NA KIZITO MPANGALA
TUNASIKILIZA muziki wa Nigeria
mara kwa mara na pengine huenda uliwahi kujihoji aina lugha wanayotumia kuimba
na hata katika mazungumzo ya kwaida ya wananchi wa Nigeria. Mtindo huo umejaa
pijini kwa kiasi kikubwa hali iliyopelekea kuitwa NIGERIAN ENGLISH.
Fela Anikulapo Kuti alizaliwa mjini Abeokuta nchini Nigeria mwaka 1938. Alipewa
majina OLUFELA OLUSEGUN OLUDOTUM RANSOME ANIKULAPO KUTI lakini alifupisha na
kuwa FELA ANIKULAPO KUTI. Mama yake alikuwa ni mwanaharakati wa haki za
wanawake katika utawala wa kikoloni wakati huo, na baba yake alikuwa ni mwalimu
na vilevile alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza mweusi wa chama cha walimu
nchini Nigeria. Fela ni binamu ya Akimwande Oluwole Babatubde Soyinka maarufu
kama Wole Soyinka.
Fela alisoma nchini Nigeria na
baadae mwaka 1958 alikwenda nchini Uingereza kwa ajili ya
kusoma Udakitari wa Dawa lakini alipofika huko alivutiwa na masomo ya muziki
hivyo akasoma masomo hayo ya muziki katika chuo cha Trinity. Fela alikuwa mjuzi
wa kupiga tarumbeta na Saxophone.
Alianzisha bendi yake iliyoitwa
Koola Labitos ambayo ilipiga muziki aina ya jazz. Huko alimuoa mwanamke aliyeitwa Remilekun
Taylor na wakawa na watoto watatu. Mwaka 1963
alirudi nchini Nigeria na kuendelea na bendi yake aliyoianzisha na pia utangazaji
katika shirika la utangazaji redioni la Nigeria.
Mwaka 1967
alihamia nchini Ghana na kuanzisha mtindo mpya wa muziki ambao uliitwa
Afrobeat. Mwaka 1979 alisafiri kwenda
Marekani na alikaa kwa muda wa miezi 10 jijini
Los Angels, huko alibadili jina la bendi yake na kuitwa NIGERIA 70. Baadae
alitimuliwa nchini humo pamoja na waimbaji wenzake kwa kutokuwa na kibali cha
kufanya kazi nchini humo.