April 18, 2013

RAIS KIKWETE, RAFIKI WA WOTE NA ADUI WA WOTE.Na Mwinjilisti Kamara Kusupa, Dar es salaam
WAKATI naandika kitabu changu cha pili kiitwacho ‘Tanzania tunayoitaka,’ nilizifanyia tathmini falsafa za utawala wa marais waliopata kuitawala Tanzania yetu. Nilianza na Rais wa kwanza wa Tanganyika huru ambaye ametawala kwa muda mrefu kuliko marais wote wa nchi hii, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alitawala kwa miaka 25 tangu  Mei, 1960 tulipopata madaraka ya ndani, hadi Novemba 1985 alipostaafu na kumpisha Rais wa pili Ally Hassan Mwinyi. Nimeielezea falsafa yake ya utawala kwamba kiongozi ni lazima kwanza apendwe, pili aogopwe. 

Ndio maana wakuu wa wilaya, mikoa na makatibu wakuu wa Wizara walikuwa wakifundwa mara kwa mara mithili ya mwanamwali wa Kizaramo, ili tu wasije kukiuka miiko ya utawala wake. Enzi zake uongozi na utawala vilihesabiwa kama kitu kimoja, lakini ukweli ni kwamba iko tofauti kubwa ya uongozi na utawala, pia iko tofauti kubwa kati ya kiongozi na mtawala, hayo nimeyajadili kwa kina ndani ya kitabu.

Katika utawala wake kuna Jaji aliwahi kuachishwa kazi kwa kosa dogo la kukojoa kando ya barabara usiku. Mkuu wa wilaya au mkoa asingeweza kwenda kwenye disco au kwenda kwenye dansi labda iwe amealikwa kama mgeni rasmi wa kufungua  tamasha.
Kwenye utawala wake kiongozi au mtawala akitaka ‘kusosholaizi’ alitakiwa kwenda kwenye maeneo maalum waliyotengewa watu wa aina yake, ndio maana hapa Dar es Salaam ikajengwa ‘Leader’s Club’ ,  Kinondoni.
Lengo kuu lilikuwa ni kuwatenganisha hao wanaotawala na tabaka la watawaliwa ili isije ikatokea mtu anayetawala akajichanganya na watu wa kawaida, akazoeleka hadi ‘kuzimua’  (dilute) makali ya madaraka yake na kuondosha au kuondokewa na ‘utisho’ anaopaswa kuwa nao mtawala.
Ndiyo maana enzi zake ukubwa haukuwa kitu cha kukimbiliwa na kila mtu ama mtu yeyote yule kwasababu kuna nafasi fulani ambazo hao walioteuliwa kuzishika walilazimika kulipa gharama ya kuishi maisha tofauti na maisha ya walio wengi.
Ndiyo maana pia enzi za utawala wa Nyerere nafasi zote za kuteuliwa na Rais yaani ‘presidential appointments,’ mtu aliarifiwa mapema kwamba 'Rais anakusudia kukuteua uwe mkuu wa mkoa au waziri unatakiwa useme kama unaukubali uamuzi huo ama unasita'.
Wakati mwingine Nyerere mwenyewe alipiga simu kwa mhusika hasa ilipotokea mtu ameshinda uchaguzi na kuwa mbunge, “kumwambia nataka kukujumuisha kwenye Baraza langu la Mwaziri, nimekupigia ili useme kama unaafikiana na uamuzi wangu au unasita.”
Mtu alitakiwa kutafakari na kupima maisha ya kuwa kiongozi maisha yanayolazimisha kukosa baadhi ya vionjo kama disko, sinema, night clubs na mengine ya aina hiyo.
Kama alitaka kuendelea kuyafaidi hayo nje ya uongozi, alitakiwa kuamua lakini sio kuchanganya yote kwa pamoja. Kwa kujumlisha mengi ya utawala wake ndipo nikahitimisha kwamba falsafa yake ya utawala ilikuwa hiyo kwamba kiongozi wa Tanzania ni lazima upendwe na pia ni lazima aogopwe.

Rais wa pili Ally Hassan Mwinyi amedumu madarakani kwa miaka kumi tangu 1985 hadi 1995, wananchi walimwita jina la mzaha kwamba ni mzee Rukhsa!
Utawala wake pia ulipewa jina la utani ukaitwa utawala wa ‘Rukhsa.’ Hilo jina la mzaha alilopewa na umma lilitosha kuelezea falsafa ya Mwinyi ya utawala. Kwa kutumia vigezo kama hivyo nikahitimasha kwamba Rais Mwinyi falsafa yake ya utawala ilikuwa hiyo kwamba raia awe huru ili ajiletee maendeleo.
Lakini nilipofika kwenye utawala wa Kikwete nilishindwa kuielewa falsafa yake ya utawala.
Kwakuwa mchakato wa kutoa kitabu ulikuwa umetokea wakati Kikwete bado anaendelea na kipindi kingine cha utawala, niliamini wakati ndio utakaoifunua falsafa yake ya utawala.
Hali ya kwamba hadi sasa umma haujampa Kikwete hata jina la mzaha inaashiria kitu, bado umma haujaelewa utawala wa Kikwete ni utawala wa namna gani.
Lakini taratibu sura ya utawala wake inaanza kuumbika na kuonekana dhahiri kwa watanzania anaowatawala.
Rais Kikwete anataka kumpendeza kila mtu na kumpendeza yeyote yule atakayetokea kuwa karibu naye.
Hataki kulaumiwa na yeyote ingawaje hawezi kuzuia wale walioamua wasimlaumu.
Kwakuwa hataki lawama inapotokea kulaumiwa anakerwa hata akilaumiwa kwa mambo madogo, yanapotumika maneno yasiyomtaja kwa mazuri anakerwa sana.
Kwakuwa hapendi kulaumiwa, amejiumbia utamaduni wa kujihami dhidi ya lawama zote zinazoelekezwa kwake.
Utamaduni wa Kikwete wa kujihami unajionyesha wazi kwenye hotuba zake kwa taifa, hasa zile anazotoa kila mwisho wa mwenzi.
Kila inapotokea Kikwete kuhutubia iwe mkutano wa hadhara ama kulihutubia taifa kupitia redio na televisheni za hapa nchini, lazima aonyeshe kujihami.
Haitokei kwa Rais Kikwete kuhutubia tangu mwanzo hadi mwisho wa hotuba yake pasipo aidha kulalamika ama kujibu mapigo kwa kujitetea kuhusiana na suala fulani ambalo amelaumiwa.
Hii kanuni yake ya kutaka kuwa mwema kwa wote na kwa wakati wote siyo nzuri kwasababu haitatokea kabisa binadamu akawa na uwezo huo wa kuwapendeza watu wote na kumpendeza kila mtu.

Pale ambapo binadamu amethubutu kumpendeza kila mmoja, ameishia aidha kuwahuzunisha wote ama kuwakasirisha wote.

Kuna kisa cha mfalme mmoja aliyekuwa na washauri watatu, mshauri wa kwanza alimwendea mfalme na kutoa ushauri wake kuhusiana na tatizo fulani lililoisumbua nchi.

Mfalme alimsikiliza na kumkubalia akaja mshauri wa pili akatoa ushauri wake kuhusiana na tatizo lile lile ukatofautiana na ushauri wa kwanza, yaani ushauri alioupokea toka kwa mshauri wake wa kwanza.

Baadaye mshauri wa tatu naye alimwendea mfalme na kutoa ushauri wake ambao ulitofautiana na wa pili.
Mfalme akamkubalia bila kujali alichoshauriwa na washauri wake wa kwanza na wa pili, mwisho wa yote akajikuta amekubaliana na wote watatu lakini hakuna ushauri wowote alioufanyia kazi.
Vivyo hivyo Rais Kikwete kwa hiyo kanuni yake ya kutaka kumpendeza au kumridhisha kila mtu na kuwaridhisha wote, hatimaye atajikuta hakuna yeyote anayeridhishwa na maamuzi yake anayoyatoa akiwa kama Rais.
Kinyume chake, Kikwete atajikuta analaumiwa na kila mtu, anamhuzunisha kila mtu na kuwakasirisha wote anaojaribu kuwaridhisha.
Upo mfano hai, katika hotuba yake ya kufunga mwezi Machi 2013, Rais Kikwete amenukuliwa akisema misikiti mitatu ilimsomea ‘itikafu’ ili afe akaongeza kusema wapo watu wanaoona anawapendelea wakristo na pia wanaosema dini yake ni Islamu.
Maana ya kauli yake ni hii kwamba analaumiwa kutoka pande zote mbili wakristo na waislamu kwa sababu waumini au wafuasi na viongozi wao hawaridhishwi na namna yake ya kushughulikia masuala yenye utata.

Mbali na kanuni yake ya kumridhisha kila mtu, Kikwete anaonyesha kanuni nyingine isiyomsaidia, nayo ni kuogopa kukosea.

Kwakuwa hataki kukosea kuna mambo ambayo yanamhitaji kutoa uamuzi wa haraka na ulio mgumu lakini yeye hukwepa kufanya uamuzi mgumu ili tu asije kukosea.
Lilipojitokeza suala la wafanyabiashara na waingizaji wa mafuta ya petroli kutaka kupandisha bei ya bidhaa hiyo, Kikwete alijikuta yuko njia panda maana hali halisi ilimtaka aidha ajitambulishe  na maslahi ya walalahoi wa nchi hii na kusimama kinyume na wafanyabiashara ama kusimama na hao wachache wenye nacho kuyapuuza matakwa ya waliompigia kura.
Kwa ujanja akaepa, hakutaka kujionyesha anajitambulisha na tabaka lipi kati ya hayo matabaka mawili yanayovutana mfano wa mwamba ngoma ambaye ngozi lazima aivutie kwake.
Tatizo la matabaka ya nchi hii na maslahi ya kila tabaka mbali na kumsumbua, pia litamwelemea Rais Kikwete.
Matabaka yanamfanya awe kwenye mtihani kwa wakati wote, dalili zinaonyesha Kikwete amefeli mtihani muhimu kwa sababu hataki kuonyesha wazi wazi amejitambulisha na tabaka lipi kati ya tabaka la wachache wenye nacho na wengi wasiokuwa nacho.
Haitawezekana akajitambulisha na matabaka yote kwakuwa mnyukano wa maslahi kati ya wenye nacho wa wasio nacho ndani ya nchi moja, hauruhusu mwafaka.
Rais pekee aliyefanya uamuzi mgumu kuhusiana na tatizo la matabaka ni Nyerere peke yake, maana kupitia Azimio lake la Arusha, alijionyesha wazi kwamba ametangaza vita dhidi ya mabepari.
Ni dhahiri mazingira ya utawala wa Nyerere hayafanani na mazingira ya utawala wa Kikwete, lakini jambo moja lililomsaidia Nyerere kutokana na uamuzi mgumu, wa kuziweka njia kuu za uchumi mikononi mwa dola, aliwapunguzia uwezo wa wenye nacho.
Nyerere alidhibiti  kiburi kitokanacho na mali, kwani matajiri wote walijua wazi kwamba vitu viwili utajiri na utawala haviko sawa.

Wote walijua kuwa utawala ni mkubwa kuliko utajiri na kwahiyo utawala una nguvu kuliko utajiri.
Hali hiyo ndiyo iliyosababisha Nyerere awe Rais mwenye nguvu na maamuzi yake yasichezewe na yeyote hata yale maamuzi yaliyoonekana wazi wazi kwamba yamekosewa.
Lakini Kikwete kwa msimamo wake atataka awe rafiki wa matabaka  yote kitu ambacho ni kigumu, mwisho wake atajikuta ni adui wa matabaka yote, maskini wakiwa hawamwamini, hawamkubali wala hawaridhishwi na utawala wake kutokana na kuamini kwamba Rais hayuko pamoja nao.
Nalo tabaka la wenye nacho halitamwafiki kwa kuona halindi maslahi yao kwa namna waliyoitarajia, kwani kiburi cha utajiri kina kawaida moja ambayo inawafanya matajiri wathubutu kuielekeza serikali namna ya kuendesha nchi.
Itakapotokea serikali kutofanya neno moja tu kati ya mengi wanayoyataka wao, hapo tabaka la matajiri litaona Rais hayuko nao.
Hapo ndipo Rais atakapojikuta ameambulia uadui toka pande zote, ni adui wa maskini, ni adui wa matajiri ni adui wa wakubwa na adui wa wadogo anayelaumiwa na kila mtu.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako