November 15, 2017

TANZIA

Ilikuwa runununi, 
Saa kumi za jioni,
Ni jumatatu mwanzoni, 
Wiki ilipoanzia.

Kwa ujumbe wa majonzi, 
Denisi kashusha pumzi,
Kanijulisha mpenzi, 
Ndugu yetu katufia.
 
Mnenaji alinena, 
Si usiku ni mchana,
Tumepoteza kijana, 
Songea kaniambia.


Namtumbo kaumia, 
Maumivu kumjia,
Mwikinimwe kaumia, 
Mshituko kumjia.


Pikipikini kanguka, 
Nao mwili kuchunika,
Damu zikamchuruzika, 
Fahamu memkimbia.

Akawa yu mahututi, 
Pumzi vema havuti,
Akabaki kama mti, 
Unaojiangukia.

Kwa sautiye ya mwisho, 
Huku akitokwa jasho,
Kasema 'sifiki kesho', 
Uhai umenishia.

Japo walimkimbiza, 
Kadiri walivyoweza,
Songea wakamlaza, 
Tiba haikutimia.

Kumfikisha mjini,
Mungu wangu masikini,
Kabaki kulala chini, 
Marehemu amekua.

Baada ya kufikishwa, 
Mauti akasafishwa,
Hatima kusafirishwa, 
Hadi Lundu kwingia.

Tumeshikwa na uchungu, 
Kwa kupotewa Ndugu,
Alokuwa mlimwengu,
Katika hii dunia.

Wengi wamlilia, 
Vile wakimwangalia,
Kama amejilalia, 
Na hata wakazimia.

Kweli ametoka kweli, 
Watu walizua swali,
Na huku wakijadili, 
Ajali ilivyokua.

Imemkumba ajali, 
Ni lazima tukubali,
Amemuita Rasuli, 
Sikuze zimewadia.

Kwa kweli kijana wetu, 
Alikuwa mwenzetu,
Mwenzetu katika watu, 
Mengi tumejifunza.

Hakuwa mbinafsi, 
Kwake mweupe mweusi,
Wengi kawapa nafasi, 
Kupiga nao soga.

Utani aliupenda, 
Utani wa kijamaa,
Undugu ukakomaa, 
Ucheshi hakuuacha.

Leo miye nipo hapa, 
Na kesho nitaondoka,
Nanyi mtanikumbuka, 
Ikinichoka dunia.

Kila avumaye sana,
Wahenga waliyanena,
Siyo leo siyo jana, 
Hakawii kuungua.

Jogoo linapotuna, 
Asubuhi likanena,
Usidhani litapona, 
Watu watajichinjia.

Nguo iking'aa sana, 
Na watu wakinong'ona,
Kujadili kila kona, 
Hatimaye hufifia.

Kila avumapo papa, 
Majini akajitapa,
Wavuvi nyavu hutupa, 
Wapate kumnyakua.

Anaye kimbia sana,
Mbio za kila aina,
Na sifa akazivuna, 
Hakawi kujichokea.

Ndivyo kwetu siye jama, 
Tuwe vipi na huruma,
Na kuzama tutazama, 
Katika hii dunia.

Ni kama wavu dunia, 
Chochote hukichukua,
Pasipo kutarajia, 
Kila inapoamua.

Kweli kimeniathiri, 
Kifo cha huyu jasiri,
Mlimwengu machachari, 
Utenzi namtungia.

Hakika pale mwanzoni, 
Nilipokuwa nyumbani,
Taarifa runununi, 
Ilinipora furaha.

Mwapila mzee wetu, 
Mapadiri kahudumu,
Ni Parokiani Lundu, 
Pole kwa lilokufika.

Kengele aliigonga, 
Waumini kuamsha,
Kanisani jisalia, 
Pata nguvuye Rabana.

Mjombawe maarufu, 
Aliyejawa na utu,
Ni Walter au Metu, 
Pata nguvuye Rabuka.

Mwanakwaya machachari, 
Kwa nota ni mahiri,
Afurahisha padiri, 
Kipajiche kujiimbia.

Pumzika kwa amani, 
Hapohapo mavumbini,
Nasi tupo safarini, 
Uliko tutawadia.

Utamuona mwalimu, 
Atakupa tabasamu,
Upenuni kwa Karimu, 
Nawe atakupokea.

Mwalimu katangulia, 
Na kajipumzikia,
Uwinguni katulia, 
Nawe sasa umewadia.

Wanandugu nyumbani,
Rabi awe'ke nguvuni,
Mpungukiwe huzuni,
Na nguvu kuwajalia.

Ni mimi hapa Kalemba, 
Nayo radhi ninaomba,
Dada kaka na wajomba, 
Pele nilipokosea.

Utenzi nimeutunga, 
Msinilipe mpunga,
Msinichape na ndonga, 
Tuomboleze pamoja.

Maneno yamenitoka, 
Tamati hapa nafika,
Msamaha nautaka, 
Pale nilipokosea.

© KIZITO MPANGALA
     0692 555 874.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako