombea wa urais hapa Kenya. Kwanza, suala la kisiwa cha Migingo ambalo limeleta ugomvi na Uganda ya Yoweri Museven. Kenya na Uganda zingeweza kuingia vitani kutokana na kuzozania kisiwa cha Migingo ambacho kimsingi ni chetu hapa Kenya.
Yoweri Museven alinuia kupeleka majeshi kisiwani Migingo, lakini alisahau kuwa hata sisi Kenya tunaweza hilo. Mwai Kibaki alilaumiwa kupuuza sana suala la kisiwa cha Migingo lakini ni vema anaondoka madarakani huku mapigano baina ya Kenya na Uganda hayakutokea. Suala hili linachukuliwa kama hatua nzuri ya kulinda amani, lakini haieleweki iwapo mshindi wa urais Machi 4 atavumilia kama Mwai Kibaki alivyofanya kwa kisiwa cha Migingo.
Hili ni suala la nje ya mipaka ya Kenya yetu, lakini yapo mengine yanashiria kuleta mapigano baada ya uchaguzi. Hofu hii imejaa kwa wengi miongoni mwa wakenya.
Dalili mojawapo ni mapigano ya kikabila kule Tana River ambako watu 140 walifariki dunia kutokana na ugomvi wa kuwania mifugo. Hili la Tana River lazima itakuwa moja ya dalili za kutoelewana kwa wakenya hivyo ukabila kuchukua nafasi hata kwenye uchaguzi huu. Yapo maeneo ambayo yanaongoza suala la kabila hapa Kenya.
Raila Odinga
Mfano, ingawa si sehemu zote, lakini Rift Valley Province kuna ukabila sana. Hofu ni vita baada ya uchaguzi kutokana na makabila kutoelewana kabisa. Kwa Rift Valley Province ina makabila nyingi, lakini kabila lenye watu wengi ni Kalenjin na Wakikuyu, ambao hawajawahi kusikizana kabisa.

Sasa hawa Wakalenjin na Wakikuyu wamekuwa mwiba kwa miaka mingi kila mmoja akiona yeye ni bora kuliko kabila lingine. Eneo jingine ni Nyanza Province ambalo kuna kabila la Wajaluo. Nyanza hasa eneo la Kisumu City huwa machafuko makubwa yanatokea kwani wenyeji wake wamekuwa wakifukuza makabila wasiyotaka pamoja na kuchoma maduka ya wahindi. 
Kule Nyanza Province Wahindi ni wahanga wa kwanza wa machafuko kwani maeneo yao ya biashara yamekuwa yakiharibiwa sana. Imekuwa hivi kwa miaka mingi na sasa Wahindi hawa wanaona ufikapo uchaguzi ni nyakati zao za kufunga biashara kwa wale wenye uwezo wanahama kabisa Kenya yetu.
Wengine huenda huko India na wengine huishi nchi za kigeni kwa muda na uchaguzi ukimalizika kwa amani wanarejea. Eneo jingine ni Eldoret ambalo lipo Western Kenya. Kwanza hapa huwa na hali mbaya zaidi. Hapa Eldoret inasemekana kuna watu wamekusanya silaha na kujiandaa kwa mapigano baada ya uchaguzi Machi 4. Sio Al Shabab wala magaidi wowote bali ni watu wa kabila la Kalenjin wanasemekana kuhifadhi silaha kuwadhuru makabila mengine baada ya uchaguzi iwapo kutakuwa na ukosefu wa amani.

Martha Karua
Haya maeneo mawili Rift Valley Province na Nyanza Provine yanakuwa na machafuko sana, inatia hofu sisi wananchi wa Kenya namna gani tutaweza kuishi. Wakenya wenyewe hawapo tayari kuona wanamaliza uchaguzi halafu wanaingia kwenye machafuko kama mwaka 2007 baada ya uchaguzi. Hatupo tayari kuwa na machafuko ila kwa dalili zilizopo inatia hofu hatima ya uchaguzi itakuwaje mwaka huu. Kingine ni hata wagombea kuamiani kuwa kutegemea makabila yao ndio siri ya ushindi, huku wakisahau inaleta picha mbaya na kusababisha machafuko.

Raila Odinga anawafuasi wengi na anategemewa kushinda uchaguzi. Uhuru Kenyatta ndiye anampa ushindani mkubwa manake ‘ruuning mate’ wake William Ruto hushawishi Wakalenjin wenzake kumuunga mkono Uhuru Kenyatta. Ruto hatumii sera ya kushawishi kwa Wakalenjin bali anatumia ukabila wake ili kuwashawishi Wakalenjin waweze kumchagua Uhuru Kenyatta. Mimi natokea kabla la Luhya, lakini kura yangu iko wazi nitampa Uuru Kenyatta na ‘running mate’ wake Willaim Ruto ili waweze kushinda bila kujali, Uhuru ni kabila la Embu na Ruto kabila la Kalenjin.

Sisi Luhya tunatokea eneo la Western Kenya kama nilivyosema kuhusu Nyanza Province na hofu ya machafuko. Raila Odinga anazo sera nzuri kwa wakenya, lakini Uhuru Kenyatta anaweza kumtisha kwani ameleta sera ambayo itamfanya aungwe mkono na wasomi wengi wa Kenya, kuanzia wanafunzi wa vyuo vikuu, wahadhiri, na watu wa sekta ya elimu kwa ujumla.
Uhuru Kenyatta atapata kura yangu sababu ameahidi akishinda ataondoa Parallel Program kwa University ili wanafunzi wote waliofuzu walipe pesa sawa. Parallel program ni mwanafunzi ambaye hakupata alama B ya pointi 61 lakini anafuzu kuwa University anajilipia zaidi ya laki moja kama karo chuoni. Kwa sera hii Uhuru Kenyatta anapata kura yangu na atafanikiwa kupata kura nyingi za watu wa sekta ya elimu kwani atawaondolea ubaguzi wakenya katika elimu.

Wengi wanakosa kulipiwa karo sababu hawana alama Ba, hivyo hujilipia kiasi cha pesa wenyewe chuoni. Ninaamini Raila Odinga anaweza kushinda uchaguzi huu, ingawa wakati uliopita tuliamini na hakushinda kwani ilisemekana Mwai Kibaki aliiba kura.
Lakini ushindani anaotoa Uhuru Kenyatta si uchwara kwani amekuwa mwerevu kuelezea makusudio yake pindi akiingia madarakani, ambayo yanaonyesha kabisa kuwaunganisha wakenya.
William Ruto
Kuna jambo lingine limejitokeza siku chache zilizopita kabla ya uchaguzi ambalo linatia hofu ya machafuko. Kama kura zinaibwa maana yake itachochea machafuko, mfano juzi gari ya Mkuu wa IEBC (Electoral and Boundaries Commission), Isaac Hassan alipigwa risasi, uzuri hakuwa ndani hivyo hilo nalo linaashiria kuna mambo yatajitokeza baada ya uchaguzi hasa hawa Wakikuyu na Kalenjin wanapenda fujo na hawajawahi kuelewana.

Sasa ukiangalia mapigano ya Tana River, watu 140 wamekufa sababu za kikabila na kugombea mifugo. Halafu hali mbaya ya mji wa Garrissa mpakani mwa Somalia na hapa Kenya, kisha miji ya Kisumu na Siaya pamoja na eneo la Kibera mjini Nairobi, ni dalili za wazi kuna mambo uchaguzi ujao.Ni eneo la Kiberra kule Nairobi ndipo machafuko yalipoanzia mwaka 2008, tunakumbuka hili na Wakikuyu walikuwa na chokochoko dhidi ya Wakalenjin. Mzee Daniel Arap Moi naye ni mkalenjin amekuwa akisisitiza wakalenjin waache mapigano dhidi ya wakikuyu lakini hakuna dalili za kumaliza suala hili.

Moi anakula pensheni yake ya randi milioni 2.5 sawa na pauni 175,000 anamuunga mkono Musalia Mudavadi, badala ya Uhuru Kenyatta ambaye alimuunga mkono mwaka 2002.
Kubadilika kwa Moi kumuunga mkono Mudavadi wa kabila la Luhya ni wazi ameamua kubadili mbinu za kisiasa baada ya kuona hakuungwi mkono na wagombea wengine. Moi pamoja na hotuba zake, lakini hawezi kumaliza hofu ya machafuko  baada ya uchaguzi.

Na kwakuwa nitakuwa Voters Clerk uchaguzi wa Machi 4, nadhani nitapata wasaa mzuri zaidi kuyasoma mawazo ya wapigakura na mwenendo mzima wa uchaguzi wetu hapa Kenya.
Lakini hofu kubwa itakuwa kwa wafuasi wa Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, kati ya Wakalenjin, Wajaluo na Wkikuyu. Kuna hofu ya mchafuko hapa. Kwa mfano, Februari 15, Raila Odinga alitembelea watu wa jamii ya Embu ambako ni kabila la Uhuru Kenyatta, kulitokea rabsha, kama si juhudi za Polisi, basi Odinga angetimuliwa kwani wanamtaka Uhuru Kenyatta tu.

Dorine Otinga ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton nchini Kenya na atakuwa miongoni mwa wasimamizi wa uchaguzi ujao.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako