SONGEA, RUVUMA
Watalii toka nje ya nchi wameanza kutembelea hifadhi ya
Asili ya Luhira iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma. Takwimu za mwaka 2016/ 2017 zinaonesha kuwa hifadhi hiyo
imepokea watalii toka nchi za Ujerumani,Afrika ya Kusini,India,Ufaransa,Italia,
Uholanzi na wageni toka mikoa mbalimbali nchini ambao pia wanafanya utalii wa
kuchunguza aina ya mimea na ndege katika hifadhi hiyo.
Msimamizi wa Hifadhi hiyo Msonda Simwanza anasema
wanajiandaa kuweka mazingira ambayo yatawezesha wanyama kama tembo,simba na wanyama
wengine adimu kuishi katika hifadhi hiyo bila kuleta athari kwa wanyama na
binadamu.
Simwanza anasema hivi karibuni Hifadhi hiyo imetumia zaidi
ya sh. Milioni 15 kuleta wanyama aina ya swalapala watano na pongo wawili toka
Hifadhi ya Arusha.
Moja ya vivutio vikubwa vya utalii katika mkoa wa Ruvuma ni
hifadhi ndogo ya asili ya wanyama inayoitwa Ruhila Natural Game Reserve yenye
ukubwa wa hekta 600 ambayo ilianzishwa mwaka 1973,ipo umbali wa kilometa saba
kutoka mjini Songea.
Ndani ya Hifadhi hiyo kuna aina mbalimbali za wanyama
wakiwemo pundamilia, fisimaji, nyani,pongo tumbili, kakakuona,swalapala na
kobe,pia bustani hiyo ni makazi ya reptilia na ndege wa aina mbalimbali. Mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga
picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kufanya
mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum.
©Albano Midelo
No comments:
Post a Comment
Maoni yako