August 15, 2013

DRFA KUENDESHA SEMINA KLABU ZA LIGI KUU NA DARAJA LA KWANZA


Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kitaendesha semina ya siku moja kwa klabu 11 za Mkoa wa Dar es Salaa zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara ili kuboresha weledi na hatimaye kufanya vizuri.
Mada zitakazotolewa katika semina hiyo ni sheria 17 za mpira wa miguu, majukumu ya benchi la ufundi na jinsi ya utoaji habari kwa klabu.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo semina hiyo imepangwa kufanyika Agosti  18 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa.

Washiriki wa semina hiyo ni Mameneja wa timu, kocha, nahodha wa timu na Ofisa Habari kutoka katika klabu hizo.
Klabu hizo za Mkoa wa Dar es Salaam zitakazoshiriki semina hiyo ni Simba, Yanga, Azam FC, Ashanti United, African Lyon, Villa Squad, Trans Camp, Police Central, Green Worriors, Tesema na Friends Rangers.

Watoa mada katika semina hiyo watakuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sunday Kayuni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Omari Kasinde na Ofisa Habari wa TFF,  Boniface Wambura.

Mgeni rasmi katika semina hiyo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadik.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako