August 15, 2013

JESHI LA POLISI LAANZA OPERESHENI MAALUMU


Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
Jeshi la Polisi nchini limewaomba wananchi kuimarisha na kulinda amani na usalama kwa kuwafichua wahalifu wa aina yeyote wakiwemo wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakilisumbua jeshi hilo. 

Kwa mujibu wa Msemaji wa jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema kuwa uamuzi wa Jeshi la Polisi kuwaomba wananchi washiriki katika zoezi hilo ni kutimiza amri ya Rais Kikwete ambaye alitoa siku 14 kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinawakamata wahalifu na wahamiaji haramu pamoja na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria hususani maeneo ya mipakani. 

“Jeshi la Polisi linasisitiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama nchini wawe tayari kuwafichua wahalifu wa aina yeyote ile wakiwemo wahamiaji haramu kwa vyombo vya dola au mamlaka yoyote ya serikali, wananchi wasikubali kuwahifadhi wahamiaji haramu na  watoe taarifa wawaonapo wakiingia kwenye maficho maarufu kama njia za panya,” alisema Senso.
Aidha, msemaji huyo aliongeza kuwa ni lazima jamii ihamasike kulinda amani na usalama, pia Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola limepanga kuendesha operesheni maalumu ya kuwabaini na kuwamata watu wote wanaokiuka sheria au kuhatarisha ulinzi na usalama hapa nchini

“Tunawaomba wananchi washirikiane na vyombo vya dola, hii itsaidia  nchi yetu kuendelea kuwa salama, hususani wananchi waishio mipakani. Baada ya siku kumi na nne alizotoa Mhe. Rais kumalizika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitaendesha operesheni kali ya kuwabaini ikiwemo wanaomiliki silaha kinyume  cha sheria,”

No comments:

Post a Comment

Maoni yako