Showing posts with label Usalama. Show all posts
Showing posts with label Usalama. Show all posts

February 14, 2018

UTEUZI WA MNADHIMU MKUU JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA

January 19, 2018

MTO MAKATA WASABABISHA USUMBUFU KWA VYOMBO VYA USAFIRI MBAMBA BAY

Tukiwa tunasubiri Ujenzi wa Barabara ya Mbinga-Mbambabay mwezi February 2018, hali ya barabara MTO Makata mjini Mbambabay leo si nzuri kwani imesababisha masuala ya usafiri kusimama kwa muda. 
Basi la Abiria likiwa limeshindwa kuendelea na safari kutokana na eneo la mto Makata kuwa bovu.
Picha kwa Hisani ya Egbert Jemeny(pichani).

January 12, 2018

JIMBO LA NYASA: KWANINI WANANCHI WA TARAFA YA RUHUHU WAMEACHWA UKIWA?

NA MARKUS MPANGALA
Ubovu wa Barabara katika kijiji cha Ndumbi.
RUHUHU ni miongoni mwa Tarafa zinazounda Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa. Wilaya hii ni miongoni mwa zingine kama Songea Vijijini, Songea Mjini, Mbinga, Namtumbo, Tunduru zilizopo mkoani Ruvuma. Wilaya ya Nyasa ilianzishwa rasmi mnamo Machi 2012 baada ya kugawanywa wilaya ya Mbinga. Eneo la wilaya ya Nyasa liko kando la Ziwa Nyasa.
Tarafa ya Ruhuhu ipo kwenye mwambao huo, ikiwa ni miongoni mwa maeneo yaliyoachwa nyuma kimaendeleo na kiuchumi. Tarafa hiyo inazo Kata za; Mbaha, Lituhi, Ngumbo na Liwundi. 
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka wa 2012, Kata ya Mbaha ilikuwa na wakazi wapatao 6,972. Ni Kata ambayo ndiyo mwenyeji wa Shule ya Sekondari ya Monica Mbega iliyoanzishwa rasmi mwaka 2006. Jina la shule hiyo lilitokana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Monica Mbega kabla ya kuondoka.
Wananchi wa Tarafa hii wanakabiliwa na changamoto nyingi mno hali ambayo inadhoofisha ukuaji wa uchumi. Changamoto hizo zinatokea katika nyakati tofauti na kuziba mianya ya kujipatia pato kutokana na huduma kadhaa wa kadhaa kuwa dhaifu. 

October 16, 2017

“RAIS ANA MIAKA 31”


Sebastian Kurz
JUMAMOSI nilikuwa nasoma makala ya James Masters kwenye tovuti ya CNN. Sentesi yake ya kwanza ilinivutia sana, “Ulikuwa unafanya nini ulipokuwa na umri wa miaka 31? Ingawa aliendelea na mengine lakini staili pekee haikuwa kivutio bali mtu aliyekuwa akizungumzwa alivutia zaidi.
James Masters alikuwa anamzungumzia Sebastian Kurz ambaye amewahi kuwa waziri wa  Ushirikiano wa Kimataigfa tangu mwaka 2013 akiwa na miaka 27.  Sebastian  Kurz ambaye amekuwa Kansela wa Austria mwenye umri mdogo zaidi kwani sasa hivi ana miaka 31 tu. 

Ni mwenyekiti wa chama cha  OVP. Sebastian kuanzia jana jumapili aanaongoza serikali ya Austria ( kama vile Rais hapa kwetu) baada ya chama chake kushinda viti vingi vya bunge. 

September 27, 2017

ADHABU KWA MWENDESHA BAISKELI




Jana mchana mwendesha Baiskeli alipita kwa kasi katika makutano ya barabara ya Bibi Mohammed na Morogoro bila kuruhusiwa na taa za kuongoza magari. Wakati anapiga taa zilionyesha magari yapite, na yalikuwa yakipita kwa mwendo kasi mno, kiasi kwamba ingetokea gari linalopita basi angegongwa na kusababisha matatizo makubwa.

December 17, 2013

JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YAANZISHA BARAZA LA AMANI NA USALAMA


KAMPALA, Uganda
 
VIONGOZI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wametia saini kuanzishwa rasmi Baraza la Usalama la Jumuiya(East African Peace and Security Council) ambalo litashughulikia mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki. 

Viongozi hao kutoka Uganda, Tanzania, Kenya, Rwanda na Burundi wamefikia uamuzi huo juzi jumamosi wakati wa mkutano wao uliofanyika mjini hapa. Uamuzi wa kuanzisha Baraza la Usalama la Afrika Mashariki ni kutokana na kitisho cha kusambaa kwa ugaidi kama ambavyo yalivyotokea Dar es salaam(1998), Nairobi(1998 na 2013), na Kampala(2010).

Akizungumza mbele ya viongozi  waliohudhuria katika mkutano Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Richard Sezibera, alisema “Nathibitisha uamuzi uliofikiwa katika mkutano huu kuanzisha Baraza la amani na Usalama kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa na lengo la kuhakikisha ulinzi na usalama wa eneo hili dhidi ya tishio lolote litakalotokea,” 

Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakabiliwa na tishio la ugaidi unaofanywa na kundi la Al Shabab ambalo lina uhusiano na Al Qaeda. Kwenye mkutano huo, nchi wanachama wamekubaliana kukabiliana na tishio la ugaidi kwa pamoja ili kuepusha matukio kama yaliyokea mjini Nairobi katika maduka ya Westgate ambapo zaidi ya watu 60 wasio na hatia walifariki dunia na wengine 175 wakiwa majaerhu. 

Mwaka 2010 kundi la Al shabab lilidaiwa kufanya mashambulizi katika jiji la Kampala na kusababisha vifo vya watu 70 baada ya mabomu mawili ya kutegwa ardhi kulipuka.

August 15, 2013

JESHI LA POLISI LAANZA OPERESHENI MAALUMU


Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
Jeshi la Polisi nchini limewaomba wananchi kuimarisha na kulinda amani na usalama kwa kuwafichua wahalifu wa aina yeyote wakiwemo wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakilisumbua jeshi hilo. 

Kwa mujibu wa Msemaji wa jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema kuwa uamuzi wa Jeshi la Polisi kuwaomba wananchi washiriki katika zoezi hilo ni kutimiza amri ya Rais Kikwete ambaye alitoa siku 14 kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinawakamata wahalifu na wahamiaji haramu pamoja na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria hususani maeneo ya mipakani. 

“Jeshi la Polisi linasisitiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama nchini wawe tayari kuwafichua wahalifu wa aina yeyote ile wakiwemo wahamiaji haramu kwa vyombo vya dola au mamlaka yoyote ya serikali, wananchi wasikubali kuwahifadhi wahamiaji haramu na  watoe taarifa wawaonapo wakiingia kwenye maficho maarufu kama njia za panya,” alisema Senso.
Aidha, msemaji huyo aliongeza kuwa ni lazima jamii ihamasike kulinda amani na usalama, pia Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola limepanga kuendesha operesheni maalumu ya kuwabaini na kuwamata watu wote wanaokiuka sheria au kuhatarisha ulinzi na usalama hapa nchini

“Tunawaomba wananchi washirikiane na vyombo vya dola, hii itsaidia  nchi yetu kuendelea kuwa salama, hususani wananchi waishio mipakani. Baada ya siku kumi na nne alizotoa Mhe. Rais kumalizika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitaendesha operesheni kali ya kuwabaini ikiwemo wanaomiliki silaha kinyume  cha sheria,”

June 13, 2013

ULINZI NA USALAMA WETU:


Na Edgar Mwandemani

Leo naomba nijitumbukize katika mjadala mgumu kidogo. Ni hili suala la ulinzi na usalama wa watanzania na mali zao. Natambua kuwa hapa nchini tunavyo vyombo vilivyokasimiwa majukumu ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao upo, unadumishwa na kuondoa aina yoyote ya tishio dhidi ya raia.

Tunalo Jeshi la Polisi, JWTZ, JKT, Magereza, Uhamiaji, Usalama wa Taifa kwa kutaja vichache. Vyombo hivi pamoja na mambo mengine vinahudumiwa na kodi za raia ili vitulinde lakini vyote pia vinaundwa na raia wa nchi hii. Kwahiyo, usalama wa raia ndio usalama wa vyombo hivi.

Nijielekeze kwenye lile nililotaka tujihoji. Siku za hivi karibuni kumeibuka mlolongo wa matukio ambayo yanatuingiza shakani kama nchi, japo inaonekana ni matukio yanayolenga kundi fulani tusipongalia yatasambaa na kumhusu kila raia.

Ukiondoa matukio ya vifo na majeraha yanayotokana na vurugu za raia, mapigano baina ya makundi kama wakulima na wafugaji, vifo vilivyotokana maandamano na migomo. Ni dhahiri kwamba katika maeneo fulani majeraha na vifo ni matokeo ya mikakati madhubuti inayopangwa ama na watu binafsi, vikundi au taasisi zetu rasmi ambazo kwa upande mwingine zilipaswa kuhakisha hayo hayatokei.

Matukio ya kuumizwa na kuuwawa kwa raia wasio na hatia wakiwa katika himaya za vyombo vyetu vya ulinzi na usalama yameongezeka nitakumbusha machache tu. Wale wafanyabiashara wa vito "kesi ya Zombe", yuko dereva teksi pale Kimara, kijana mwingine aliwawa kule Chunya akiwa kituo cha polisi. 

Unyama dhidi ya waandishi Saed Kubenea na Ndimara Tigambwage, Dr. Stephen Ulimboka, Daudi Mwangosi kule Iringa, na hivi karibuni mwandishi Absolom Kibanda. Huyu wa mwisho ameweza kutoka hadhani na kutuambia "haya yote ni matukio ya kupanga kutokana na namna yanavyojitokeza" na akahoji kuwa pamoja na ahadi nyingi kwamba "tutahakikisha wahusika wanakamatwa mara moja na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria" hakuna lililokwisha kufanyika akichukulia mfano wa tukio lililomkumba yeye binafsi.

Inawezekana tukaona matukio haya yote hayatuhusu, lakini nina hakika kuwa iko siku sisi sote tutahusika kwa sababu tumekubali utaratibu huu ndio uongoze maisha yetu. Hatuwezi kudumu katika vurugu hizi harafu siku moja zisiiangamize jamii nzima!

Kwanini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kushindwa kushughulikia wahalifu hawa wanaoumiza, kutesa na kuua wasio na hatia. Je, vinataka tuamini kuwa navyo vinahusika na uchafu huu unaondoa hali ya amani na utulivu. Hali inayokaribisha ile dhana ya "survival for the fittest". Tujiulize itakuwaje pindi kila raia atakapochukua jukumu la kujilinda mwenyewe?

Mbaya ya jambo hili ni kuwa hivi sasa limefanywa ni silaha ya kisiasa. Hivi sasa pande zinazohusika katika siasa za nchi hii zimekuwa haziishi kutuhumiana kwa mauaji na utesaji. Kila upande umekuwa ukieleza kuwa una ushahidi na unawajua watekelezaji wa unyama huu. Na wengine wamekuwa wakiwatumia wahanga wa matukio haya ili kuendeleza agenda za kisiasa ikiwemo kuonyesha ubaya wa upande wa pili.

Muda wote huo sisi kama raia tumekuwa tukichekelea na wengine kushabikia upuuzi huu, huku upande wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ukiwa hauonekani kushtushwa na hali ya mambo. Ni kutokana na hali hii wahanga wa matukio haya wameanza kujilinda kwa makundi yao: waandishi wanalia kivyao, viongozi wa dini nao wanabaki kulalama; raia kule mtaani nao hivi sasa wameanza hata kuvamia na kuchoma vituo vyetu vya polisi kwa hisia kwamba vimepoteza maana. Wakati wa matukio ya kule Mtwara inaelezwa kuwa gari la Afisa usalama lilitekezwa kwa moto.

Naomba tushirikiane katika tafakuri hii juu ya hali ya ulinzi na usalama wetu, huku tukiendelea kudadisi yaliyomo katika rasimu ya Katiba iliyotoka hivi karibuni

March 11, 2013

KUFUKUZA MAKURUTA 95 WA JESHI LA POLISI HAITOSHI


Markus Mpangala

Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
Tukio la waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi kuwafukuza Makuruta 95 wa Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi kwa kile alichooita kugundulika kutumia rushwa kujipatia ajira, bado linaelea katika vichwa vya watu juu ya msingi wa maadili yetu.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Renatus Chalamila amehusishwa na rushwa katika kuajiri. Waziri Nchimbi amechukua hatua zaidi baada ya kumsimamisha kazi Kamishna huyo. Alisema pia taarifa za uchunguzi za Kamishna huyo, ambaye anashughulikia masuala ya ajira zimewasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete ambaye ana mamlaka ya kumfukuza kazi au uamuzi mwingine wowote.

Japokuwa waziri Nchimbi ametaja pia maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi ambao wamehusishwa na makosa mbalimbali lakini binafsi nimeguswa na huku chini kabisa (Makuruta). Kwa maana nyingine harakati za vijana 95 ambao wamefukuzwa na waziri Nchimbi waliokuwa wakitarajiwa kuingia kwenye ajira ya ndani ya Jeshi la Polisi, linatuletea swali la msingi juu ya maadili na namna tunavyojenga usalama wetu nchini. Hii ina maana katika Makuruta hao 95 tulikuwa na watu wenye tabia tofauti, lakini baya zaidi wamekutana katika msingi wa kutoa rushwa ili wapate ajira.

Namna nyingine tunajiuliza mfumo wetu wa jira katika sekta za ulinzi na usalama ukoje na nani anawajibika kuutengeneza pale unapokwenda kombo. Makuruta 95 ni wengi au hata wangelikuwa watano tu, lakini ukweli tunabakia katika mwenendo mbovu wa jamii iliyochoka kufuata kanuni hivyo kila kitu kinatakiwa kwenda ‘fasta fasta’. Ni tabia hii ya ‘fast tracking’ inatufikisha mahali pabaya kabisa na kushuhudia vijana wadogo wakijihusisha na rushwa.

Naam kufukuzwa kwao ni ushahidi wa wazi kabisa jamii yetu imeoza na hata wale viongozi kule juu akiwemo Kamishna Renatus Chalamila, ni taswira iliyoko huku kondeni. Kama CCP leo hii imegubigwa na vikwazo vya ajira mpaka vijana wetu watoe rushwa ina maana mfumo wetu wa kutumia rasilimali watu umegubikwa na maadili duni. Wengi wanatoa ajira kwa misingi ya jinsia, wajihi, rushwa, na kadhalika.

Kwa namna nyingine sio sifa nzuri kwa Jeshi letu adhimu la Polisi. Mwanazuoni wa masuala ya kijeshi Sun Tzu kwenye kitabu chake cha ‘The Art of War” anasema kama jeshi likiingia vitani kisha likapoteza mwelekeo basi wakulaumiwa ni Jenerali wa jeshi husikal Sun Tzu anasema iwapo jeshi likiwa kwenye gwaride linatii maagizo yote; kushoto geuka, kulia geuka, au mbelee tembeaaaa!

Waziri Nchimbi
Iweje jeshi hilo likapoteza umahiri huo ndani ya uwanja wa vita. Bahati mbaya Sun Tzu alisahau kuwa katika uwanja wa vita kuna matukio ambayo yanaweza kubadilisha mwelekeo au tabia za jeshi. Kama mwanajeshi hakuwa thabiti licha ya mafunzo yake, basi haitashangaza kuona siku moja akishindwa kuingia uwanja vita sababu tu ya kukosa misingi binafsi ya kulitumikia jeshi.

KWANINI JESHI LA POLISI LIWE NYENZO?
Moja makosa makubwa yanayofanyika katika jamii yetu ni kushindwa kuelewa watoto wetu wanatakiwa kufanya kazi gani katika maisha yao. Wapo wazazi ambao hawajui na watoto nao hawajui wafanye kazi gani hata wanapofika kidato cha nne. Wengi wao wakishapata matokeo ya mitihani yao ndipo huanza kujiuliza wafanye kazi gani.

Kwa Makuruta 95 waliokubali kutoa rushwa ina maana kuwa walikuwa wanataka kulitumia Jeshi la Polisi kama nyenzo ya kufanya kazi nyingine hapo baadaye. Mtu makini akichambua hili na kuangalia mwenendo wetu kwa Jeshi la Polisi, wapo wanaojiunga sio sababu ya mapenzi yao bali kwakuwa wanataka ‘kutoka’ kimaisha hivyo mwelekeo uliopo ni CCP Moshi. Sina shaka kabisa, Jeshi la Polisi linaweza kufanya uchunguzi wa mambo mbalimbali ikiwemo hili. Ni rahisi kukukotoa idadi ya wahitimu wa Jeshi la Polisi kila mwaka na wanakopelekwa na muda wao kazini.

Kisha Jeshi la Polisi linaweza kuanza kufuatilia wahitimu hao kama wameendelea na kazi ya Upolisi kwa muda gani na wanafanya nini baada ya kujiondoa katika jeshi la Polisi. Ninasema hivi kwakuwa katika nyakazi zetu Jeshi la Polisi kwa baadhi ya watu wanatafsiri kama sehemu ambayo wanakwenda vijana walioshindwa maisha hivyo kwa muda fulani wanajua wataweza kupata nyenzo ya kufanya kazi nyingine.

Ni wazi wengi waliowahi kujiunga Jeshi la Polisi kwa uadilifu wamedumu na wanaendelea kuheshimu taalumu yao. Lakini wapo wengine wanalitumia Jeshi la Polisi kama nyenzo ya kufanikisha mipango ya maisha. Ni kweli wana haki, lakini hawa vijana wetu baadhi yao wanaweza kabisa kuwa ndani ya jeshi la Polisi kisha baadaye wakipata njia za kufanya shughuli nyingine (baada ya kuelimishwa na au kulifanya jeshi kuwa mtaji).

Endapo Jeshi la Polisi limeweza kugundua Makuruta 95 wameingia kwa rushwa safari hii ni vema likafanya uchuguzi mwingine juu ya wahitimu wake na vituo vyao vya kazi. 

HASARA
Hakuna hasara kubwa kama watu kutumia idara za usalama kama nyenzo ya kufanikisha mipango yao. Tunahitaji askari waadilifu na wenye kuipenda kazi yao. Tunahitaji watu ambao sio tu watakuwa wakilalamikia mishahara midogo bali kutumia kidogo hicho kwa uadilifu na kulinda maslahi ya nchi yetu.

Lakini hakuna hasara kubwa inayotokea kama kitendo cha Makuruta 95 hao au wale waliowahi kupitia CCP Moshi na kadhalika wanaoingia maisha ya kawaida ya mtaani. Katika mazingira haya, “hisia” za ongezeko la Uhalifu haliwezi kukosekana kabisa. Na ili kukabiliana nalo ni vema kutafuta njia mwafaka za mkunusuru Jeshi letu la Polisi ili lisiwe na linakusanya tu kama kokoro na kujikuta limejaza askari wasiowaadilifu.

Ni mbaya, na hatutakuwa tumeokoa jamii inayoamua kufikiria RUSHWA kwanza ndipo ipate ajira. Ni vyema katika tukio la Makuruta waliofukuzwa wafuatiliwe na kuhojiwa zaidi, na iwapo wazazi wao walihusika kuchochea (kama) basi nao wanatakiwa kupitiwa na mkono wa sheria. Kuwafukuza Makuruta pekee hakutoshi mheshimiwa Waziri Nchimbi. Nimemaliza.