Showing posts with label warsha. Show all posts
Showing posts with label warsha. Show all posts

October 21, 2017

MBUNGE WA CHEMBA AONDOA HOJA YA KUONGEZA MUDA WA UBUNGE

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MBUNGE  wa Chemba Juma Nkamia (CCM)amesema ameondoa kwa muda kusudio lake la kutaka kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba unaohusu kuongeza ukomo wa Bunge. 
JUMA NKAMIA
Nkamia ambaye aliwasilisha kusudio hilo  katikati ya mwezi uliopita mjini Dodoma kwa mujibu wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016,kupitia barua yake aliyoisaini Septemba 12  iliyokuwa ikipendekeza kuongeza muda wa bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kupunguza wa uongozi wa vijiji kutoka miaka mitano hadi minne.

Kupitia ujumbe mfupi aliouandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp,alisema ameamua kuondoa kusudio hilo  baada ya mashauriano  na maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).

“Ndugu viongozi wenzangu naomba kuwataarifu kuwa baada ya mashauriano na maelekezo  ya viongozi wa juu wa chama(CCM) na hali ya kisiasa  katika nchi kadhaa za Afrika  Mashariki  nimelazimika kuondoa kwa muda hoja yangu binafsi ya ukomo wa Bunge niliyokusudia kuiwasilisha katika bunge lijalo,”aliandika Nkamia.

Mbali na andiko hilo gazeti hili pia lilimtafuta Nkamia kupitia simu yake ya kiganjani ili kumuuliza kama  na sababu nyingine zaidi ya alizozitaja kupitia ujumbe  huo mfupi na lini atakuwa teyari kuwasilisha tena muswada huo alisema.

“Naomba ibaki hivyo hivyo kama ilivyo kwenye meseji  sina cha kuongeza,kuhusu ni lini nitapeleka tena nayo subiri kwa sababu nimesema nimesitisha kwa muda maana yake nitawasilisha tena nitakapokuwa teyari,”alisema Nkamia.

Hoja ya  Nkamia ambayo ilianzia  katika Bunge lililopita ilikuw aikipingwa na wanazuoni pamoja na wanasiasa wakongwe akiwemo Spika Mstaafu wa Bunge Pius Msekwa.

Msekwa ambaye alikuwa akiongea na televisheni ya Azam  mwishoni wa wiki hii alisema  chama cha CCM hakiwezi kukubaliana na maoni au mpango wa kuongeza muda wa kiongozi yeyote kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kikatiba kwa sasa.

Msekwa alisema kwa uzoefu wake bungeni tayari anaona kuna tafakari nyingi zilizofanywa kabla ya Taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano na si vinginevyo.

Alisema hoja hiyo inabidi iangaliwe kwa umakini mkubwa kutokana na ukweli kuwa, iwapo kiongozi atakuwa mbaya, maisha yanaweza kuwa ya mateso kupitia kiongozi huyo na kuongeza kuwa hilo hata Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere aliliona hilo.

“Ni kwamba miaka kumi tu inatosha, ili kama mtu ni mbaya tuvumilie kwa hiyo miaka kumi, na siyo kwamba haikufikiriwa. .na sidhani kama CCM itakuwa na nafasi ya kujadili hilo kwa sasa” alisema Msekwa. Mbali na Msekwa wasomi wakiwemo Dk.Benson Bana nao walimpinga huku akisema kuwa lengo lake lilikuwa ni kujipendekeza kwa Rais Dk. John Magufuli ili ampe uwaziri.

October 10, 2011

FREDDY MACHA NDANI YA DAR ES SALAAM+RATIBA YA WARSHA ZAKE

Freddy Macha akizungumza na waziri wa mambo ya nje Bernad Membe
Freddt Macha akiwa na wanafunzi wa sekondari ya Mwandege mkoani Pwani mwaka 2009. Sasa yuko nchini, fuatilia ratiba yake hapo chini.
WARSHA NA  FREDDY MACHA

Moja kwa moja toka London; mwanamuziki na mwandishi huyu Mtanzania atafanya semina ukumbi wa Fasdo, Tandika,  Dar es Salaam, Jumanne tarehe 11 na Jumatano  12, Oktoba, 2011.

Mwenyeji:
Fasdo:  (Faru Arts Development Organisation)
Mawasiliano : Chande Nabora: Simu 0713-310755
Nasibb: 0713-261011 

Mada

1.    Utafanikishaje afya yako? Chakula (kula sawasawa), mazoezi mbalimbali na mambo mengine kibao.

2.    Mtu anawezaje kutoka kwao kuishi ughaibuni na akafanikiwa? Mambo ya msingi unayohitaji kuelewa. Yalete maswali na mambo yanayokusumbua kuhusu suala hili.

3.    Je, unataka kuwa mwanamuziki?  Kwenu nyinyi wote wasanii wa leo na kesho, njooni mpokee vidokezo na ushauri.

4.    Je, unataka kuwa mwandishi msanii au mwanafasihi? Siri za kukufanya uwe bora zaidi ya wengine! Ongeza kipato chako kupitia uandishi wa kimataifa.

5.    Kukua na maendeleo ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza

6.    Ukumbi wa Maswali na Majibu

Mhusika

Freddy Macha ni mwalimu, mwandishi wa insha na habari, mwanafasihi, mtunzi wa vitabu, mkalimani, mwanamichezo, msingaji, mwanablogu na mwanamuziki.  Hapa Tanzania anajulikana zaidi kama mwanasafu, aliyeanzia kazi magazeti ya Uhuru na Mzalendo, 1976-1978;  akajenga jina na safu ya kila jumapili Cultural Images gazeti la Kiingereza, Sunday News 1981-84. Kuanzia 2003 amekuwa akiandika kolamu kadhaa nchini ikiwemo : Kalamu Toka London kila jumapili gazeti la Mwananchi na Chat from London gazeti la Kiingereza, The Citizen kila Ijumaa.
Anazo blogu kadhaa ; na hufanya kazi za usingaji, muziki, mtafiti na mtangazaji wa runinga mbalimbali za mtandaoni  mathalan Urban Pulse Creative Media na Global Fusion Music and Arts, Greenwich, London.

Baadhi ya kazi kuu alizozitoa:-
Ø  2006, kitabu cha Mpe Maneno Yake,  hadithi fupi fupi za Kiswahili alizokusanya miaka 30 katika nchi nyingi alizoishi na kuchapishwa na E & D Limited, Dar es Salaam.
Ø  2001,  Wimbo wa “Kilimanjaro” na bendi ya Kitoto, London.

Ø  2000, CD ya muziki na fasihi –Constipation- iliyotolewa na kusifiwa na majarida kadhaa Ulaya.

Ø  1996, hadithi yake “Nilipomuua Nyoka” (When I Killed a Snake) kwa Kiingereza ilichukua nafasi ya pili katika Tuzo la Jumuiya ya Madola, London. 
Ø  1995,  alitoa CD ya muziki na fasihi– Kitoto- Quebec, Canada.
Ø  1986 alichapisha mwenyewe mashairi  ya Kiingereza na Kijerumani (Papers! Papers! Papers! ) Cologne, Ujerumani.
Ø  1985, alichapisha kitabu cha maisha ya mwanamuziki Remmy Ongala.
Ø  1984, mkusanyiko wake wa hadithi fupi za Kiswahili : Twenzetu Ulaya (Gap, Dar es Salaam).

Ø  1981, mashairi yake ya Kiingereza yalishinda tuzo la BBC.

Ø  1979, alisaidiana na wenzake kuanzisha jarida la  Wimbi  lakini kutokana na sababu mbalimbali  hawakufanikiwa.
Maisha Ughaibuni
Alitoka Tanzania mwaka 1984 na bendi ya Sayari iliyochanganya muziki, dansi, ngoma, mashairi ya maonyesho na tamthiliya  wakazuru nchi za Scandinavia (Sweden, Norway, Denmark).  Baada ya miaka michache Ulaya alienda zake kusomea muziki, Brazil huku akipigia  bendi kadhaa hadi 1994 alipohamia Canada na hatimaye Uingereza.
Habari  zaidi na video zake tembelea : www.freddymacha.com