Showing posts with label lundu. Show all posts
Showing posts with label lundu. Show all posts

March 26, 2018

AFISA MTENDAJI MPYA WA KIJIJI CHA LUNDU

Mara baada ya kustaafu kazi ya utendaji wa kijiji, bwana Remigius Nyenyembe maarufu kama Remmy au Fish, Kijiji chetu cha Lundu hakikupata mtendaji kwa muda mrefu ikasababisha Afisa Maendeleo wa Kata kukaimu nafasi hiyo.
 
Sasa kijiji chetu cha Lundu kimepata Afisa Mtendaji ambaye amewasili kijijini kwetu hapa tayari kuanza kazi. Ni mwenyeji wa Arusha, kwa jinsia ni mwanamke. Tunawaomba wanakijiji wenzetu wa Lundu wampokee na kumkaribisha ajione kama yuko Njiro,Philips,Ngarenaro,Ngaramtoni,Usa river, Sinoni daraja mbili yaani namaanisha Arusha.
KIJIJI CHA LUNDU
Kwa wakazi wa kijiji chetu kama watamtumia vizuri basi atasaidia kuleta maendeleo kwenye kijiji chetu kwasababu hawa wataalamu siku hizi wana viwango vizuri vya elimu na wamesomea masuala ya Maendeleo ya Jamii katika vyuo vinavyotambuliwa na serikali kama vile Homboro na vyuo vikuu vingine.

Tumtumie vyema mtendaji wetu kwa manufaa ya kijiji chetu cha Lundu kupata maendeleo. Itapendeza sana kama suala la kulewa asubuhi litapatiwa ufumbuzi maana wanywaji wamezidi.

©Honorius Mpangala

March 22, 2018

WODI ZA KULALA WAGONJWA ZA ZAHANATI YA MTAKATIFU RAPHAEL KIJIJI CHA LUNDU

 

February 23, 2018

MBOGA 7


Ukiwa mji kama wa Dar es salaam utasikia stori nyingi za Mboga 7. Au ukiwa maeneo ya mijini hii stori ya mboga 7 imezoeleka sana kusimuliwa. Lengo ni kuelezea familia yenye uwezo wa kuandaa mlo mmoja ukiwa umesheheni mboga za kila aina(nyingi). Lakini kwa wakazi wa Nyasa na Kijiji cha Lundu suala la Mboga 7 ni kawaida sana. Tofauti iliyopo ni kuelezea mazingira tu. Pengine watu wa mjini “Mnalamba lamba tu, hamshibi kisa hamna mboga”. Njoeni Lundu.

February 10, 2018

MIAKA 72 NA UBORA WA WAHANDISI WA KIJERUMANI PAMOJA NA WAASHI WA TANGANYIKA KIJIJINI LUNDU

NA KIZITO MPANGALA
MIAKA 72 tangu jengo hili la kiroho liliponengwa halijaleta usumbufu kiujenzi. Msingi wake ni imara. Ni mwaka 2005 pekee jengo hili liliathiriwa na kimbunga (chinangunga) ambapo ni paa pekee liliharibiwa na ni sehemu ndogo sana iliyoathiriwa. Ilikarabatiwa kwa muda mfupi na kukamilika. Boriti zake kwenye paa hata watu 10 boriti moja hawawezi kunyanyua. Huu ni uhandisi wa Wajerumani.

Tazama upande wa juu kuna msitari mweusi umenyooka ukutani hapo. Hii siyo rangi kusema kwamba imepakwa. Hayo ni matofali yaliyoiva na kuzidi viwango vya ubora, na ni ngumu kwa matofali haya kuvunjika kirahisi. Hivyo msitari huo hapo juu ni urembo tu kiujenzi.

Kuni ambazo ni bora sana kuchomea matofali ni Miyombo. Miti hii ipo katika vinasaba vilivyopo kwenye makundi mawili. Kuna Myombo ambao mara nyingi huzalisha aina fulani ya kamba (mighoyi) ambazo zina matumizi makubwa sana katika jamii ya watu wa Nyasa. Aina ya pili ni Myombo unaoitwa "Mpangala", mti huu pia ni dawa nzuri sana endapo utasumbuliwa na tumbo hasa kwa wanaoharisha. Mimi ninatumia sana dawa hii pamoja na Mwarobaini.

February 01, 2018

MANDHARI YA KUPENDEZA YA FORODHA YA LUNDU WILAYA YA NYASA

NGUVU YA MAWIMBI

UPANDE wa kushoto katika picha hii tazama jinsi mchanga ulivyojipanga. Haya ni matokeo ya vipindi mbalimbali katika Jiografia ya ziwa Nyasa. Kipo kipindi ambacho kikitokea mchanga huwa unasombwa na mawimbi na kupelekwa majini, hivyo unaweza kuingia majini na kutembea meta 50 na zaidi halafu kina si kirefu kwa sababu mchanga mwingi unakuwa umesambaa ndani ya maji. Kama unavyoona pichani, sehemu kubwa ya mchanga inemegwa. 

 Na kuna mchanga wenye rangi nyeusi inaying'ara nyakati za jua, pichani unaona sehemu fulani ya mchanga ni mweusi, ni mchanga unaovutia kwa macho.
Kipindi kingine ni kile kinachotokea halafu mchanga unarudishwa nchi kavu na kutengeneza kitu kama tuta fulani wakati huo ndani ya maji ukiingia unaweza kutembea meta 10 tu maji yakafikia shingoni, maana yake ni kwamba kina kinaongezeka kutokana na mchanga kurudi nchi kavu. 

January 26, 2018

NDOTO YA UPADRE ILIYOYEYUKA

Na. Honorius Mpangala
AKIWA amezaliwa katika kijiji cha Lundu wilaya ya Nyasa. Wazazi wake Daudi na Mama yake Neema wakambatiza jina la Markus ambalo lilitolewa na Padre Markus Komba alipohudumu parokia ya Lundu. Aliamini  labda siku za usoni angekuja kuwa kama yeye.
 
Alianza shule ya msingi Lundu na baadae kuhamia Kiwanjani iliyoko Mbinga Mjini akiwa darasa la sita. Maisha ya kijijini yalimfanya kujishughulisha na Masuala mbalimbali ya wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa hasa ikiwa uvuvi. Alikuwa akipenda kuroposha samaki siku za mapumziko ya wiki hasa kwa siku ya jumamosi tu maana jumapili ilikuwa lazima kwenda kanisani. 


Michezo pendwa wakati huo kwa vijana wengi ilikuwa kupigana kwa kutumia maembe mabichi wenyewe wakiita ' Ngondo ya mapula' yaani vita ya maembe mabichi ba chandimu. Alikuwa mtumiaji mzuri wa mikono yote yaani wa kuume na wa kushoto katika shughuli zake lakini mkwala wa baba yake juu ya matumizi ya mkono wa kushoto ukafanya aache kuutumia kwa hofu ya adhabu.

January 11, 2018

AFYA, IMANI NA HUDUMA LUNDU

Hapa ndipo tunapopata busara za kiroho tuwapo kijijini kwetu Lundu (Nyasa). Lilijengwa mwaka 1946. Awali wamisionari walifanya makao yao katika mlima Chipyaghela (haupo pichani).
Eneo walilofanya makao mlimani hapo lilikuwa linakumbwa na upepo mkali sana nyakati za kiangazi, ndipo mwaka 1929 wamisionari hao wakiongozwa na Padre Adrian (Mjerumani) waliiomba serikali ya kijiji cha Lundu kuwashawishi wazee Machwembele na Lipondelu ambao walikuwa ni wa ukoo wa akina Mpangala.
Ni ukoo ulioshika maeneo mengi yanayoizunguka misheni kijiji cha Lundu. Basi baada ya serikali kuwashawishi wazee Machwembele na Lipondelu, waliamua kuwapa wamisionari eneo la kujenga kanisa la kuanzia na nyumba ya kuishi mapadre.

December 30, 2017

PUGU HADI PERAMIHO; Kijiji cha Dar, Utemi wa Wangoni na kumbukizi maridhawa.

Katika kitabu cha "PUGU HADI PERAMIHO" kuna masimulizi ya kutoka mwaka 1888-1988 na ujio wa Wamisionari wa kijerumani kupitia Shirika lao la Benedictine Fathers lenye makao yale mjini Peramiho kwa sasa.  
Kitabu hiki ni mkusanyiko wa barua na kumbukizi binafsi (Diaries) zilizoandikwa na Mapadre, Mabruda, Masista wakielezea masuala ya ukoloni wa Kijerumani, Injili, Umisionari, Wapagazi, Wangoni na kupenda vita na starehe pamoja na mahusiano ya kibadamu kati ya wazungu na waafrika.

PADRE ANDREAS AMRHREIN
Kitabu hiki kinaanza kwa maandiko ya Abate Lambert Doerr, OSB. Kwanza "Abate" ni wadhifa waliopewa wakuu wa mashirika ya Benedictine Fathers. Lambert anafungua pazia la masimulizi ya Wamisionari Wabenediktine kusini mwa Tanzania. 

December 27, 2017

...KUMBUKIZI ZA MZEE MPANGALA NA WAMISIONARI WABENEDIKTINE LUNDU



Mwaka 1931 Wamisionari waliomba eneo la kujenga himaya yao ya kitawa kwa serikali ya kijiji cha Lundu. Baada ya pendekezo lao serikali iliwaomba wazee wawili kutoka Ukoo wa Mpangala ili kuwapa Wamisionari hao eneo la kujenga makazi ya Kitawa.
Alikuwa Mzee Machwembeli Mpangala (Baba yake Mzee Hansgary Mpangala au Waziri) na Lipondelu Mpangala (Babu yake Mzee Hubungu au Robert Mpangala).Mzee Machwembeli alikuwa anamiliki eneo la kuanzia kilipo kituo cha afya kuelekea kaskazini( Kwa wale wanao ifahamu Lundu) na Mzee Lipondelu alitoa kuanzia Hapo kituo cha afya kuelekea Kusini iliko nyumba ya mapadre.
1959 Walijenga machine ya kupump maji toka forodha ya Chivanga hadi eneo la misheni.Mzee alishiriki ujenzi Huo akiwa na Bruda Lambert. Ananiambia gari ya kwanza kufika kijijini kwetu ilikuwa ni 1954.
Asubuhi ya Leo alinipiga na salamu ya kijerumani nikabaki natoa macho tu.Uishi miaka mingi zaidi Mzee wangu.

Honorius Mpangala,
#Mtoto_Wa_Misheni

December 09, 2017

SALAMU KUTOKA LUNDU, ZIWA NYASA

Nipo kijijini kwetu Lundu kwa muda wa mwezi mmoja sasa. Naendelea kukusanya taarifa mbalimbali zinazofaa kuchapishwa hapa barazani “Karibuni Nyasa”.  Kama tunavyoona habari mbalimbali za utalii, basi ndivyo utakavyosikia habari usizowahi kuzijua kutoka mwambao wa Ziwa Nyasa. Mazingira yanayovutia mno, yenye kuhitaji kutembelewa.
 
Kuna picha mbili; ya kwanza nikiwa katika Mto Chipapa, uliopo mtaa wa Likwambe hapa hapa kijijini Lundu. Ni mto ambao miaka 1990 ulikuwa ukitiririsha maji yake mwaka mzima kwa ufasaha. Lakini sasa mambo yamebadiliika, hakuna uwezekano huo. Kwahiyo mto huo unangojea msimu wa masika kama hivi sasa uweze kuwa na maji ya kutiririsha hadi Ziwa Nyasa.

November 22, 2017

FUKWE ZA LUNDU, KARIBUNI ZIWA NYASA

 Hapa ni Forodha ya Lundu. Eneo hili lina fukwe mzuri sana kama huu. Picha ya Juu ni upande wa Kusini mwa forodha. Picha ya chini ni upande wa kaskazini magharibi mwa forodha hiyo. Ufukwe huu umepokea wageni kutoka Ujerumani, Italia, na wengineo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibuni sana Lundu. Karibuni Wilaya ya Nyasa.

November 15, 2017

TANZIA

Ilikuwa runununi, 
Saa kumi za jioni,
Ni jumatatu mwanzoni, 
Wiki ilipoanzia.

Kwa ujumbe wa majonzi, 
Denisi kashusha pumzi,
Kanijulisha mpenzi, 
Ndugu yetu katufia.
 
Mnenaji alinena, 
Si usiku ni mchana,
Tumepoteza kijana, 
Songea kaniambia.

November 10, 2017

KINANDA: MAJI YA ZIWA NYASA YANAPUNGUA?

NA MARKUS MPANGALA

JIWE hili ni maarufu sana katika kijiji cha Lundu. Linaitwa Kinanda au kwa wenyeji tunaliita kienyeji “Chinanda”. Lipo katika forodha ya Chivanga. Picha hii ilipigwa mapema Mwezi Februari mwaka huu. 
Honorius Mpangala akiwa katika Jiwe la Kinanda, Februari mwaka huu.
 
Lipo jambo moja la kusikitisha ni kwamba kiasi cha Maji katika Ziwa Nyasa si kama kile kilichokuwa zamani. Katika miaka ya 1980 hadi miaka 90 jiwe hilo lilizungukwa na Maji. Lakini miaka mwanzoni mwa 200o kumekuwa na mabadiliko mengi katikam ziwa.

November 04, 2017

UTALII: UFUKWE WA KIJIJI CHA LUNDU

Wilaya ya Nyasa imebarikiwa kuwa na fukwa zuri zinazotokana na ziwa Nyasa. Huu mojawapo ya ufukwe wenye historia kubwa sana, kupokea wageni kutoka Ujerumani, Uingereza, Italia na nchi mbalimbali ambao wengi wao walikuja kupitia Shirika la Benedictine Fathers la Peramiho na wengine kwa njia zao binafsi. Ni ufukwe wenye kumbukumbu nzuri sana kwa wakazi na wageni.
KARIBUNI NYASA.

October 27, 2017

KWANINI WILAYA YA NYASA IMESHIKA MKIA KATIKA MATOKEO YA DARASA LA SABA?



RAYMOND NDOMBA, SONGEA
WILAYA ya Nyasa iliyopo mkoa wa Ruvuma imekuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba mwaka huu 2017 kimkoa. Swali la kujiuliza ni kwanini hali hiyo imetokea. 


Mawazo yangu ni haya; Pamoja na sababu nyingi zilizosababisha matokeo hayo ya aibu kubwa. Wazazi wanapaswa kubeba lawama kubwa. Wengi wao hawafuatilii maendeleo ya watoto wao, pia makuzi na malezi mabaya.

Miaka ya hivi karibuni (kuanzia mwaka 2000), Wazazi wengi katika wilaya ya Nyasa hawajali elimu, hawajigusi katika ufuatiliaji wa watoto wao kielimu na hata kitabia (Angalia matokeo ya mitihani ya Taifa ya shule za msingi na sekondari kunzia miaka hiyo ya 2000 kwa shule kongwe ndani ya wilaya). 

October 17, 2017

TAKWIMU MUHIMU ZA WILAYA YA NYASA HADI OKTOBA 2017


1. Total Number of Hamlets in the District = 425

2. Total Number of Households for Nyasa dc = 31,146

3. Total Female Population for Nyasa dc = 74,768.


4.Total Male Population for Nyasa dc = 71,392.

5. Total Population for Nyasa dc = 146,160.

6. Total Number of Secondary school = 14

7. Total Number of Primary School = 106
Total Number of Villages = 84


8. Total Number of Ward = 20

9. Total Number of Division = 3

CHANZO: Nyasa dc statistics

October 12, 2014

UCHIMBAJI WA MAKAA YA MAWE KIJIJI CHA NDUMBI NA UTATA WAKE

 


Tanzania shamba la bibi haya makaa ya mawe yanasubiri kusafirishwa kwenda kusikojulikana via bandari ya Ndumbi wilayani nyasa.

Picha kwa hisani ya Hoops Kamanga.