Showing posts with label Hisia za moyo. Show all posts
Showing posts with label Hisia za moyo. Show all posts

March 16, 2018

FURAHA, EASTERLIN PARADOX NA MARIANO ROJAS

NA EZEKIEL KAMWAGA
 
JANA, ripoti kuhusu utafiti wa kimataifa ulioonyesha kwamba nchi yetu ina hali mbaya kwenye kigezo cha furaha kwa watu wake ilizua mjadala wa aina yake. Kuna walioupinga utafiti huo moja kwa moja kwa hoja kwamba ziko nchi zina vita wakati huu na haiwezekani wananchi wake wakawa na furaha kuliko sisi. Wengine wakapinga tu kwa sababu huwa wanapinga. Wengine wakaunga mkono kwa sababu za kisiasa tu.

Kitu kikubwa ambacho nilikiona jana ni kwamba wengi wetu tulitoa maoni kabla hata ya kuisoma ripoti yenyewe. Na hili ndilo tatizo kubwa ambalo wengi wetu tunalo. Tunapenda kutoa maoni katika mambo ambayo ufahamu wetu ni mdogo sana. Nafurahi kwamba nilijipa muda kuisoma ile ripoti jana. Hapa chini ni mawazo yangu baada ya kuisoma. Nimeyagawa mawazo yangu katika pande mbili tofauti; kabla ya kuisoma ripoti hiyo na baada ya kuisoma.

KABLA YA KUISOMA
Mimi ni muumini wa dhana kwamba furaha ni jambo gumu sana kulipima kwa mwanadamu. Nimewahi kuandika humu mitandaoni kwamba kuwa na furaha si jambo unaloweza kulipima kwa sababu ya wingi wa mali au marafiki.

February 10, 2018

‘LOCATION’ YA WANAMUZIKI WA BONGOFLEVA ASLAY NA NANDY


Unaupata wimbo unaobamba sana katika vituo vya redio, kwenye magari ya abiria, bodaboda na Bajaj wa “SUBAKHERI MPENZI” ulioimbwa na wanamuziki wawili; ASLAY na NANDY?

Sasa hii pikipiki niliyokaa ambayo inamuundo wa aina yake imetumika katika video ya huo wimbo, maana ina usukani kama gari na makorombwezo ya mfumo Wa gari. Cratch inakanyagwa kama ya gari. Subiri kile ambacho wenye maeno yao wanavyosema pale inapotokea msanii anafanya video ya wimbo au kazi nyingine ya Sanaa kama filamu wao wanavyojisikia na namna gani wananufaika kupitia Location za hizo video zinazochukuliwa.

 Honorius Mpangala,

Matimbwa, Bagamoyo

November 30, 2017

SAFARI YAO YA MAISHA


Kuna dhiki na shida. Safari yao ina milima na mabonde. Sauti zao hazisikiki kokote. Hawajui itikadi zenu bali wanatafuta shibe zao. Mazingira yao hayavutii, lakini hawachokii kuyatumia kupata matumaini na kipato. LAKINI wanaishi kwenye nchi yenye utajiri pomoni. Hawana amana benki watakuwaje na amani?  Hawana chakula nyumbani watakuwaje na utulivu?
Tafakari makuzi ya mtoto huyu....
 Tafakari mwelekeo wake na hitimisho lake. Atarudishaje faida kwa jamii iliyomtenga kiasi hiki? Nani anajali hisia zake? Nani anajali hatima yake? Nani anagusa moyo wake?
Sauti zao zisikike!

©Picha kwa hisani ya Musa Makongoro. Imepigwa katika eneo la Mburahati, jijini Dar es salaam

November 22, 2017

WEMA SEPETU NA KISA CHA J.LO

NA MARKUS MPANGALA
NIMEPATA tabu kuandika makala haya tangu kumalizika mahojiano ya mwigizaji wa filamu na mshindi wa taji la Miss Tanzania, Wema Isack Sepetu aliyofanyiwa wiki iliyopita (Mei 24/2016) na kampuni yetu ya New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya Rai, Mtanzania, Dimba, Bingwa na The African.
Mwandishi wa makala haya akiwa na mwanamitindo Wema Sepetu.
Tabu hii niliyopata ni kutokana na kuujua ukweli wa pili kuhusu maisha ya mlimbwende huyo. Ni mhariri wa Michezo wa gazeti dada na hili la Mtanzania, Mwani Nyangassa ndiye hasa aliyefanikiwa kumbana vilivyo Wema Sepetu na kujikuta akifunguka zaidi kuhusu maisha yake na mambo mengine yanayomzunguka kama msanii wa filamu, mjasiriamali na mwanasiasa na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Mambo yaliyonishtua ni uamuzi wa Wema kueleza kiundani kabisa nini kinachoyasibu maisha yake kwa ujumla kwenye filamu na maisha binafsi. Makala haya naelezea mambo ya kujifunza kwa Wema Sepetu pamoja na kisa cha Jennifer Lopez. 

December 22, 2013

UHABA WA SAMAKI



Mwandishi wetu Vitus Matembo amezoea kula samaki huko Nyasa, lakini kwa sasa analalamika kuwa kuna uhaba wa Samaki. Katika hali ya kawaida miezi ya Septemba, Oktoba mpaka Novemba kunakuwa na uhaba wa samaki wa aina fulani. Kwa wanyasa kuna samaki wanawapenda sana, lakini wanapotoweka basi inakuwa tatizo. 

Hivyo kwa sasa samaki wanaopatikana zaidi ni maarufu kama MCHUKWA, lakini samaki aina ya Kambale upatikanaji wake ni mgumu kipindi hiki labda kuanzia januari. Na kwakuwa wanyasa wamezoea kula samaki wanono basi tusmishangae ndugu yetu Matmebo akilalamikia kukosekana kwa samaki anaowapenda.
Ndiyo Nyasa yetu, raha na changamoto.
Kwa sasa ununuzi wa Kambale unaweza kuuziwa kipande badala ya kambale mzima. Hapo ni kipande cha Kambale akiwa tayari kwa kuuzwa. KARIBUNI NYASA


December 17, 2013

JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YAANZISHA BARAZA LA AMANI NA USALAMA


KAMPALA, Uganda
 
VIONGOZI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wametia saini kuanzishwa rasmi Baraza la Usalama la Jumuiya(East African Peace and Security Council) ambalo litashughulikia mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki. 

Viongozi hao kutoka Uganda, Tanzania, Kenya, Rwanda na Burundi wamefikia uamuzi huo juzi jumamosi wakati wa mkutano wao uliofanyika mjini hapa. Uamuzi wa kuanzisha Baraza la Usalama la Afrika Mashariki ni kutokana na kitisho cha kusambaa kwa ugaidi kama ambavyo yalivyotokea Dar es salaam(1998), Nairobi(1998 na 2013), na Kampala(2010).

Akizungumza mbele ya viongozi  waliohudhuria katika mkutano Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Richard Sezibera, alisema “Nathibitisha uamuzi uliofikiwa katika mkutano huu kuanzisha Baraza la amani na Usalama kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa na lengo la kuhakikisha ulinzi na usalama wa eneo hili dhidi ya tishio lolote litakalotokea,” 

Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakabiliwa na tishio la ugaidi unaofanywa na kundi la Al Shabab ambalo lina uhusiano na Al Qaeda. Kwenye mkutano huo, nchi wanachama wamekubaliana kukabiliana na tishio la ugaidi kwa pamoja ili kuepusha matukio kama yaliyokea mjini Nairobi katika maduka ya Westgate ambapo zaidi ya watu 60 wasio na hatia walifariki dunia na wengine 175 wakiwa majaerhu. 

Mwaka 2010 kundi la Al shabab lilidaiwa kufanya mashambulizi katika jiji la Kampala na kusababisha vifo vya watu 70 baada ya mabomu mawili ya kutegwa ardhi kulipuka.

January 24, 2013

JOHN STEVEN AKHWARI ANASTAHILI HESHIMA


Na Hance Forogo, Dar es salaam
Mzee wetu tunayempa Heshima leo alizaliwa mwaka 1938 katika wilaya ya Mbulu iliyoko mkoa wa Arusha....hapa namzungumzia mzee John Steven Akhwari!....akiwa kijana mdogo kabisa alianza kujiingiza katika mchezo wa riadha na haikumchukua muda mrefu kuwa mwanariadha wa mbio ndefu wa kutegemewa na Taifa la Tanzania akishiriki mashindano mengi ndani na nje ya Tanzania na amewahi kuwa bingwa wa mbio ndefu wa bara la Afrika,pia mwaka 1970 alimaliza mbio akiwa na 05 katika mashindano ya mbio ndefu kwa nchi za jumuia ya madola!....
Akitumia muda wa 2:15:05 wakati mshindi alitumia muda wa 2:09:28,inaaminika kuwa alikuwa ni mkimbiaji "World Class" mwenye hadhi ya dunia kati ya miaka ya 1960 na 1980!....
Katika tukio la kihistoria,mzee Akhwari katika mashindano ya Olimpiki mwaka 1938 nchini Mexico,katika mji wa Mexico akiwa wanafanya utani na wakimbiaji wa kuviziana na wakimbiaji wengine ili kupitana na kuwania ushindi alianguka ghafla akiwa amemaliza 19km kati ya 42km.
Baada ya kubanwa na misuli tatizo lililotokana na hali ya hewa kwani kabla hakuwa amefanya mazoezi katika mazingira yenye hali ya miinuko na hali ya nchi kama ya Mexico.
Kutokana na tukio hilo aliteguka goti na kupata jeraha kubwa pia alipata maumivu makali kwenye bega lake!.....hata hivyo aliendelea na mashindano na kumaliza wa mwisho akitumia muda wa 3:25:27 kati ya 57 waliomaliza mbio wakati wanariadha 18 hawakuweza kumaliza mbio huku mshindi Mamo Wolde toka Ethiopia akitumia muda wa 2:20:26!....baada ya muda mfupi kumaliza mbio zake,waandishi walimfuata na kumuuliza kwa nini aliendelea na mbio wakati alikuwa ameumia sana!?....
akajibu kuwa "Nchi yangu(Tanzania) haikunituma kushiriki maili 5000,imenituma nije kumaliza mbio za maili 5000" Jina lake linatumiwa na taasisi ya John Steven Akhwari Athletic Foundation ambayo inatumika kuandaa wanamichezo wanaojiandaa kwa mashindano ya Olimpiki,mwaka 2000 alialikwa kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Sydney nchini Australia na baada ya hapo alichaguliwa kuwa balozi wa heshima katika maandalizi ya mashindano ya Olimpiki jijini Beijing,China,pia 13/04/2008 alihusika na ubebaji wa Mwenge wa Olimpiki ulipokuja Tanzania katika maandalizi ya Olimpiki!....
Licha ya kwamba mwaka 1983 mzee wetu alitunukiwa medal ya heshima kama shujaa wa Taifa "National Hero Medal of Honor" hatuna budi nasi pande hizi KUMPA HESHIMA ZAKE kwa juhudi kubwa na uzalendo alioufanya kwa ajili ya nchi yake!....ameitangaza nchi kupitia mchezo wa riadha!.....
Huyo ndiye mzee John Steven Akhwari ambaye kwa sasa ni mkulima stadi,hakika anastahili HESHIMA!....Thanx!...

December 29, 2012

AZIMIO LA ZANZIBAR LILISAHAU B.E.E


Na Markus Mpangala 



Azimio la Zanzibar linafahamika kuwa nyenzo iliyotumika kuua lile la Arusha.
Ingawaje viongozi wetu hawasemi walichokubaliana kule Zanzibar, lakini hali haijifichi na inaonekana tunazidi kusonga mbele.
Kuna mtikisiko wa kijamii unaendelea kwa sasa, kutoka kwenye mitazamo na maisha ya ujamaa hadi kwenye kiwango cha chini cha ubepari. Bahati nzuri ni kwamba ujamaa upo mioyoni mwetu yaani ndio maisha ya watanzania.
Ni kwa sababu hii ndiyo maana Mwalimu Nyerere aliuita ujamaa wa kiafrika. Sasa basi, katika azimio la Zanzibar viongozi wetu bila shaka walikusudia kufanya mabadiliko katika uchumi. Bahati mbaya mabadiliko hayo yalikuwa yanafanyika kwa kudanganywa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Dunia.
Walichodanganywa viongozi wetu ni sera za asasi hizo kuwa mwongozo wa uchumi wetu. Halafu hali ikiwa mbaya wanachofanya ni kulaumu kuwa nchi imeshindwa. Sera za IMF na WB hazijali mazingira ya mwanadamu wa kitanzania.
Maeneo mengi imetokea hali hiyo na hivyo kuongeza kiwango cha ufukara kwa wananchi katika nchi husika. Ufukara huo unachochewa zaidi na jinsi sera inavyopuuza hali halisi ya mazingira ya nchi na utamaduni wa watu.
Sera za IMF na WB zinatokana na uzoefu wa nchi za Ulaya na Amerika. Kule wataimba nyimbo kuwa ruzuku ni muhimu kwa mkulima na wanakwenda nchi zetu za Afrika na kusema kama, ‘utampatia ruzuku mkulima basi unampunguzia uwezo wa kuwa mbunifu.’
Lakini hatujiulizi kwanini wakulima wa Ulaya wanapewa ruzuku na kadhalika. Sera za IMF na WB ndizo zilisababisha azimio la Zanzibar kuonekana kituko mbele wa wajuzi wa mambo.
Azimio hilo lililo katika kibarua cha Azimio la Arusha halikuja na mbinu mbadala ya kuweka msingi wa kukuza uchumi. Badala yake likaja na mageuzi ya uchumi katika mkondo wa sera za IMF na WB.
Kimsingi hilo lilikuwa kosa na dosari kiuchumi. Serikali yetu haikumwandaa au haikuhodhi moja kwa moja uchumi. Bali ikadanganywa na IMF na WB kuwa jambo muhimu ni kufungua milango ya mageuzi ya uchumi.
Milango iliyofunguliwa sio ile ambayo ilifunguliwa na chama cha siasa cha ANC cha Afrika Kusini. Chama cha ANC kilifungua milango ya mageuzi ya uchumi kwa sera yake, misingi yake na baadaye kikawa kinapokea ushauri tu.
Sera kubwa ambayo iliing’arisha ANC ni B.E.E. ( Balack Economic Empowerment). ANC ilikuwa wazi kabisa, hata kama sera hiyo iliwalenga watu weusi wa Afrika Kusini, na kuwatenga wazungu ambao ni raia halali wa nchi hiyo, lakini kilichofanyika ni kuziba pamba masikioni.
ANC ikasema inatambua kuwa B.E.E inaonekana kama inabagua lakini ni wajibu wao kutimiza uwezeshaji wa watu weusi katika mitaji ya kiuchumi. Mazao ya ANC ndio Tokyo Saxwalle, au familia ya kina Khoza.
Mfanyabiashara Tokyo Saxwalle anafahamika kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa na wawekezaji wa kiwango cha juu kutoka jamii za waafrika. Ni kutokana na sera hiyo iliwezesha kuibua wafanyabishara, wawekezaji na wajasiriamali wengine ambao walifanya kila jitihada kwa kutumia sera ya B.E.E kufanikiwa.
ANC ikasema lazima watu weusi wawezeshwe. Tafsiri sahihi hapa ni kuwawezesha wazawa. Hali hiyo ilitokana na miaka mingi ya utawala wa kaburu kuwanyonya na kuwakandamiza watu weusi. ANC ilipania, ikathubutu, ikatimiza dhamira yake.
Ni sababu hiyo tunaona baadhi  wawekezaji wakubwa waafrika kutoka Afrika Kusini, vinginevyo ubaguzi ulioanzishwa na makaburu ungeendelea kuwafanya waafrika wabaki hohehahe.
Mfano wa pili ni Chujusong, Korea Kaskazini. Tangu mwaka 1925 Korea Kaskazini chini ya chama cha kikomunisti ilifanya jitihada kubwa ya kujenga uchumi huku ikitanganza kuwa ni Jamhuri ya Kisoshalisti.
Chujusong ni mpango wa kujitegemea kiuchumi. Msingi mkuu ulikuwa kuhakikisha mitaji ya kiuchumi inakuwa huru ili kuondokana na utegemezi kutoka nje. Sera hiyo ilichukua ngumu na kuhodhi mwenendo wa nchi hiyo kujenga uchumi wake.
Polepole mabadiliko makubwa yakajitokeza hadi Korea Kaskazini tunayoiona leo. Hapa kwetu sera ya wazawa tu ilitushinda, na kwakuwa tulikuwa tumekosa uelewa wa kutosha tukadhani sera hiyo inabagua.
Laiti tungelikuwa na msimamo na uelewa wa kutosha kuwa huo siyo ubaguzi sababu hata wageni walioingia nchini mwetu waliwabagua wenyeji. Kwahiyo ili kukabaliana na pengo lililokuwepo zama za ukoloni, ilipaswa serikali ya awamu ya pili ilipofungua milango kuruhusu mageuzi ya kichumi, itunge sera za B.E.E.
Mpango wa kuwawezesha waafrika sio dhambi. Mpango wa kuwawezesha wazawa sio dhambi. Wazawa hao maana yake tuwe na wawekezaji sampuli ya Reginald Mengi.
Watu wa aina yake tuwe nao wengi ili kuimarisha mitaji ya serikali na uchumi wetu. Tusipokuwa na misingi inayoakisi ustawi wa taifa kiuchumi, itawezesha fedha nyingi za Tanzania kuishia mikononi mwa wadokozi. 
Na wadokozi wengine tulipowajua wakati wa miaka ya 1990 ntumejikuta sasa nchi inabomolewa benki yake. Sasa baada ya kuipoteza misingi hii tumejikuta tunahamasisha ujasiriamali.
Tunahangaika na ujasiriamali sababu wakati wa kufungua milango ya mageuzi ya uchumi hatukujua mageuzi hayo yanafanyikaje na uchumi utakuwaje.
Milango iliyofunguliwa ikawa ni kuruhusu wachuuzi ambao walidhaniwa wawekezaji, wakawa wanachuma mali za watanzania. Sasa, akili inapoibuka kipindi hiki tunajikuta kumbe wakati tunazika azimio la Arusha tulipaswa kutamka kwakuwa lazima tuwezeshe wazawa. Lazima watu weusi wawezeshwe kwenye mitaji. Na iwe sera sio huruma. Kwa sasa tumejikuta tunao wawekezaji wengi kutoka nje, halafu wawekezaji wa ndani bado uwezo wao  sio mkubwa sababu hawakuwa sehemu ya mageuzi ya uchumi yaliyofunguliwa wakati ule.
 Nionavyo, tunatakiwa kuwa na sera za kuondokana na uchuuzi wa kijasiriamali. Lazima tujenge uwezo kwa wazawa. Lazima tuwaige ANC kwa sera ya Black Economic Empowerment. Tujiulize, hivi kuna ofisi ngapi za Benki ya Dunia na IMF katika nchi za Kiarabu? Jibu hakuna ofisi hizo kwakuwa hazihitajiki. Tafakari. Nahitaji changamoto. 

December 04, 2012

KUITWA KWENYE USAILI DESEMBA 6&7

WALIOOMBA KAZI KATIKA SEKRETAIETI YA AJIRA NCHINI.

SOMA HAPA ....

November 20, 2012

KARIBUNI SANA NYASA, MLO WENYE VIRUTUBISHO VYA ASILI

                                                            KARIBUNI NYASA
Hilo tunaloweza kusema kuhusu wilaya ya Nyasa. Ni wakati wa kuburudika zaidi na kupata vyakula vyenye virubisho vya asili kama vinavyoonekana pichani.


November 14, 2012

SHULE ZA AWALI NYASA ZINAKABILIWA NA CHANGAMOTO LUKUKI


Na Albano Midelo, Nyasa
SERIKALI kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi iliamua kuanzisha mfumo wa elimu ya awali katika shule za msingi kwa lengo la kuwaandaa watoto wenye umri kuanzia miaka mitano.
Wizara ya elimu imedhamiria kuhakikisha kuwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi sita wanasoma darasa la awali kabla ya kuanza kuingia shule ya msingi wanapokuwa na umri wa miaka saba.
Uchunguzi uliofanywa katika kata za Kihagara na Liuli umebaini kuwa madarasa ya awali katika shule hizo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali hali ambayo inaathiri utoaji wa elimu hiyo muhimu kabla ya kuanzia shule za msingi.

Wanafunzi wa Darasa la Awali wapatao 90 katika Shule ya Msingi PUULU, Kata ya LIULI, wilayani Nyasa wakiwa katika darasa ambalo halina dawati hata moja.

Mwalimu wa taaluma katika shule ya msingi Ndonga kata ya Kihagara Amos Kilongo anasema shule hiyo ina darasa la awali lenye wanafunzi 37 ambao wanasomea kwenye mti kutokana na kukosekana kwa chumba cha darasa na kwamba mwalimu anayefundisha katika darasa hilo ni aliyemaliza kidato cha nne.
“Wanafunzi wa darasa la awali hawana darasa wanasomea chini ya mti,pia darasa halina madawati wa awali wanakaa  wakati wa mvua wanafunzi hao wanasome katika kanisa katoliki ambalo tumewaomba wamiliki wa kanisa hilo wamekubali kutusaidia’’,alisisitiza.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kihagara Anet Ngindo anasema shule hiyo ina darasa la awali lenye wanafunzi 52 ambao wanasomea chumba cha shule ya msingi wakifundishwa na mwalimu ambaye hajapata mafunzo ya ualimu na sio mwajiriwa analipwa posho kupitia michango inayochangwa na wazazi.
Mwalimu mkuu katika shule ya msingi Tumbi  Evaristo Ndiwu anasema katika shule yake kuna darasa la awali lenye watoto 45 ambalo halina chumba cha kusomea ambapo mwalimu wake hana taaluma ya ualimu ni mhitimu wa kidato cha nne analipwa posho kutokana na michango ya wazazi na walezi.
Katika shule ya msingi Mango,mkuu wa shule hiyo anasema katika shule yake kuna darasa ka awali lenye wanafunzi 60 ambao hawana chumba cha kusomea na  wanafundishwa na mwalimu ambaye hajapata mafunzo ya ualimu sio mwajiriwa badala yake analipwa posho na wazazi kati ya shilingi 30,000 hadi 50,000 kwa mwezi.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ngehe Silivanus Mbeya anasema katika shule yake kuna darasa la awali lenye watoto 36 ambalo halina chumba cha kusomea na linafundishwa na mwalimu ambaye amehitimu kidato cha nne hana mafunzo ya ualimu analipwa posho na wazazi ambayo haikidhi mahitaji ya mwalimu huyo.

Uvuvi ni shughuli inayoongeza kipato na ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa wilaya ya nyasa. hapa wavuvi wakiwa kazini.

Katika shule ya msingi Puulu  mwalimu mkuu wa shule hiyo Cathibert Maluka anasema katika shule yake kuna darasa la awali lenye wanafunzi 90 na kwamba wanafunzi hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo na ukosefu wa madawati ambapo wanafunzi wote wanasoma kwa kukaa chini.
“Darasa la awali katika shule yetu limebahatika kuwa na walimu wawili ambao wamepata mafunzo rasmi ya kufundisha wanafunzi wa darasa la awali hali ambayo inawawezesha kutoa elimu ya awali kulingana na malengo ya wizara ya elimu licha ya wanafunzi kusomea chini’’,alisema .
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nkali Erasmus Haule  anasema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 210 ina darasa la awali lenye wanafunzi 45 ambao hawana darasa badala yake wanasomea kwenye banda ambalo jioni linatumika kama klabu cha pombe na kwamba mwalimu anayefundisha hajasomea.
Katika shule ya msingi Hongi  kwa mujibu wa mwalimu mkuu Simon Ndunguru shule hiyo ina darasa la awali lenye wanafunzi 52 changamoto kubwa hakuna chumba maalum cha kusomea na kwamba mwalimu anayefundisha sio mwajiriwa na wala hajasomea kufundisha darasa la awali.
Katika shule ya msingi Mwongozo yenye wanafunzi 654 inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa darasa la awali lenye watoto 81 halina sakafu lina mwalimu mmoja ambaye hana mafunzo ya ualimu ,hajaajiriwa analipwa posho na wazazi wenye watoto hao
Baadhi ya wadau wa elimu katika kata za Kihagara na Liuli ambao ni Neema Msumba,John Ndunguru,Joel Makelele,Melikion Mapunda na Victor Komba wametoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa kila shule ya msingi inajenga darasa rasmi kwa ajili ya elimu ya awali badala ya shule nyingi kutumia vyumba vya shule ya msingi.
Wameitaka wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kuhakikisha kuwa kila darasa la awali inapeleka walimu waliopata mafunzo rasmi ya namna ya kufundisha watoto wa awali badala ya tabia ambayo inafanywa na shule nyingi kuwatumia vijana ambao wamehitimu kidato cha nne huku wakiwa hawajapata elimu ya ualimu.
Mratibu elimu kata ya Liuli Abrahamu Challe amesema kata yake imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto zote zinazoikabili elimu ya awali katika kata yake yenye shule saba zinatafutiwa ufumbuzi haraka ikiwemo kuwa na chumba rasmi kwa ajili ya awali,walimu na madawati.
Challe ametoa wito kwa serikali kutumia mfumo wa uboreshaji wa elimu ya awali kama ilivyokuwa kwa uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari kwa kujenga  vyumba viwili vya madarasa kwa kila shule na kusisitiza kuwa vifaa vyote vya ujenzi vitolewe na serikali na wananchi waachie ujenzi.
Afisa elimu msingi katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali ambaye anahusika na wilaya ya Nyasa anasema elimu ya awali ni sera ya wizara ya elimu kuhakikisha kila shule ya msingi inakuwa na darasa la awali kwa lengo la kuinua elimu hapa nchini.
Ameahidi kushirikiana na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani,watendaji wa vitongoji,vijiji,kata,tarafa pamoja na wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wanahamasisha wananchi katika maeneo yao kusimamia ujenzi wa madarasa ya awali na kutengeneza madawati ili watoto hao waweze kusoma katika mazingira bora.
“Ni ukweli madarasa ya awali yaliyo mengi yanafundishwa na walimu wasiopata elimu ni kutokana na uhaba mkubwa wa walimu uliopo katika shule nyingi nchini,lengo ni kuhakikisha tunapata walimu wa kutosha ikibidi hata kuwatumia walimu wanaostaafu kufundisha katika madarasa ya awali’’.alisisitiza.

Unaweza kuwasiliana na mwnadishi kwa anuani ifuatayo: albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129