Showing posts with label ng'ombo. Show all posts
Showing posts with label ng'ombo. Show all posts

January 15, 2013

MRADI WA MAJI KIJIJI CHA NG'OMBO WAKAMILIKA

Na Mwandishi  wetu, Ng'ombo
Wakazi zaidi ya 2450 wa kijiji cha Ng’ombo katika Kata ya Chiwanda wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wameondokana na adha iliyokuwa ikiwakabili ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji kijijini hapo,

Akizungumza na Lundunyasa Network, Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo Amos Mtweve alisema mradi huo ambao umejengwa kwa ufadhili wa UNDP kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira umegharimu jumla ya shilingi 298,346,700 na kwamba kuna vituo 23 ambavyo wakazi wa kijiji hicho watakuwa wakivitumia kupata maji.
Mhandisi Mtweve alisema kuwa kabla ya kujengwa kwa mradi huo wananchi walikuwa wakilazimika kutumia maji ya ziwa Nyasa kwa ajili ya kunywa, kupikia, na kuoga hali ambayo ilikuwa ikihatarisha usalama wa afya zao.
Alisema pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza wakati wote wa ujenzi wa mradi huo ikiwemo baadhi ya wananchi kutojitokeza kuchangia nguvu zao kama uchimbaji wa mtaro kwa ajili ya kulaza mabomba lakini bado mradi umekamilika kwa kwango kilichotakiwa.
“kukamilika kwa mradi huu kimsingi ni sifa kubwa kwetu kwani itawapa matumaini wafadhili wetu kufadhili miradi mingine hasa ikizingatiwa kuwa UNDP wamefadhili miradi michache ya maji hapa nchini ikiwemo huu wa kwetu,” alisema Mhandisi Amos Mtweve.

November 01, 2012

JAMES ZOTTO ALIPOZUNGUMZIA MGOGORO WA ZIWA NYASA, KABLA YA KUWASILISHA UTAFITI WAKE KWENYE UMOJA WA AFRIKA NCHINI ETHIOPIA

Mgogoro wa mpaka Malawi na Tanzania: siasa na ukweli

Na James Zotto, University of Dar es Salaam
Ndugu zangu watanzania, naamini mnafuatilia vizuri tatizo la mpaka wetu wa ziwa Nyasa na Malawi! Na pia mmefanikiwa kusikia au kusoma hotuba ya Waziri wa Mambo ya nje, Benard Membe. Nilishtushwa kidogo na hotuba hiyo. Niharakishe kusema, mimi napenda utaifa wangu na uzalendo wangu. Lakini napenda sana kutetea mambo yangu kwa kukubali ukweli, kujua hali halisi, kukubali hata zile zinazonipinga, ili nami nijipange kujenga joja. Niongeze tu kuwa, eneo hili nafanyia study yangu ya PhD. Sidhani kama nipo sahihi zaidi na lengo langu si kusema nani anamiliki nini!  
James Zotto akiwa pembezoni mwa ziwa Nyasa.
Ukweli ninaofahamu, tatizo si kubwa sana kama tunavyolifikiri, na pengine tutachukua muda kupitia nyaraka zote muhimu. 
Kwanza, tunahitaji kwenda Idara ya Kumbukumbu ya Uingereza(Public Records Office). Pili tunapaswa kufuatilia Colonial Archives Potsdam, Ujerumani. 
Aidha, tufuatilie pia Malawi National Archives, Tanzania National Archives, Maktaba Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM) na Chancellor College Malawi. Ninaamini ubishi utaisha kwa kuwa nyaraka zote zipo.
Naomba nianze kujadili kwa kuweka angalizo katika suala hili ili ikilazimika, Malawi wasalimu amri kwa njia yoyote tutakayoamua, nitasema hapo baadaye. 
Angalizo lenyewe: ziwa Nyasa liligawanywa na mabeberu wa Kiingereza, Kijerumani na Kireno. mkataba wa mwaka 1890 uitwao Anglo-German Agreement, unasema mpaka wa uliokuwa miliki ya Ujerumani au kwa kiingereza German East Africa (Tanzania Bara ya leo) na Nyasaland (Malawi ya leo) unapita kando kando ya ziwa Nyasa kutoka mto Ruvuma(mkoani Ruvuma) mpaka mto Songwe(mkoani Mbeya).
Mkataba huo upo katika nyaraka nyingi sana. Mathalani katika Sheria za Kimataifa (International Law) wanafahamu jambo hilo na sina shaka ndugu zetu wanasheria wa kimataifa (International Lawyers) wanaelewa nini nazungumza! 
Sehemu nyingine ilikuwa ya mkataba ilikuwa mwaka 1891 kati ya Ujerumani na Ureno. Kulingana na mkataba huo, walikubaliana kuwa mipaka ilianzia mto Ruvuma kuelekea Portuguese East Africa (Msumbiji ya leo).
Mkataba mwingine ulikuwa ni kati ya Ureno ambayo ikawekeana mipaka na British Nyasaland (Malawi), kwahiyo, kipindi cha Ujerumani, mipaka inasomeka 'it passes along the shore of the lake (Nyasa).”
Hata hivyo kuliwahi kutokea mabadiliko ya mipaka hiyo. Mabadiliko ya mipaka yalianza kipindi cha ukoloni, kabla ya Ujerumani kuondoka.
                    
                             Kikwete na Banda
Marekebisho ya mipaka yalifanyika kati ya Ujerumani na Ureno kwa kusogeza mipaka mbele na kutamka, “0.5 KM from the original tripartite point” na vijisiwa vya mto Ruvuma vikagawanywa. Mipaka hiyo ipo hivyo hadi leo. 
Na eneo lingine ni kati ya Uingereza na Ureno, ambapo, kisiwa kilichopo eneo la Malawi kinamilikiwa na Msumbiji mpaka leo na eneo la ardhi lililopo Msumbiji linakaliwa na Malawi. 
Huo ulikuwa mkataba wa marekebisho na ipo hivyo mpaka leo. Kwahiyo, tulivyorithi mipaka, tumerithi na mabadiliko haya na hivyo hatuwezi kugombana na Msumbiji wala Msumbiji hawawezi kugombana na Malawi. 
Mpaka wetu na Malawi haukurekebishwa popote pale mpaka Ujerumani ilipoondoka nchini. Nafikiri viongozi wajiandae pia kwa hili ili tuweze kuwashinda ndugu zetu wa Malawi.
Marekebisho ya mipaka kipindi cha Uingereza:- sote tunajua German East Africa, ni sisi(Tanzania) pamoja na Rwanda na Burundi tuligawanywa katika sehemu kuu mbili.
Mosi, tulipokuwa chini ya League of Nations tukiangaliwa na Uingereza. Kuna mambo nahitaji tuweke sawa ili kuongeza hoja kwa mheshimiwa waziri wa mambo ya nje, Bernad Membe. 
Tulipokuwa chini ya League of Nations, tukaitwa ‘Mandated Territory’, na Uingereza ikawa ni ‘Mandatory Power’. Turudi katika Kamusi tutofautishe “a an annexed colony and a mandate.” 
Mpaka ukawekwa kati ya Ubelgiji na Uingereza, uliitwa The Milner-Orts Agreement of 1922! Naam, katika mkataba huu, mto Kagera ulikatwa katikati , hivyo  hadi naandika makala hii mipaka hiyo tumerithi hivyo. 
Hapakuna mahali popote pale ambapo eneo la ziwa Nyasa kama palirekebishwa kwa njia ya mkataba baina ya Nyasaland State na Tanganyika State.
Isipokuwa tofauti na Mandates zote, Tanganyika pekee, ilikuwa na tofauti ndogo, ambapo mpaka wake wa ziwa Nyasa ukapewa wanachoita 'Wording'. Na hivyo, ramani ya Tanganyika na Official Records zikaonyesha kuwa mpaka umepita katikati ya ziwa Nyasa! 
Hapa ndipo tatizo linapoanza na sisi tumeshindwa kusogea mbele kidogo. Ninachokisema hapa kipo pale National Archives Secretariat Files, Accession Numbere AB 8 na AB 30!

                 
James Zotto akiwasilisha utafiti wake kuhusu mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa.
Nafikiri hotuba yote ya mhehimiwa Waziri Membe imetokana na Files hizo, ndizo walizopelekewa. Ndugu zangu watanzania, ni muhimu kujadili zaidi ya hapo.
Twende mbele kidogo, ni kweli kama mheshimiwa alivyosema katika hotuba yake, ramani nyingi kuanzia mwaka 1922 hadi mwaka 1939 zinaonyesha mpaka upo katikati ya ziwa Nyasa! 
Je, ukweli huu utatutosha pekee mbeleni tukifikishana mbali? Hapana, tuendelee kusaidiana kwa hili, nafikiri ujumbe utawafikia tu.
Waziri Membe hakusema kuwa ramani zingine, japo chache muda huu na Official Reports hazionyeshi mpaka au zinaonyesha mpaka upo chini. Lakini ni chache! Kwanini hili?
Bado natafuta majibu, lakini kwa haraka, tunaweza kusema kuwa Uingereza ilitamani Tanganyika iwe koloni lake na si Mandate! Na pia ilishinikizwa na wawekezaji na hata jeshi ilisema afadhari waiteke ili liwe koloni na waachane na Mandate
Nahitaji tuelewe maana ya mandate. Hii yote ilitokea baada ya gavana Donald Cameroon, wa Tanganyika kusema kuwa “Tanganyika is a part of the British empire and it will remain so”.
Hii ni siasa na si ukweli kama unaelewa maana ya kuwa wao hawakuwa wamepewa koloni kama mali yao, bali kuliangalia hadi wananchi wapate 'akili' ili wapewe uhuru! 
Kwa hiyo na kimsingi, kwa maana ya sheria ya kimataifa, Tanganyika haikuwa Part ya British Empire kama yalivyo makoloni yaliyotekwa moja kwa moja na Uingereza yenyewe! 
Hapa pakatokea mvutano mkubwa sana katika House of Lords na House of Commons! Na hivyo basi, mtafaruku huu wa mipaka ulianzia hapo, hivyo hata waingereza wenyewe walivutana kuhusu mipaka. 
Kwa mfano, mwaka 1926, wajumbe wa mabaraza waliibana serikali iseme mipaka ya Tanganyika na ule wa ziwa Nyasa! Mabishano, kama haya yetu leo yalikuwa makubwa, ila si kwa kutishiana kwa kuwa walikuwa wenyewe na walitaka kuwekana sawa!     
                              
Rais Kikwete na Joyce Banda walipokutana katika kikao cha SADC mjini Maputo, Msumbiji.
Naam, ndipo Secretary of state for colonies alibanwa na mjadala ulikuwa wa kisheria zaidi ukihoji Status of the Mandate, British Empire n.k, na kama waingereza wana mamlaka ya kujipangia kuhusu koloni walilokabidhiwa kuliangalia(nieleweke na sio kulimiliki koloni).
Mwishowe wenye dhamana(Waingereza) walisema kwamba, hata wao wanashindwa kuelewa, 'What exactly is the sovereignty of  Tanganyika lying', jamani mnamwelewa huyu mtu wa kiingereza? 
Kwamaana hiyo, haelewi vizuri mipaka yetu, ambayo wenyewe ndo wameirekebisha au kuipa 'Wording'! hivyo, tatizo linaanzia hapa na si muda mwingine wowote!
Jambo kubwa ambalo Waziri Membe hakusema ni hili: kuanzia mwaka 1939, mambo yalibadilika na hawa hawa watu(Wakoloni) tunaochukua ushahidi kutoka kwao, wakafanya madudu! 
Na ilipoisha vita ya pili ya dunia, jamani oneni haya, hawa waingereza katika ramani zao, tena nyingi mno, tuangalie East Africana Section ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, katika sehemu ya Thesis, kuna Cabins 3 zimejaa ramani na bado ni mpya sana kutokana na kutunzwa na pia kutotumika sana.
Zinaonyesha, bila shaka yoyote, kuwa mpaka wa Tanganyika na Nyasaland unapita pembeni mwa ziwa na sio katikati! Nieleweke naonyesha tu mambo yalivyo ili tuweze kuchukua hatua zaidi. 
Hotuba ya Waziri Membe, iliishia nyaraka za mwaka 1939! Kumbe hawa jamaa walichora tena ramani zote zikionyesha mpaka upo pembeni mwa ziwa! Kwanini hili? Natafuta majibu.
Lakini kwa haraka naweza nikakisia mambo mawili. Mosi, karibu na vita vya pili vya dunia, ilisikika tetesi kule duniani(ughaibuni) kuwa, Ujerumani inarudi na inakuja kuchukua makoloni yake. 
Tukitaka kuhakikisha jambo hili, tusome National Archives of Tanzania, Secretariat Files zote zenye kichwa cha habari, 'The future of Tanganyika in British Empire'
Kwa hiyo, waingereza walihofia kutimuliwa na kurudi kwa wajerumani, na hivyo, wakarudisha ule mpaka wa awali wa mwaka 1890 unaotumiwa tena na Malawi kwa sasa! 
Na pia, katika kipindi hicho, baada ya kumalizika vita hivyo, Tanganyika ikawa chini ya Umoja wa Mataifa(United Nation Organisation), ambapo ilipewa Trusteeship Status!
                            
                                      RAMANI YA ZIWA NYASA.
Maana ya hii ni rahisi kuliko Mandate! Kwanini? Hii ilimaanisha ‘to be granted immediate independence’! maana ya neno ‘immediate’ hapa ni kwamba, kwa tafsiri yangu, waingereza walifahamu wanatimka mapema mno kwani mkataba unasema hivyo.
Nafikiri, wakarudisha ramani zikionyesha mpaka upo pembeni mwa ziwa na kitabu cha ‘Nyasaland’ cha mwaka 1958, kinaonyesha mipaka ya Nyasaland na ziwa lote likiwa kwao! 
SASA TUFANYE NINI WATANZANIA?
Tukitaka kuwashinda watu wa serikali ya Malawi, lazima tukisome vizuri kipindi hiki na tuelewe ukweli, hoja zipi zinawapa kiburi. Na hoja zipi sisi tuzitumie kupambana nao, tunaweza! 
Kwahiyo hatima ya nchi yetu haikujulikani itakuwaje. Kipindi hiki, pamoja na mipaka yake pia, tujiulize, kwa maana ya Mandate, waingereza walikuwa na ‘Legal Authority  'kurekebisha' mpaka wa ziwa nyasa? 
Na je makosa waliyofanya waingereza, ndio Legal backing yetu sisi Watanzania?  Hebu tuzame tena tutafute ukweli zaidi ili tuwashinde hawa jamaa wa Malawi!
Tulishindwana na Uingereza kurekebisha mipaka. Mwalimu Nyerere, alisubiri hadi Malawi ipate uhuru, ndipo akatoa miaka mitatu tu na asingetambua mipaka ya kikoloni(Soma Hansard, 1962). 
Malawi walipopata uhuru, kukawa na matatizo ambayo Waziri Membe aliweza kuyaeleza. Nampongeza kwa hilo, ni dhahiri mwaka 1964 wakati wa mgogoro wa baraza la mawaziri la Malawi, na baadhi ya mawaziri kutorokea nchini kwetu kupitia ziwa Nyasa, Rais Kamuzu Banda akaona ziwa ni infiltration route
                                
                             WAZIRI MEMBE akinawa maji ya ziwa Nyasa mjini Mbamba Bay.
Sera zetu za mambo ya nje za Tanzania zilikuwa tofauti na Malawi. Tanzania ilikuwa nchi iliyoongoza ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, wakati wenzetu Malawi wakaunga mkono Makaburu na Wareno na wakawa na balozi sehemu hizo
Rais Banda akagombana na Mwalimu Nyerere, na matukio ya kutishiana kijeshi yalijitokeza kati ya miaka ya 1967-8; matusi na kejeli zikatawala kati yetu na wao.
Tunakumbuka tuliimba, .....kipara cha Kamuzu Banda kina magamba”, tuliimba tukiwa jeshini hayo. Mwalimu Nyerere  akasema suala mipaka ni hadi Malawi itakapota Sensible Leader akitokea Malawi ndipo tutajadili tena, sio utawala ule wa Kamuzu Banda! 
Kipindi chote hicho tulikuwa kimya, na kuanzia mwaka 1975, hatukuwa na tatizo, lakini sio kusema kuwa tulitatua tatizo la mipaka yetu na Malawi! 
Tulikaa kimya! Mipaka haina tatizo isipokuwa ni time bomb ambapo ikitokea rais mwendawazi akamwaga petroli tu, basi ni vurugu kubwa! 
Tuliirithi kupitia Article III ya Azimio la Umoja wa Afrika la mwaka 1964(OAU Charter, 1964), baadaya ya majadiliano makubwa na wengi wakaridhia “uti possidetis, ita possidetis principle” (so as you exist, so may you exist).
Kama kawaida yetu tulinakili kanuni za mipaka za kibeberu za Westphalia(Westphalia border inviolability)! Hatukupata muda mwingi wa kutafakari na kuangalia kila mpaka na matatizo yake....tulirithi na matatizo na yanatutatiza leo!!!
UTATUZI WA MGOGORO: Tusonge mbele! Nakiri tuna namna tatu ya kulimaliza;- moja ni kwa majadiliano ya kawaida(Diplomacy) kama Waziri Membe alivyosema katika hotuba yake. 
Pili ni kupigana vita (war is another means of diplomacy). Ndugu zangu watanzania nadhani mnataka kuniona kichaa kutamka hilo! Huo ndo ukweli, atakayeshindwa atasalimu kama ilivyokuwa kwa Uganda na sisi watanzania. 
                        
                     WAZIRI WA MAMBO YA NJE, BERNARD MEMBE.
Tatu; ni Mahakama ya Kimataifa(International Court of Justice) hapa nina wasiwasi. Kama nyaraka zenyewe ni zile za Waziri Membe tu, sijui kama tutafanikiwa kushinda kesi.
Tutulie, tuite wataalamu wetu wajikite ndani sana. Ni kweli kama alivyosema Waziri Membe kwenye hotuba yake kwa kunukuu kesi nyingi na zilizoshinda, na kwa kusema kuwa, tukienda mahakama ile sisi ndo tutashinda. 
Nina shaka, tumejipa favour  ya verdict, kabla ya kesi. Sijui, ila nina shaka kubwa, kuna kushinda, kushindwa au suluhu! Ninashaka tena na tena!
Mimi ni mzalendo, nataka ukweli kwa njia ya mahojiano na kuumiza kichwa, tutetee mali zetu tukijua tunawashinda kwa hoja.
WASIWASI: Inasemekana kuna mafuta ziwani,  kwahiyo tujue Marekani na washirika wake hawako mbali! Kampuni ya Surestream ya Uingereza ndio ilipewa leseni ya kutafiti mafuta na utawalawa Bingu wa Mutharika.
Lakini, tujue operesheni ya majeshi ya kibeberu na huyu mama Joyce Banda, ambaye ni mpwa wa Kamuzu Banda, anapata wapi hiki kiburi? Nyuma yake kuna nini na nani? Tuangalie haya pia. 
HITIMISHO: Tusiwe na hoja moja tu mkononi kama ndio water-tight evidence yetu kwa serikali na wananchi kwa ujumla. Tujaribu kuzibishanisha hoja zetu. Na hoja nzuri ni zile zinazopingana nasi na tusizozipenda, tukizielewa na kuzikubali ndipo tutajipanga namna ya kuzigalagaza. Tumwelewe vizuri adui yetu. Mungu ibaraki Tanzania, ziwa Nyasa, wanyasa, na watanzania! Tusing'ang'anie tu Reparian Law.
James Zotto ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM). 

October 17, 2012

HARAKATI ZA MAENDELEO WILAYA YA NYASA, KARIBU KUWEKEZA


Wilaya ya Nyasa ni miongoni mwa Wilaya mpya zilizoanzishwa na serikali ya awamu ya nne. Habari za kuundwa wilaya ya Nyasa nilianza kuzisikia mwaka 1993 nikiwa shule ya msingi. Lakini mwaka huu Wilaya ya Nyasa imezinduliwa rasmi na shughuli za maendeleo zinaendelea ili kukidhi mahitaji ya wananchi. Katika harakati hizo ni pamoja na huduma ya Maji ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya hiyo. Hapa ni picha mbalimbali ambazo zinaonyesha suala la upatikanaji wa maji katika vijiji mbalimbali wilayani humu.  Bila shaka wageni na wenyeji watavutiwa kuwekeza katika wilaya mpya ambayo fursa mbalimbali zinajitokeza. karibuni. Picha zote na Hoops Kamanga
 Chanzo cha Mradi wa maji kikifanyiwa ukaguzi.
 Tenki la Maji katika mradi wa maji katika kijiji cha Ng'ombo wilaya ya Nyasa
 Mradi wa Maji katika kijiji cha Kindimba Juu ambao umekamilika na wananchi wanategemea kutumia siku chache zijazo. Hapo fundi anamalizia marekebisho katika tenki.

May 06, 2010

KAZI UKIIPENDA,ITAKUPENDA

                                             Kazi ni kuipenda
Maisha ndivyo yalivyo lakini mpangaji ni wewe. Ukiipenda kazi yako nayo itakupenda. Ukiithamini kazi yako nayo itakuthamini, ukiheshimu kazi yako nayo itakuheshimu.
Kazi ni kazi bora mkono kwenda kinywani, lakini siyo kazi yenye dhuluma ukadai bora mkono unakwenda kinywani, bali kazi ni ile halali na uifanye kwa uhalali.


Kazi yoyote ni kuipangilia, na zingine hazina ofisi ambayo utakaa kuandika kwa kalamu ya wino. Kwetu hapa nyasa kazi yetu na ofisi yetu ni mtumbwi ambao kalamu yake ni ngalawa/kafia.
Kazi hii ni ngumu lakini ndiyo inayoweza kutupatia kipato na kupanga maisha.
Kazi ukiipenda nayo itakupenda, hata kama ni ndogo aghalabu inakupa heshima.
Ndipo unapomkumbuka Vilfredo Pareto, mchumi wa kitaliano katika '2080 Theory', kwamb asilimia 20 ya mipango yako ni sawa na asilimia 80 ya matokeo'.


Ukiifanya kazi kwa bidii,maarifa na kwa asilimia zote, itakuletea ufanisi. Ufanisi unatokana na juhudi ndiyo maana hatuachi KUVUA SAMAKI. Najua jamaa zangu wa pale bandarini Chilumba, Malawi hawaachi na serikali yao imewaletea zana mpya. Hongereni. Lakini sisi tunatumia mitumbwi ya zamani na tuna uhakika wa kufanikiwa labda.

January 03, 2009

Mandhari na Maudhui

Uzuri, Maudhui na Mandhari ya maeneo ya milima ya kaskazini mwa mbamba bay. yaani toka maeneo ya Kilosa, Matenje, Kwambe, Ng'ombo, Chamate, Linda, na mengineyo. Miinuko na vilima

October 01, 2008

zana za kazi hizi

Mitumbwi imetu;lizana baada ya kazi yake

September 14, 2008

nakupenda nyasa yangu.....upendo wa dhati

karibuni nyasa, unajua wakati mwingine naishiwa maneno ya kusfia labda mna wivu mno hata nashindwa kusifia. kazi kwenu

hata hivi pia inawezekana

wanyasa ni mafundi wa kufinyanga vyungu kama hivi, karibuni sana bei ni poa kabisa wala msijali sana

August 14, 2008

kama kawaida yetu kuvua

hapo ni kama kawaida na shughuli za nyasa yetu kuvua kwa mitumbwi.umeona hiyo au haionekani

July 09, 2008

Nimesahau!Ah Nyasa pale.....

June 04, 2008

Mshashi Anavinjari Nyasa

Inaelekea huamini kama nyasa Washashi wanakuja kuselebuka..Bisha na hii.Halafu kuna jamaa anapenda sana kupingapinga mambo sasa nampa ngumi ya tumbo,sikio na mbavuni aaah samahani nilisahau bado sijapona ile ngumi ya ukutani ya yule jamaa.Hebu mwangalie Bibie huyo,anakukuna sana?eeeeh usije ukatangaza ndoa..wala sihusiki,lakini ananiambia anataka mvulana mwenye mwanya,je unao?

June 03, 2008

Niambie Mnyasa Mwenzangu Maana Hawaamini

Tazama kwa umakini halafu jiulize wapi hapo....jibu ni Nyasa yetu ndugu

June 02, 2008

Uoto wa Asili Nyasa Yetu...Karibu jionee

Angalia kunavyopendeza,angalia uoto wa asili,majengo ya asili.Lakini hapo ni makazi ya muda mfupi, unajua wanyasa huwa wanakwenda kuvua samaki mahli ambako hakujavulia siku nyingi?Basi wakifika huko hujenga nyumba kama hizo.Karibuni nyasa jamani yaani hapo tu sijawawekea wale wamisionari walioishi huku enzei zile za wale wahuni kutoka ulaya na wizi wao.Lakini kwetu walikuwa mapadre na mabruda.Mmh inanikumbusha nikiwa na ndoto ya kuwa Padre au bruda lakini samaki walinizidi kete wakanipa hamu ya kuvua.Muulize dada pale ruhuwiko{tafuta kwenye ukurasa wa Tovuti/blogu}bloguni akupe hamu ya wanyasa kuingi katika Monesteri za kijerumani..Mhh ngoja nikumegee msomaji unajua dadangu huyu alitaka kuwa nani?Utajiju nenda kaone pale Chipole misheni halafu utaniambia lakini usije ukanisingizia nimekwambia mimi..wala tena najificha uvunguni mwa kitanda...aaaah nimekumbuka kitu najua utasema mbona leo nina usongo wa kublogu...jibu sijaandika siku nyingi nimekuja na ari ya zamani,nguvu za zamani na kasi ya zamani.Naenda kula ugali na dagaa leo,tena jana jumapili nimekula

April 30, 2008

Bado Hasira hazijaisha kwani nakumbuka sna Nyasas

Unajua kipi kinachonikasirisha hapa?aa samahani siyo hapa kwenye blogu yangu bali huku ninakoongeza kaelimua Mlimani chuo kikuu cha Dar es salaam.LKulikuwa na mgomo na vurugu za hapa na pale watu wanalilia haki halafu watawala wahuni na wasiojali utu wa wanafunzi wanakandamiza uhuru wa kufikiri.Ngoja nikomee hapa kwani ukisoma mengi utasema nimehama nyasa yangu na kuandika yasiyonihusu.Nyasa napakumbuka kwasababu ni nyumbani na napapenda kuliko chochote.Ngoja kuna habari nimezipata kwa wanyasa nitaandika

April 20, 2008

Ziwa Limechafuka,Wanyasa na Ngalawa Tu

Nilikaa juu ya jiwe nikiangaza huku na huko kuwatazama wanyasa wanavyohaha katika shughuli zao za maisha ya hapa na pale.Nikaona ngalawa zinaumiza vifua vya wanyasa kwani hali siyo nzuri katika ziwa kwa sasa.Hakika ziwa nyasa limechafuka namaanisha dhoruba kali sana wiki hili,kila myasa/mvuvi unayemuona kanuna,kafura kama chatu ghadhabu imejaza vibaba wala haimithiriki zaidi ya hapo,hawacheki.Ziwa linanguruma mawimbi makali makali,nyavu zinapotea nyakati hizi shauri maboya yanazama kwa kushindwa kuhimili nguvu ya mawimbi.Lakini pamoja na kuchafuka kwa ziwa hilo hakuna hata mvuvi anayethubutu kusema atabaki nyumbani kujipumzisha au kurejesha zana za uvuvi nyumbani ili kupisha dhoruba hiyo,wapi bwana sahau kabisa habari ya wanyasa kuogopa dhoruba nyakati hizi au kuacha ngalawa ili kukosa kitoweo,hakuna mnyasa anayefikiri kula nyama za kuku wasiokomaa,wanaotafunika hata mifupi,wanaokuzwa kwa kudungwa sindano,wanatia kinyaa kuwala,au chipsi za huko mijini.Wanyasa wanaelewa uzuri wa kuwa wajuzi wa ziwa hili ambalo wenyewe wanasadiki kuwa hakuna ziwa lenye dhoruba kali ulimwenguni zaidi ya hili.Hakuna aliyeka chini kuacha ngalawa au kuacha kupanda mitumbwi.Yaani uvuvi unaendelea kana kwamba ziwa lipo shwari wakati "limekasirika" utafikiri limedungwa sindano ya kukasirika.Yote hao ni kitoweo cha asili hiki utamu adimu huu.

October 07, 2007

Ng'ombo;nyasa na habari zake

NG'OMBO ni kijiji kilichopo kandokando mwa ziwa nyasa.Kijiji huku kunapakana sana na Mtupale na kwa wasiofahamu wanadhani ni mtaa tu fulani huku wakijua mtupale ni kijiji kamili,kumbe hiki ni kijiji kamili na kina historia yake tokana wamisionari kujenga hospitali hapo toka zama zao za ukoloni na hadi leo inawasaidia wakazi wake.Shughuli kubwa hapa ni kama vijiji vingine yaani kilimo,uvuvi na ufugaji.Ni eneo lenye kupendwa sana na walevi kwani hujukusanya katika eneo lao la 'malini' kwa kujiburudisha au kushuhudia burudani mbalimbali za ngoma kama kioda,mganda,makanya n.k hizi ni ngoma za utamaduni ambazo huipendwa na wakazi wake.Uzuri wake ni kama vingine kwani hakuna uchafuzi wa hali ya hewa kama maeneo ya mijini,ni eneo linalofaa kwa kilimo cha mpunga ambacho wakazi wake wamekuwa wakijipatia kipato tokana na kilimo hicho.Ulimaji mwingine ni ule ulezi,mihogo na matunda.matunda ni mengi sana katika vijiji vya mwambao mwa ziwa nyasa tokana hali yake ya hewa kuruhusu ya baridi ambayo ni nzuri kwa kilimo chamatunda.Samaki ni wengi sana na dhana zitumikazo ni za asili mfano mitumbwi ambayo ni tegemeo kuu kwani huwezesha utunzaji na ulinzi kwa samaki ziwani.kifupi hiyo tu karibuni nyasa