February 19, 2013

TAKUKURU NA MAHAKAMA YA UHUJUMU UCHUMI


Markus Mpangala

Na Markus Mpangala
“Katika kesi nyingi za rushwa, zimekuwa zikilalamikiwa sana na wananchi na kwa kuliona hilo mara zote nimekuwa nikimshauri Jaji Mkuu, Othman Chande kuanzisha Mahakama Maalumu za kesi ya rushwa kama ilivyo Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki,”.
Hayo ni maneno ya Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah akizungumza wakati wa Mafunzo ya Walezi na wenyeviti wa klabu za wapinga rushwa jijini Dar es salaam.
Dk. Hoseah ameibua hoja niliyowahi kuwasilisha baada ya mahojiano yangu na Hakimu Ambroce Nkwera, siku chache tu baada ya kuajiriwa kuwa hakimu wilayani ya Mbinga, mkoani Ruvuma.
Mahojiano hayo yalitokana na kuibuka wka tuhuma za rushwa wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini uliowasilishwa bungeni  kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, na kutawaliwa na tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge katika Kamati ya Bunge  ya  Nishati na Madini.
Katika mjadala huo Wizara ya Nishati na Madini na Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi, walifichua mambo mbalimbali ya ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya wabunge kupitia kamati zao, ambayo baadaye yalishindwa kuthibitishwa kutokana na Kamati ya Ngwilizi kuwasafisha wabunge waliotuhumiwa.
Hakimu Ambroce  Nkwera ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, alieleza kwa kina juu ya mchakato wa kuanzisha Mahakama maalumu ya rushwa ambayo aliita Mahakama ya Wahujumu uchumi. Nini alichosema wakati huo na ambacho kinasadifu tamko la Dk. Hoseah,  fuatilia mahojiano haya;-
SWALI: Ndugu Ambroce Nkwera, shutuma za kupokea rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge, bila shaka umezisikia. Kuna Kamati za Bunge zinalalamikiwa kwa vitendo vya rushwa, mfano Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC). Nini tafsiri yako katika suala hilo?
JIBU: Nimesoma taarifa nyingi kuhusiana na shutuma hizo. Kimsingi hizo ni shutuma, kwahiyo kuna mamlaka zinazohusika na ufuatiliaji wake. Mathalani Spika wa Bunge, Anna Makinda amewasilisha suala hilo mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi.
Spika ametumia madaraka ya kupeleka suala hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1). Sasa kumbuka ile ni kanuni ya 53(2) na 58(3)(f) inasema malalamiko juu ya vitendo vya rushwa kwa baadhi ya Kamati za Bunge na wabunge, lazima Spika atumie kanuni hizo.
Siyo hapo tu, Spika wa Bunge anayo madaraka ya kuvunja kamati inayotuhumiwa ama kama zipo nyingi zinazotuhumiwa zitavunjwa. Sikushangaa Spika alipoiagiza Kamati ya Ngwilizi kutengeneza code of ethics ili mbunge yeyote atakayetuhumiwa, hatua dhidi yake zichukuliwe.
Sasa, tunachoona ni matumizi ya ile kanuni 113(3) inayompa madaraka Spika kuvunja kamati zinazolalamikiwa kwa vitendo vya rushwa. Hapo Kamati ya Nishati na Madini ikavunjwa. Kwahiyo uchunguzi unaofanywa na Kamati ya Ngwilizi, utatupa majibu.
SWALI:Umeeleza kanuni za Bunge zilitumika kuvunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Nini mtazamo wako kwa ujumla katika suala la vitendo vya rushwa bungeni?
JIBU: Mimi, nimeshtushwa kama watanzania wazalendo wengine. Napata wasiwasi sana na hii nchi mwisho wake itakuwaje, na siyo mwisho tu bali hali ya maisha itakuwaje kwa watanzania.
Hivyo ni hofu ya kila mmoja, ingawa ni kipindi cha mpito, ninayo hofu eneo la muhimili wa pili wa dola limeingiliwa na ubadhirifu. Lazima tutafute njia za kukomesha hilo. Na hilo lisiwe interim decision maana athari zinaweza kushamiri kwa wananchi.
SWALI: Umedokeza suala la interim decision, unasema iepukwe, nini unachokusudia au unachomaanisha hapo?
JIBU: Ok! Nazungumzia uamuzi wa mpito. Hii interim decision ni mbaya, usifikiri kutafuta suluhisho na  kukomesha ubadhirifu kwa tafsiri ya kushutumiwa baadhi ya wabunge, hata sekta zote wapo na wanatakiwa kutafsiriwa ni wala rushwa. Suluhisho la muda mfupi hatuwezi kufanikiwa hata kidogo kwa suala la rushwa.

SWALI: Unadhani wananchi wanachukulia uzito wowote katika suala la tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge?

JIBU:Huu sio wakati wa mwaka 1947. Uzito upo siyo lazima wananchi wapayuke, kwamba mtu afike barabarani aanze kusema nakerwa na rushwa ama inakera wabunge kutuhumiwakwa  vitendo vya rushwa.
Matokeo yake unaweza kuyaona katika uchaguzi, nadhani patakuwa na mabadiliko bila kujali chama. Natoka kusoma taarifa zao hapa, nashauri kwa kurudia hii sio interim decision, tuwe au tuanzishe Mahakama za wahujumu uchumi, mimi nadhani zitakuwa na msaada sana katika haya mambo ya rushwa.

SWALI: Kwanini Mahakama ya uhujumu uchumi. Muundo wa Mahakama hiyo utakuwaje, sababu tunazo mahakama zinazofanya kazi vizuri tu?

JIBU:Katika Mahakama Kuu kuna kitengo au division ya biashara, division ya kazi na wangeanzisha kitengo cha ku-deal (kushughulikia) na economic embezzlement, kwenye nchi nyingine zipo mahakama hizo, zimefanikiwa sana. Na hapa hilo linawezekana tukiwa na dhamira ya kukomesha rushwa nchini. Dhamira tu ndio msingi.

SWALI: Hebu, kabla hujaendelea,  ina maana katika mahakama za kawaida, hatuwezi kuwafungulia mashtaka hao unaosema wahujumu uchumi?

JIBU: Kama nilivyosema mwanzo, suala la mgawanyo tu hapa, kama ipo division ya kazi na biashara, basi nayo ujuhumu uchumi iwe division peke yake. Sasa, mahakama za kawaida siyo vibaya ila tupanue mitazamo yetu. Mimi naona wahujumu wana uwezekano wa kushinda kesi mahakama za kawaida.
Kwanza sheria yenyewe haiweki nguvu au adhabu kali kwa tafsiri zangu za uhujumu uchumi. Mifano ipo, na mimi natafsiri ni uhujumu uchumi, kuna mifano ya watu ambao wamefungwa jela kwa miaka michache kutokana na sheria zetu, hasa  kwenye mahakama za kawaida.

SWALI: Kwahiyo, hapa tatizo ni kushinda kesi na kiwango cha adhabu tu, na pia hizo sheria haziwezi kuboreshwa na kutumika mahakama za kawaida?

JIBU: Naongelea sheria inayowahukumu watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na adhabu zake. Mahakama za kawaida naona wengi wanapata adhabu ndogo. Ingawa ni adhabu lakini bado tunahitaji kukomesha rushwa, na maana ya kukomesha ni pamoja na kutoa adhabu kali, hivyo  na sheria za ku-deal  na wahujumu zipatiwe mahakama yake. Hata zile sheria za zamani alizotumia Sokoine (Waziri Mkuu, Edward Sokoine), tutumie na kuongeza kulingana na mazingira ya sasa na huko mbele, tutengeneze sheria na mahakama za kukomesha wala rushwa, wanazorotesha nchi.
SWALI: Unasema sheria za kushughulikia  wahujumu uchumi zipo. Ni sheria gani hizo?
JIBU: Kuna hii Economic and Organized Crime Act, lakini sijui kama hasa wanatumia, kwani ni sheria ya zamani sana. Pia hii nyingine ya Penal Code inaweza kutumika. Lakinitukisema economic and organized crime Act, inabidi ujue sheria hiyo ilikuwa inatumika sana wakati wa Rais Julius Nyerere, ni hiyo iliyotumiwa pia na WaziriMkuu, Edward  Sokoine kuwashika walanguzi na wahujumu uchumi.Hivyo utaona kuwa tuanzie pale alipoishia mzee Sokoine.
Lakini Penal Code wahujumu wanakuwa wanapelekwa tu katika mahakama za kawaida. Mimi naona haitoshi kabisa kukomesha suala hili, napendekeza lazima tufanye jambo dhidi ya wahujumu, nasisitiza lazima tumrejee Sokoine kutengeneza njia mwafaka kukomesha wala rushwa.
Spika wa Bunge Anna Makinda
SWALI: Lakini, unadhani tunao Majaji wa kutosha kuhudumia Mahakama ya uhujumu uchumi au tuanze mchakato mpya wa mafunzo mapya yao?
JIBU: Siyo kweli kwamba Majaji hawatoshi, labda tufahamishane, majaji wapo, nahawa wana weledi tofauti kwenye taaluma hii ya sheria. Kwahiyo, wale majaji wenye weledi wa mambo ya uchumi watapewa eneo hilo, na jukumu lao litakuwa mahakama ya wahujumu uchumi.
Ni mpango wa kimkakati na kiutendaji zaidi, na hapa tusizungumzie vikwazo kwamba hatuna fedha, bali tujikamue kadiri tuwezavyo. Mfano, serikali yetu imeonyesha pesa zipo za kutosha linapokuja suala nyeti, angalia kama kwenye Tume ya kukusanya maoni ya wanachi kupata Katiba Mpya inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, wana nyenzo za uhakika, dhamira imo serikalini, labda tutapata katiba mpya.
Lakini siamini kama suala la mahakama hii itatufanya tushindwe sababu ya fedha. Tuweke dhamira tu, yote yanawezekana. Zipo nchi zinawashughulikia ipasavyo wahujumu uchumi, nazo zilikuwa na dhamira mbali ya majaji wachache kama tatizo lilikuwepo au la.
Mfano tufanye comparison (tulinganishe) hapa na nchi za China, Thailand, Marekani, Uingereza au Scotland tuone wanawafanya nini wahujumu uchumi ili nasi tuwe na mwarobaini wa kukomeshwa rushwa. Angalia, mfano kule Thailand ulimuona Thaksin Shinewatra, alikuwa waziri mkuu wa nchi ile. Lakini akituhumiwa na kufunguliwa mashtaka ya vitendo vya rushwa.
Hapa lazima tuelewe hawa PCCB ya bwana Edward Hosea (Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini) ndio wanajua suala gani au kesi gani ni ya aina ya uhujumu. Yupo DCI, Manumba, hivyo wale wengine kule kwa DPP anakuwa tayari amepelekewa kesi inayopaswa kwenda Mahakama ya uhujumu uchumi, ikiwepo.
Sio hilo tu, hapa tunataka pia watu werevu, well trained katika PCCB ili tusiharibu mpango wenyewe. Lazima tuwe na mahakama hizo kila kanda ya nchi yetu. Uhujumu ni janga baya sana kwa nchi, haya yanayotokea ni kilelezo cha jamii. Tuchukue hatua, hatuchachelewa.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako