February 19, 2013

UCHUMI NA BIASHARA: "NJIA BORA YA KULINDA BIASHARA ZAKO"

Albert Sanga, Iringa

Wiki iliyopita niliandika makala iliyokuwa na kichwa “Unahitaji gia ya uvumilivu kumudu biashara”. Kwenye makala hiyo nilieleza visa kadhaa vilivyowahi kunitokea katika harakati zangu za kibiashara. Mamia ya wasomaji kutoka pande zote za nchi wameonesha kuguswa mno na yaliyowahi kunitokea.

Wengi wamenitumia ujumbe, mfupi, wameniandikia baruapepe na kunipigia simu nyingi wakinipa pole na ushauri mbalimbali. Hata hivyo ninapenda kuutambua mchango ya msomaji mmoja ambae alinitumia meseji kwa simu. Mchango wake ndio msingi wa makala hii ya leo.
Msomaji huyu ni Mchungaji Ency Mwalukasa wa Dar es Salaam. Mch. Mwalukasa anasema, “Halo kaka ALBERT! Nimefurahia sana shuhuda za mapito katika biashara zako. Hata kwenye huduma ya MUNGU mapito ni hivyo hivyo. Nimeguswa nikushirikishe kinga na ulinzi wa mali na fedha zetu: ni kumtolea  Mungu fungu la kumi au zaidi.”

“Kwa kufanya hivi inaleta ulinzi na baraka. Malaki 3:8-12. Mungu ameahidi unapotii ni lazima atende. Au asilimia Fulani ya fedha na mali zako wape wahitaji utazidishiwa na kupokea ulinzi wa mali na fedha zako. Mtu wa Mungu ni lazima upate mafanikio ya kudumu” Mwisho wa kunukuu.

Ninapoendelea na makala haya ninasukumwa kuweka wazi mambo mawili ili nisilete migongano ya kifikra na kimaslahi. Mosi; ninapenda nitangaze maslahi yangu kiimani. Mimi ni mkristo niliyezaliwa mara ya pili. Kwa  hiyo leo ninaandika ulinzi wa biashara zetu kwa mtazamo wa tamaduni na sheria za kibiashara lakini pia kutoka katika Biblia. Pili; si lengo langu kuhubiri katika makala haya; hivyo kama nitarejea mafundisho ya kidini ijulikane kuwa ni nukuu tu za kutusaidia.

Kama alivyosema Mchungaji Ency Mwalukasa ni kweli kuwa mfanyabiashara unatakiwa kutoa fungu la kumi pamoja na sadaka nyingine. Kiimani, utoaji wa sadaka huleta ulinzi wa kiroho katika biashara zako. Ukiacha ulinzi, utoaji wa sadaka huachilia nguvu za uweza wa Kimungu katika fahamu na fikra za mfanyabiashara anaetoa sadaka; kiasi ambacho kunakuwa na mtiririko wa mawazo ya kibiashara (costant flow of business ideas), unakuwa mbunifu na unakuwa na nguvu za kuendelea mbele hata vinapotokea vikwazo kibiashara.Mimi ni msomi wa masuala ya biashara lakini pia najivunia uzoefu nilionao na ninaoendelea kuupata kwa kufanya biashara kwa vitendo. Hata hivyo; kule madarasani na kwenye vitabu vya biashara kuna jambo eidha linafichwa ama linapuuzwa. Jambo hili ni nafasi ya Mungu katika kumfanikisha mtu kibiashara.

Watu wanapofundishwa masomo ya biashara hawaambiwi kuwa ukitaka kuwa na mafanikio ya kweli ni lazima uanze kuimarika kiroho (spiritual mindset). Mimi kamwe sitaacha kuitaja na kufundisha wazi nafasi ya Mungu katika mafanikio ya watu.
Kwa sababu kama tukiwaficha watu kuhusu Mungu tutakuwa tunajenga mafanikio yasiyo ya kudumu. Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa, “Mtu yeyote anayepata mafanikio ya kifedha ama mali, ikiwa hajaijenga roho yake kwa kuwa na uhusiano mzuri na Mungu; basi mtu huyo ameuchuma msiba”

Pengine changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi ni namna gani ya kutoa hizi sadaka. Mathalani, sadaka ya fungu la kumi ni asilimia kumi ya faida unayoipata katika biashara. Sasa, utajuaje asilimia kumi ya kumtolea Mungu ikiwa haujui unapata faida ya shilingi ngapi kwa wiki, kwa mwezi, au kwa mwaka?

Asilimia kubwa ya wajasiriamali na wafanyabiashara nchini wanaendesha biashara kienyeji na kwa kubahatisha. Wengi hawajui ni faida gani anazalisha kwa wiki, mwezi au mwaka na hili linatokana na kutokuwa na utamaduni imara wa kutunza kumbukumbu.. Jambo hili ni hatari sana linapokuja suala la kumtolea Mungu sadaka; kwa sababu utajikuta eidha unamwibia Mungu au unamuongezea unapotoa sadaka. Ni heri ukamzidishia Mungu kuliko kumwibia!

Binafsi nilijifunza mapema sana uhusiano uliopo kati ya sadaka na mafanikio ya mtu kibiashara. Kitu ambacho kilinitesa kwa muda mrefu sana ilikuwa ni namna ya kujua nimtolee Mungu kiasi gani; kwa sababu biashara nyingi nilikuwa nazifanya kimazoea, kwa kukisia. Nilipokuwa nachanganyikiwa zaidi ni pale inapotokea faida imerudi ‘juu kwa juu’ katika mzunguko na ikaongezea kwenye mtaji.

Unapofika muda wa kutoa sadaka nabaki nimechanganyikiwa maana sielewi mtaji ni kiasi gani na faida ni shilingi ngapi kwa muda gani. Huenda hata mimi nilikuwa mmoja ya watu waliokuwa wanamwibia Mungu sadaka. Lakini kwa sasa nimepata mwarobaini. Nilikuja kubaini kuwa biashara ili zifanikiwe na ukitaka usigombane na Mungu wako kwa “kumdokolea” sadaka; ni vema kuendesha biashara katika mifumo rasmi.

Ndipo nilipoamua kusajili kampuni ambapo biashara zangu zote ninaziendesha kikampuni. Uzuri wa kufanya biashara katika mifumo rasmi ni kwamba; unalazimika kuwa na utaratibu wa uendeshaji biashara, utunzaji wa kimahesabu na mipango ya biashara iliyochambuliwa (business plan). Pale kwenye kampuni huwa ninapata fedha kwa njia mbili. Mosi; ni kupitia mshahara ninaolipwa kila mwezi. Pili ni gawio la faida inayotokana na mchanganuo wa idadi ya hisa ninazomiliki.

Nimetaja habari ya mshahara ninaolipwa kila mwezi. Wengine wanaweza kushangaa kidogo, inakuwaje kampuni ya kwangu halafu tena ninalipwa mshahara? Hapa ndipo ambapo wajasiriamali wengi huwa wanateleza. Unapokuwa na biashara hata kama iwe ndogo kiasi gani, unatakiwa uwe unajilipa mshahara kiwango maalumu na sio kutumia faida ama fedha ya mtaji kadiri unavyojisikia.

Sasa linapokuja suala la sadaka sisumbuki. Katika ule mshahara ninaolipwa (ama uite ninaojilipa) kila mwezi ninatenga fungu la kumi na kumalizana na Mungu. Vile vile inapokuja suala la gawio la faida za hisa, iwe faida itarudi kukuza mtaji ama nitaichukua; ni kwamba kabla ya chochote ninatenga asilimia kumi na ninamalizana na Mungu. Hii nimeona inanisaidia sana na niwe muwazi; ninauona ulinzi wa Mungu katika biashara na mipango yangu mingi.

Ninapoeleza habari za sadaka na mafungu ya kumi mtu anaweza kusema, Huyu Sanga mbona analeta habari za kiroho hapa? Kwa taarifa yako ulinzi wa biashara zetu kwa njia ya sadaka unatajwa hata katika sheria na taratibu za biashara.

Waanzilishi wa sheria na taratibu zote zinazotumika katika biashara duniani pote ni Waingereza. Wao katika sheria hizi wanashauri na kulazimisha kuwa biashara inapozalisha faida; ni vema ikarudisha sehemu ya faida yake kwa jamii inayoizunguka. Faida hii ndio sadaka. Tena mjasiriamali usisubiri mpaka uwe na mamilioni ili kutoa sadaka. Anza na hiyo faida ndogo unayozalisha hata kama ni shilingi mia tano, toa!

Biashara yako inapowasaidia watu kuna mambo mawili yanatokea. Mosi; biashara yako inakaa akilini na mioyoni mwa watu kwa hiyo unaendelea kuwa na wateja waaminifu. Pili; biashara yako inakuwa inaheshimika na jamii unayoisaidia kwa sababu wanajua kuwepo kwa biashara yako ndio kupona kwao hivyo watailinda kwa nguvu zote.

Pamoja na juhudi zetu za utaalamu na kanuni za kuzingatia kibiashara, mjasiriamali usisahau kuwa njia bora ya kulinda biashara zako ni wewe pamoja na biashara yako kumtolea Mungu sadaka, kuwasaidia wahitaji na kupeleka sehemu ya faida kuongeza thamani za maisha ya jamii inayokuzunguka.

Wajasiriamali tunahitaji ushindi
0719 127 901, stepwiseexpert@gmail.com

No comments:

Post a Comment

Maoni yako