Na Olle Bergdahl Mjengwa, Sweden
MSOMAJI,
mchezaji anayewashangaza wengi msimu huu ni mchezaji maarufu wa Atletico
Madrid, Diego Costa.
Nikiandika
makala hii, Diego Costa amefunga mabao nane katika mechi saba katika ligi ya
Hispania. Wiki hii mechi za kufuzu Kombe la Dunia zinachezwa.
Kinachowashangaza
wengi ni kwamba Diego Costa aliyezaliwa na kukulia Brazil, na
mwenye miaka 24 , hajawahi kucheza mechi ya mashindano dhidi ya
timu ya taifa ya Brazil.
Mchezaji
huyo ameishi Hispania tangu mwaka 2007. Ana uraia ya Kihispania pia. Kwa
hiyo, mchezaji huyo anaweza kuichezea timu ya taifa ya Hispania.
Sheria
za FIFA zinasema mchezaji akicheza mechi moja ya ushindani na timu moja
ya taifa, mchezaji huyo atabidi kuichezea timu hiyo katika kipindi chake chote
cha kucheza mpira. Lakini, Diego Costa amecheza mechi moja tu na timu ya taifa
ya Brazil na ilikuwa mechi ya kirafiki dhidi ya Italia mwaka huu. Kwa
hiyo, Diego Costa bado hajacheza mechi ya ushindani na Brazil, na kwa hiyo
anaweza kuichezea timu ya taifa ya Hispania.
Lakini,
chama cha soka cha Brazil hawataki Hispania kumwita Diego Costa kucheza mechi
za kufuzu Kombe la Dunia akiwa na Hispania. Diego Costa alipata uraia wa
Hispania mwaka huu, lakini chama cha soka cha Brazil wanaamini mchezaji huyo ni
Mbrazili na wamewambia FIFA kwamba Costa hajacheza mechi ya ushindani na timu
ya taifa ya Brazil kwa sababu hawana mechi za kufuzu kwa kuwa fainali za
Kombe la Dunia zitachezwa Brazil mwakani.
FIFA
wameamua kwamba Diego Costa hata ruhusiwa kucheza mechi za kufuzu fainali
za Kombe la Dunia wiki hii na wiki ijayo, na haruhusiwi kuichezea timu ya
taifa ya Hispania wala ya Brazil mpaka FIFA wakimaliza utafiti juu ya suala
hilo, na hivyo wataamua kama Diego Costa anaruhusiwa kuichezea timu ya taifa ya
Hispania au hapana.
Vyombo
vingi vya habari vinaamini kwamba FIFA watamruhusu Diego Costa kuichezea timu
ya taifa ya Hispania, na kwamba mchezaji huyo amemwambia Del Bosque,
kocha wa timu ya taifa ya Hispania kwamba anataka kuichezea timu hiyo. Bila
shaka, Hispania wanahitaji mchezaji kama Diego Costa. Timu ya taifa ya Hispania
kwa muda mrefu hawajakuwa na mshambuliaji anayefunga mabao mengi
katika timu ya taifa na timu ya klabu.
Hispania
wamebaki na mechi mbili tu za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Na wana
nafasi kubwa kuchukua nafasi ya kwanza katika kundi lao, hivyo,
watafuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Lakini, Costa atakosa mechi
hizi. Hata hivyo, naamini kwamba kama Costa ataendelea kuwa katika hali nzuri
ya kimpira, basi, mchezaji huyo atachukua nafasi katika kikosi cha kwanza cha
Hispania kama anaruhusiwa kuichezea timu hiyo.
Brazil
na Hispania walikutana katika fainali ya kombe la mabara mwaka huu. Hispania
walifungwa mabao matatu kwa bila. Labda Hispania na Brazil watakutana katika
fainali ya Kombe la Dunia mwakani. Del Bosque anajua kwamba kama Diego Costa
anaichezea timu yake, basi, Hispania watalipiza kisasi.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako