Na Albano Midelo, Nyasa
SERIKALI kupitia wizara
ya elimu na mafunzo ya ufundi iliamua kuanzisha mfumo wa elimu ya awali katika
shule za msingi kwa lengo la kuwaandaa watoto wenye umri kuanzia miaka mitano.
Wizara ya elimu imedhamiria
kuhakikisha kuwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi sita wanasoma darasa la
awali kabla ya kuanza kuingia shule ya msingi wanapokuwa na umri wa miaka saba.
Uchunguzi uliofanywa
katika kata za Kihagara na Liuli umebaini kuwa madarasa ya awali katika shule
hizo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali hali ambayo inaathiri utoaji wa
elimu hiyo muhimu kabla ya kuanzia shule za msingi.
Wanafunzi wa Darasa la Awali wapatao 90 katika Shule ya Msingi PUULU, Kata ya LIULI, wilayani Nyasa wakiwa katika darasa ambalo halina dawati hata moja.
Mwalimu wa taaluma katika
shule ya msingi Ndonga kata ya Kihagara Amos Kilongo anasema shule hiyo ina
darasa la awali lenye wanafunzi 37 ambao wanasomea kwenye mti kutokana na
kukosekana kwa chumba cha darasa na kwamba mwalimu anayefundisha katika darasa
hilo ni aliyemaliza kidato cha nne.
“Wanafunzi wa darasa la
awali hawana darasa wanasomea chini ya mti,pia darasa halina madawati wa awali
wanakaa wakati wa mvua
wanafunzi hao wanasome katika kanisa katoliki ambalo tumewaomba wamiliki
wa kanisa hilo wamekubali kutusaidia’’,alisisitiza.
Mwalimu mkuu wa shule ya
msingi Kihagara Anet Ngindo anasema shule hiyo ina darasa la awali lenye
wanafunzi 52 ambao wanasomea chumba cha shule ya msingi wakifundishwa na
mwalimu ambaye hajapata mafunzo ya ualimu na sio mwajiriwa analipwa posho
kupitia michango inayochangwa na wazazi.
Mwalimu mkuu katika shule
ya msingi Tumbi Evaristo Ndiwu anasema
katika shule yake kuna darasa la awali lenye watoto 45 ambalo halina chumba cha
kusomea ambapo mwalimu wake hana taaluma ya ualimu ni mhitimu wa kidato cha nne
analipwa posho kutokana na michango ya wazazi na walezi.
Katika shule ya msingi
Mango,mkuu wa shule hiyo anasema katika shule yake kuna darasa ka awali lenye
wanafunzi 60 ambao hawana chumba cha kusomea na wanafundishwa na mwalimu ambaye hajapata
mafunzo ya ualimu sio mwajiriwa badala yake analipwa posho na wazazi kati ya
shilingi 30,000 hadi 50,000 kwa mwezi.
Mwalimu mkuu wa shule ya
msingi Ngehe Silivanus Mbeya anasema katika shule yake kuna darasa la awali
lenye watoto 36 ambalo halina chumba cha kusomea na linafundishwa na mwalimu
ambaye amehitimu kidato cha nne hana mafunzo ya ualimu analipwa posho na wazazi
ambayo haikidhi mahitaji ya mwalimu huyo.
Uvuvi ni shughuli inayoongeza kipato na ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa wilaya ya nyasa. hapa wavuvi wakiwa kazini.
Katika shule ya msingi
Puulu mwalimu mkuu wa shule
hiyo Cathibert Maluka anasema katika shule yake kuna darasa la awali lenye
wanafunzi 90 na kwamba wanafunzi hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali
zikiwemo na ukosefu wa madawati ambapo wanafunzi wote wanasoma kwa kukaa chini.
“Darasa la awali katika
shule yetu limebahatika kuwa na walimu wawili ambao wamepata mafunzo rasmi ya
kufundisha wanafunzi wa darasa la awali hali ambayo inawawezesha kutoa elimu ya
awali kulingana na malengo ya wizara ya elimu licha ya wanafunzi kusomea
chini’’,alisema .
Mwalimu mkuu wa shule ya
msingi Nkali Erasmus Haule anasema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 210 ina darasa la
awali lenye wanafunzi 45 ambao hawana darasa badala yake wanasomea kwenye
banda ambalo jioni linatumika kama klabu cha pombe na kwamba mwalimu
anayefundisha hajasomea.
Katika shule ya msingi
Hongi kwa mujibu wa mwalimu
mkuu Simon Ndunguru shule hiyo ina darasa la awali lenye wanafunzi 52
changamoto kubwa hakuna chumba maalum cha kusomea na kwamba mwalimu
anayefundisha sio mwajiriwa na wala hajasomea kufundisha darasa la awali.
Katika shule ya msingi
Mwongozo yenye wanafunzi 654 inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa darasa la
awali lenye watoto 81 halina sakafu lina mwalimu mmoja ambaye hana mafunzo ya
ualimu ,hajaajiriwa analipwa posho na wazazi wenye watoto hao
Baadhi ya wadau wa elimu
katika kata za Kihagara na Liuli ambao ni Neema Msumba,John Ndunguru,Joel
Makelele,Melikion Mapunda na Victor Komba wametoa wito kwa serikali kuhakikisha
kuwa kila shule ya msingi inajenga darasa rasmi kwa ajili ya elimu ya awali
badala ya shule nyingi kutumia vyumba vya shule ya msingi.
Wameitaka wizara ya elimu
na mafunzo ya ufundi kuhakikisha kuwa kila darasa la awali inapeleka walimu
waliopata mafunzo rasmi ya namna ya kufundisha watoto wa awali badala ya tabia
ambayo inafanywa na shule nyingi kuwatumia vijana ambao wamehitimu kidato cha
nne huku wakiwa hawajapata elimu ya ualimu.
Mratibu elimu kata ya
Liuli Abrahamu Challe amesema kata yake imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto
zote zinazoikabili elimu ya awali katika kata yake yenye shule saba
zinatafutiwa ufumbuzi haraka ikiwemo kuwa na chumba rasmi kwa ajili ya
awali,walimu na madawati.
Challe ametoa wito kwa
serikali kutumia mfumo wa uboreshaji wa elimu ya awali kama ilivyokuwa kwa
uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa kwa kila shule na
kusisitiza kuwa vifaa vyote vya ujenzi vitolewe na serikali na wananchi waachie
ujenzi.
Afisa elimu msingi katika
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali ambaye anahusika na wilaya ya Nyasa
anasema elimu ya awali ni sera ya wizara ya elimu kuhakikisha kila shule ya
msingi inakuwa na darasa la awali kwa lengo la kuinua elimu hapa nchini.
Ameahidi kushirikiana na
viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani,watendaji wa vitongoji,vijiji,kata,tarafa
pamoja na wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wanahamasisha wananchi katika maeneo
yao kusimamia ujenzi wa madarasa ya awali na kutengeneza madawati ili watoto
hao waweze kusoma katika mazingira bora.
“Ni ukweli madarasa ya
awali yaliyo mengi yanafundishwa na walimu wasiopata elimu ni kutokana na uhaba
mkubwa wa walimu uliopo katika shule nyingi nchini,lengo ni kuhakikisha
tunapata walimu wa kutosha ikibidi hata kuwatumia walimu wanaostaafu kufundisha
katika madarasa ya awali’’.alisisitiza.
Unaweza kuwasiliana na mwnadishi kwa anuani ifuatayo: albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129
Labda ilibidi kwanza kujenga majengo na kutafuta walimu wenye elimu na kisha kuanzisha shule...Tutafika kweli?????
ReplyDelete