Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ILI kujenga jamii bora na yenye
kujua tamaduni zao, kunahitajika kuandaliwa matamasha muhimu yenye dhamira ya
kweli katika kona mbalimbali za nchi yetu. Huo ni mpango mzuri na wenye tija.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo
Rweyemamu, pichani.
Katika suala hilo, wale wadau
wanaotarajia au waliowahi kuandaa matamasha ya aina hiyo ni dhahiri wanatakiwa
waungwe mkono badala ya kukatishwa tamaa.
Kwa sasa, tamasha ambalo linatajwa
katika vinywa vya watu wengi ni lile la Handeni, linalotarajiwa kufanyika
Desemba 14, wilayani Handeni mkoani Tanga.
Tamasha hilo la utamaduni na michezo
linatambulika kwa jina la ‘Handeni Kwetu,’ jina lililotokana na mtandao ‘blog’
ya Handeni Kwetu.
Mratibu wa Tamasha la Handeni, Kambi
Mbwana, pichani.
Vyovyote litakavyotajwa na wadau wa
matamasha duniani kote, ili mradi linatimiza na kutoa majibu halisi ya namna ya
kutangaza na kukuza utamaduni wa Tanzania, si vibaya na njia ya kulitangaza
mbele ya jamii.
Katika mazungumzo yaliyofanyika
mapema wiki hii, mwishoni mwa wiki iliyopita, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo,
Kambi Mbwana, anasema kuwa lengo la kuandaa tamasha hilo ni kushirikiana na
serikali na wananchi wote kujua mbinu imara za kuutangaza utamaduni wetu.
Mbunge wa Handeni na Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dkt Abdallah Kigoda, pichani.
Anasema kwa maeneo kama Handeni na
kwingineko, kumekuwa na changamoto kubwa za wananchi kuacha utamaduni wao na
kufuata wa wenzao jambo linalotakiwa lipingwe vikali.
“Nilikaa chini na kutafakari namna
gani ya kuwaunganisha watu wote katika tukio moja na kuwa sehemu ya wao
kuangalia ngoma zetu, nyimbo zetu na mbinu za kijamii kwa ujumla wake.
“Naamini katika umri wa taifa letu
la Tanzania, kuna mengi yametokea na yaliwahi kutokea hasa wakati wa ukoloni,
hivyo naamini siku hiyo tutajua ni kiasi gani watu wa asili ya Handeni walikuwa
na mchango kwenye jamii yao,” alisema Mbwana.
Mbwana ambaye ni mwandishi wa habari
na mmiliki wa ‘blog’ ya Handeni Kwetu (www.handenikwetu.blogspot), anasema
kwamba kwa kukutana watu wote ni sehemu ya kuangalia namna ya kulitumikia taifa
letu la Tanzania na kubuni mbinu za kujikomboa kiuchumi.
Mdau huyo wa mambo ya utamaduni,
michezo na sanaa kwa ujumla wake ukiwamo muziki, anasema kwamba Handeni ni
miongoni mwa wilaya zenye changamoto kubwa hivyo kuna haja ya wadau wote
kukutana kwa pamoja na kuangalia namna ya kuzitatua, hasa kwa kupitia tamasha
hilo.
“Huu si wakati wa kuangalia Mkuu wa
Wilaya (DC) Muhingo Rweyemamu anafanya nini au Mbunge Abdallah Kigoda na
viongozi wote wa serikali, ila jambo la muhimu ni kushirikiana nao kuleta
maendeleo.
“Mtu wa kwanza katika maendeleo ni
mwananchi mwenyewe, hivyo naomba kuwakaribisha Watanzania na hata wale wasiokuwa
Watanzania kukutana pamoja na sisi kwenye tamasha hili,” alisisitiza Mbwana.
Aidha, Mbwana anatumia muda huo
kuwaomba wadau wote, wakiwamo viongozi wa serikali, mashirika na kampuni
kujitokeza kudhamini tamasha hilo litakalokuwa la aina yake. Tamasha la Utamaduni la Handeni
Kwetu linafanyika kwa mara ya kwanza, likipangwa kuanza saa tatu asubuhi hadi
saa 12 jioni, ambapo vikundi mbalimbali vya sanaa vitashiriki.
Ili kuleta hali ya kimkoa, Mbwana
anasema juhudi zinafanyika kupata vikundi katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa
Tanga ili kuimba nao, kucheza nao na kushiriki nao katika jambo la kimaendeleo. Mdau huyo wa habari anasema kwamba
hadi sasa wadau kadhaa wamejitokeza kudhamini tamasha hilo linalotikisa katika
maeneo ya Handeni na Tanzania kwa ujumla.
Anawataja wadau hao kuwa ni pamoja
na Yusuphed Mhandeni, ambaye ni Mchumi wa CCM Kata ya Makumbusho kwa kupitia
Kampuni yake ya Yusuphed Trans, yenye magari yanayotoka Dar es Salaam kwenda
Mkata, wilayani Handeni, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa
Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist,
Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group.
Wengine ni duka la mavazi la Chichi
Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa
kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason
Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu.com.
Mbwana anasema kwamba kwa kupitia
tamasha hili, wadau wote watapata fursa ya kutangaza biashara zao, ukizingatia
kuwa tamasha hili linatarajia kukutanisha watu wengi zaidi sehemu moja. “Tunaomba udhamini kwa watu wote ili
tushirikiane katika kufanikisha tamasha hili la kihistoria, huku tukiamini kuwa
wenzetu wa Kilindi, Korogwe tutakuwa nao pamoja.
“Maandalizi yanaendelea kuhakikisha
kuwa tunafanya kitu cha tofauti katika tamasha hilo, nikiamini kuwa mguso huu
utaendelea kushika kasi na habari hizi njema kuenea nchini kote,” alisema. Mbwana anasema kwamba wazo la
kufanyika kwa tamasha hilo limepewa baraka na viongozi wote, akiwamo DC
Rweyemamu na Mbunge, Abdalah Kigoda, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na
Biashara.
Anasema kuwa kwa kufanyika kwa
tamasha hili ni muendelezo wa mipango mingi mizuri ya kimaendeleo
itakayoandaliwa kwa kushirikiana na Watanzania wote, hususan wananchi wa Handeni. Mwisho kabisa Mbwana alitumia muda
huo kuwakumbusha wafanyabiashara mbalimbali wilayani Handeni na Tanga kwa
ujumla, kuingia moja kwa moja katika tamasha hili la aina yake.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako