Showing posts with label Historia. Show all posts
Showing posts with label Historia. Show all posts

March 23, 2018

LAURA BASSI: PROFESA WA KWANZA MWANAMKE BARANI ULAYA.

Na Kizito Mpangala

Wanawake wanayo nafasi ya kufikia malengo ambayo wanakusudia, ni kwa juhudi na maarifa wataweza kufikia malengo hayo. Suala la kipaumbele kwa wanawake duniani kote limepitia hatua kadhaa za ushawishi na changamoto kadhaa ambazo hasa huwakabili wanawake wenyewe. Katika uga wa sayansi na teknolojia, ni wanawake wachache ambao wamefikia malengo yao ugani humo. Hata sasa uhamasishaji bado unaendelea duniani kote.

Haikuwa kazi rahisi kwa mwanafizikia Laura Caterina Bassi kufikia kiwango cha profesa wa Fizikia katika chuo kikuu cha Bologna nchini Italia.
Laura Bassi alizaliwa mwaka 1711 mjini Bologna nchini Italia ambapo baba yake alikuwa mwanasheria. Laura Bassi alifundishwa nyumbani na mwalimu aliyeajiriwa na familia yake kwa muda wa miaka saba. Alianza kufundishwa akiwa na umri wa miaka 13. Mwalimu wake, Gaetano Tacconi, alimwelekeza zaidi katika sayansi na hisabati ndipo Laura alipoingiwa na hamu ya kutaka kujua zaidi yaliyomo katika sayansi.

Kutokana na msukumo aliokuwa nao katika sayansi, Laura alivutiwa zaidi na somo la Fizikia ambapo alijifunza zaidi kuhusu Sayansi ya Newton (Newtonian Science) ingawa mwalimu wake alitarajia kwamba Laura atajikita zaodi katika hisabati, lakini haikuwa hivyo.
Laura Bassi, katika juhudi zake za masomo alilazimika kusoma pia hisabati ili kujiimarisha katika Fizikia. Hapa Laura alimuomba binamu yake, Padre Lolenzo Stegani, amfundishe hisabati. Padre Lolenzo Stegani alikuwa akijua hisabati na lugha ya kilatini. Kwa kuwa vitabu vingi viliandikwa kwa lugha ya Kilatini, Laura alipaswa kujifunza sarufi ya lugha hiyo na baadae akafundishwa hisabati kwa lugha ya Kilatini.

Baada ya kuweka juhudi zaidi katika elimu hiyo ya sayansi, mwaka 1732 Laura aliandika kazi yake ya kwanza ambayo aliitetea mbele ya hadhira katika mihadhara mbalimbali katika ukumbi wa Pazzalo. Hiyo ilikuwa dira yake ya mafanikio ya elimu aliyokuwa akiitafuta zaidi.

February 17, 2018

WIKIENDI NJEMA WASOMAJI WETU NA PICHA ZA MAENEO YA UZAMIAJI WA SAMAKI LUNDU, NYASA

Eneo hili ni miongoni mwa yanayotumiwa na wazamiaji wengi kupata samaki. Uzamiaji wa samaki katika eneo hili hutafutwa samaki wa mapambo. Kijiji cha Lundu hutumika sana kutafuta samaki wa mapambo. Kuna samaki wazuri mno wanaotafutwa hivyo wazamiaji hutegemea kijiji hiki kujipatia samaki hao.
Watoto wakioposha samakini karibu na jiwe Stima (Liganga Stima).

SOLOMON MINTUS NORTHUP: MTUMWA ALIYEMPIGA MNYAPARA WAKE NA KUANDIKA KITABU KUELEZA MAISHA YAKE YA UTUMWA MIAKA 12.

Na KIZITO MPANGALA
Solomon Northup alizaliwa mwaka 1807 katika mji wa Essex (sasa ni New York), Marekani. Alizaliwa kwa wazazi walioachiliwa huru katika mashamba ya pamba, Louisiana. Baba yake alipokuwa mtumwa asiye huru katika mashamba ya pamba ya tajiri Henry Northup aliaminika katika kazi hiyo. Baada ya kuachiliwa huru aliamua kutumia jina la mnyapara wake, Henry Northup kama jina la pili katika kizazi chake kilichofuata. 

Hapo alimwongezea Solomon Mintus jina la NORTHUP na kuwa SOLOMON MINTUS NORTHUP. Mzee Mintus aliachiliwa huru kwa sababu alimuoa mwanamke chotara katika mji wa Minerva mjini Essex ambaye alikuwa na asili ya Afrika na Ulaya, hivyo weupe ulimzidi na kwa weupe huo alitendewa kama mtu wa kutoka Ulaya. Ndipo Solomon Mintus Northup alipozaliwa akiwa mtumwa huru pamoja na mdogo wake Joseph Mintus Northup kadiri ya sheria ya “Partus sequitur ventrem” ambayo ilirithiwa na koloni la Uingereza nchini Marekani kutoka katika Dola la Warumi (Roman Empire). Sheria hiyo humaanisha “yeyote aliyefika sehemu fulani anapaswa kufuata utaratibu (kanuni au sheria) unaofuatwa katika eneo hilo” ni kama vile kusema “ukiwa katika ardhi ya Warumi ishi kama Mrumi”

Solomon Mintus Northup alikuwa akimwelezea mama yake kuwa ni robo ya Mwafika na robo-tatu ya Mzungu anayeishi Amerika. Baba yake alifanikiwa kumiliki ardhi baada ya kuwa huru. Alijiwekea utaratibu wa kuwekea akiba ya fedha na kupata mahitaji ya lazima kwa familia yake. Pia aliwasomesha watoto wake wawili, Solomon na Joseph. 

February 12, 2018

LEVARDIS ROBERT MARTYN BURTON JR: MSEMINARI ALIYEUVAA UAFRIKA KWENYE FILAMU YA “ROOTS” KWA JIN LA KUNTA KINTE.

Na Kizito Mpangala

Ukimtazama hata kwa picha utasema ni mzaliwa halali wa Gambia kutokana na mwonekano wake katika filamu iliyomlazimu kuwa Mgambia.
Alizaliwa mwaka 1957 nchini Ujerumani Magharibi (sasa Ujerumani) kwa wazazi Levardis Robert Martyn Burton Sr na Erma Gene. Baba yake alikuwa ni mpiga picha wa jeshi la Marekani katika kituo cha afya cha Landstuhl cha jeshi la Marekani nchini Ujerumani. Mama yake alikuwa mwelimishaji wa jamii.

Burton Jr na dada zake wawili walilelewa na mama yao katika mji wa Sacramento jijini Calofonia nchini Marekani huku baba yao akibaki Ujerumani kikazi.
Burton Jr alivutiwa na kujiunga na Seminari na hivyo akakubaliwa kuanza masomo katika Seminari ya Mtakatifu Pius X katika kitongoji cha Calt jijini Califonia kwa lengo la kuwa padre.
Alipokuwa Seminarini, alipenda kusoma vitabu vya falsafa na kufanikiwa kuwasoma wanafalsfa kadhaa Seminarini hapo. Katika falsafa hizo, alivutiwa na kuwasoma kazi za wanafalsafa Lao Tzu, Nietzsche na Kierkegaard ambazo zilimfanya awahoji walimu wake kama Ukatoliki ndiyo dhehebu pekee kweli.
Alipofikia umri wa miaka 17 alihitimu katika Seminari hiyo na kuamua kujiunga na chuo kikuu cha Califonia Kusini kwa masomo ya sanaa. Alitunumiwa shahada ya kwanza ya sanaa huku akijikita katika uigizaji.

JOSEPHINA MARGARET BAKHITA: MTAKATIFU MWAFRIKA ALIYEPONEA MIKONONI MWA MAHAKAMA YA ITALIA.

NA KIZITO MPANGALA

JOSEPHINA Margaret Bakhita alizaliwa mwaka 1869 mjini Darfur kitongoji cha Olgassa nchini Sudan katika jamii ya kabila la Daju. Baba yake aliheshimiwa sana kwa kuwa alikuwa ni kaka ya Chifu wa kabila hilo. Bakhita aliishi kwa furaha akiwa hajui mateso ya kitumwa yanakuwaje.
Alipofikia umri wa miaka minane, alitekwa na Waarabu wafanyabiashara ya utumwa ambao tayari walikwishamteka dada yake miaka miwili kabla ya kumteka Bakhita mwenyewe. Alilazimishwa kutembea mwendo wa kilometa 960 peku kutoka Darfur hadi El Obeid. Kabla ya kufika El Obeid alikuwa ameuzwa mara mbili njiani.

Bakhita alipofikia umri wa miaka 12 alikuwa ameuzwa tena mara tatu na kisha kusafirishwa mpaka Uturuki. Huko alikumbwa na mateso mengi na uchungu hali iliyompelekea kusahau jina lake la asili na hivyo alilazimika kutumia jina alilopewa na Waarabu, Bakhita likimaanisha mtu mwenye bahati. Kisha akasilimishwa.

Bakhita alinunuliwa na tajiri wa biashara ya watumwa ambaye alikwa Mwarabu na kumtumikisha kama mfanyakazi wa kuwahudumia binti zake wawili ambao waliishi nae vizuri. Alipokorofishana na mtoto wa kiume wa Mwarabu huyo alipigwa na kufikia hatua ya kushindwa kutembea kwa muda wa mwezi mmoja. 

February 03, 2018

JOHN LANGALIBALELE DUBE: MWANAFUNZI ALIYEAMINIKA KUWA NA TABIA CHAFU CHUONI MWASISI WA CHAMA CHA ANC, AFRIKA KUSINI.

Na Kizito Mpangala

John Langalibalele Dube alizaliwa mwaka 1871 kwa wazazi James Dube na Elizabeti Dube katika kitongoji cha Inanda,kwa sasa ni mkoa wa KwaZulu Natal. Jina lake la katikati yaani Langalibalele alipewa na wazazi wake likimaanisha “mwanga wa jua”. Baba yake alikuwa mchungaji katika kanisa la misheni ya Waamerika walioishi katika jamii ya Wazulu.
John Langalibalele Dube

Baba yake alikuwa kiongozi wa kabila la watu wa Qadi katika jamii ya Wazulu na jina lake lilikuwa Ngcobo Dube. Baada ya ujio wa Wamisionri alimua kujiunga na Ukristo na kisha akabatizwa kwa jina la JAMES DUBE. Huo ndio ulikuwa mwisho wa kuliongoza kabila hilo. John Langalibalele Dube alikuwa Mwalimu, Mhariri, Mpigachapa, Mshairi, Mwanafalsafa, Mwandishi wa Insha, na mwanasiasa nchini Afrika Kusini. 
 
John Langalibalele Dube alianza masomo katika kitongoji cha Inanda, na baadae akajiunga na chuo cha Adams (Adams College) kitongoji cha Amazimtoti kusini mwa mji wa Durban nchini Afrika Kusini. Akiwa chuoni hapo, walimu walipeleka lalamiko kwa wazazi wa John kwamba kijana wao ana tabia chafu chuoni hapo ambayo haiendani na sheria za chuo. Ndipo Mchungaji William Cullen Wilcox alipoteuliwa kuzungumza na kumkanya John Langalibalele Dube kwa tabia zake chafu (haikuwewa wazi ni tabia zipi hasa alizokuwa akizifanya). John alifuata nasaha alizopewa na kisha akabadili tabia.

Wamisionari wa Amerika walioondoka katika kitongoji cha Inanda, John aliambatana nao na kujiunga na chuo cha Oberline nchini Marekani. Aliambatana nao kwenda Marekani baada ya kupata ruhusa kutoka kwa baba yake Mzee James Dube ambaye alikuwa mchungaji na kiongozi katika chuo cha Adams. Wamisionari hao walikubali kwa sharti kwamba hawatamhudumia chochote kifedha, hivyo Mzee James Dube alipaswa kuingia mwnyewe mifukoni mwake.

GARETT AGUSTUS MORGAN: MJASIRIAMALI ALIYEVUMBUA TAA ZA KUONGOZEA MAGARI BARABARANI.

Na Kizito Mpangala

Garett Morgan alizaliwa mwaka 1877 katika kitongoji cha Claysville mjini Kentucky nchini Marekani akiwa na asili ya Afrika yaani. Baba yake alikuwa mtumwa aliezaliwa katika kitongoji cha Huntsville mjini Alabama. Baba yake alikuwa mtumwa kwa kurithishwa na wazazi wake waliokuwa watumwa. Miaka kadhaa baadae baba yake, John Morgan akawa Luteni Kanali wa jeshi la Marekani, Brigedia Jenerali katika jeshi la Kentucky kwa lazima. Mama yake Garett Morgan pia alikuwa mtumwa kama mume wake.

Garett Morgan alipofikia darasa la sita katika shule ya Brach Elementary mjini Claysville akiwa na umri wa miaka 16 alikwenda katika kitongoji cha Cincinnati mjini Ohio kutafuta kazi itakayompa ujira ili kupata mahitaji yake. Aliajiriwa mashambani.

Kama ilivyokuwa kawaida ya watoto wengi nchini Marekani wakati huo, Garett Morgan alilazimika kuacha shule akiwa darasa la sita na kuamua kufanya kazi katika mashamba kutwa nzima. Kutokana na bidii yake katika kazi, aliletewa mwalimu awe anamfundisha hapohapo shambani ambako ndiko yalikokuwa makazi huku akiendelea na kazi za shambani huko. 

Alifundishwa ufundi na baadae akawa fundi mahiri wa kutengeneza mashine za kushonea nguo yaani cherehani. Uzefu huo wa kutengeneza cherehani aliuheshimu na kujifunza zaidi jinsi mashine zinavyofanya kazi. Kazi yake ya kwanza kuvumbua ilikuwa ni cherehani inayotumia mkanda kama cherehani za sasa. Alivumbua cherehani hiyo tofauti na za mwanzo zilizokuwa zikizungushwa kwa mikono.

GEORGE CRUM: MPISHI MASHUHURI ALIYEVUMBUA CHIPSI YA VIAZI

NA KIZITO MPANGALA

Alizaliwa mwaka 1824 katika mji wa Saratoga, sasa ndilo jiji la New York nchini Marekani. Alijishughulisha na uwindaji na upishi katika migahawa ilikuwa katika milima ya Adirondack. Alifanya shughuli hizo kwa bidii lakini baadae alielekeza nguvu zake zaidi katika upishi. Jina lake lilikuwa ni George Speck. Kutokana na jina la uchepe kushamiri zaidi ambalo ni Crum, aliamua kujiita George Crum.

Baba yake aliitwa Abe Speck ambaye alikuwa mhamiaji kutoka Kentucky kwenda Saratoga. Akiwa Saratoga alimuoa mwanamke mwenye asili ya India ambapo baadae George alizaliwa. 

Bidii yake ilipoonekana zaidi, alichukuliwa na tajiri mmoja katika mgahawa ulioitwa Moon’s Lake House, karibu na maporomoko ya maji ya Saratoga. Mgahawa huo uliaminika kuwa ndio wenye gharama za juu za chalula. Hapo ndipo ujuzi wake wa upishi ulipofahamika na watu wengi zaidi. Licha ya kuwa na gharama za juu katika mgahawa huo watu walipenda kufika kwa wingi kutokana na umahiri wa George Crum katika upishi wake.

Bada ya kufanya kazi kwa muda mrefu katika mgahawa huo, George aliamua kumchukua dada yake ili wafanye kazi pamoja kutokana na ukata ulioikumba familia yao. Walikuwa ni wenye rangi mchanganyiko.

January 23, 2018

ZOLILE HECTOR PIETERSEN: MTOTO ALIYELAZIMU KUANZISHWA KWA KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI AFRIKA KUSINI, TAREHE 16 JUNI KILA MWAKA.

Na Kizito Mpangala

Zolile Hector Pietersen akiwa amebebwa na
Mbuyisa Makhubo baada ya kupgwa risasi.
kushoto ni Antoinete Sithole, dada yake
Zolile Hector Pietersen akilia.
Zolile Hector Pietersen alizaliwa tarehe 19/08/1963 mjini Soweto nchini Afrika Kusini wakati falsafa ya ubaguzi wa rangi ikiwa imepamba moto. Falsafa ya ubaguzi wa rangi ilikuwa ikijulikana kama Apartheid, ambayo ilikuwa ikiendeshwa na makaburu waliokuwa wakitawala nchi ya Afrika Kusini.

Jina halisi la ukoo wake ambalo lilikuwa likitumika na familia yake ni Pitso, lakini fdamilia hiyo ililazimika kubadili na kuwa Pietersen ili kuendana na falsafa ya Apartheid, na kujihisi kama wao ni makaburu ilhali wakiwa ni weusi. Familia hiyo iliamaua kufanya hivyo ili kukwepa dhuruma za makaburu. Hata jina la Zolile lilifutwa kwa muda ili apate nafasi ya kusoma. 

January 21, 2018

ERATOSTHENES WA KIRENE: MWANAHISABATI ALIYEISHI AFRIKA NA KUKADIRIA MZINGO WA DUNIA KWA KIVULI CHA MWANZI.

Na Kizito Mpangala

Eratosthenes alizaliwa mwaka 276 KK (Kabla ya kuazaliwa Yesu Kristo) mjini Kirene, Libya ya sasa. Kirene ni mji mashuhuri ulioundwa na Wagiriki wa kale walioishi Afrika ya Kaskazini hasa Libya ambako ndiko ulikokuwa mji wa Kirene maeneo ya Tripolitania ( sasa ni Tripoli), na Misri maeneo ya Alexandria ilikokuwa maktaba mashuhuri iliyotumiwa na wataalamu wengi wa Ugiriki ya kale. 

Alikuwa akifanya mazoezi mbalimbali ya viungo kila siku asubuhi na jioni. Alijifunza kusoma, kuandika, na kuhesabu. Ni kama vile falsafa ya elimu ya msingi inayotumiwa nchini Tanzania yaani KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu). Pia, alijifunza uandishi wa mashairi na vilevile masuala ya muziki.

January 19, 2018

TAITU BETUL: MALKIA JASIRI ALIYEASISI MJI MKUU WA ETHIOPIA, ADDIS ABABA.

Na Kizito Mpangala

Taitu Betul alizaliwa mwaka 1851 nchini Ethiopia ambayo wakati huo ilikuwa ni Milki ya Ethiopia kabla ya kuwa Jamhuri. Neno Taitu kwao lilimaanisha “mng’ao wa jua au jua”, hilo ndilo lilikuwa jina lake la asili.
Baada ya kubatizwa katika kanisa la dhehebu la Orthodox aliitwa Walatta Mikael, lakini baadae alilirudia jina lake la asili yaani Taitu Betul. Baba yake alikuwa aliitwa Betul Haile Maryam ambaye alikuwa na uhusiano na ukoo wa Mfalme Sulemani. Lakini baba yake huyo hakufahamika sana kama alivyofahamika mjomba wake  aliyeitwa Dejazmach Wube Haile Maryam, ambaye alikuwa mtawala wa Ethiopia Kaskazini miaka ya 1840.
Familia ya baba yake Taitu ilikuwa imeweka makazi yake katika mkoa wa Semien ambao ulikuwa ukitawaliwa na Mfalme Susenyos I. Baba yake alikuwa ni mjukuu wa Ras Gugsa ambaye alikuwa mshirika wa familia iliyotawala eneo la Yejju iliyokuwa na asili ya kabila la Oromo. Baba yake huyo alikuwa Muislamu na baadae akabadili dhehebu akajiunga na Ukristo.

Taitu Betul alikuwa na nafasi kubwa ya kuwepo katika ngazi za juu katika maeneo hayo kutokana na ndugu zake wengi kuwa katika nafasi za milki mbalimbali hasa katika ngazi za mikoa. 

Taitu Betul aliolewa mara nne na kuachwa kabla ya kukutana na Mfalme Menelik wa Shewa kama mke wa tatu. Muda mfupi baadae, baada ya kuolewa na Mfalme Menelik wa Shewa, Mfalme huyo akatawazwa kuwa Mfalme wa Milki ya Ethiopia (Ethiopian Empire). Taitu Betul akiwa kama Malkia pamoja na mumewe Mfalme Menelik II walikuwa wanamiliki watumwa elfu sabini (70,000).

January 17, 2018

KUPIGA MARUFUKU MAVAZI YA NUSU UCHI

NA PROFESA ANNA TIBAIJUKA (MB)
Profesa Tibaijuka.

 UKIONA watu wanahangaika na suala la mavazi hasa kukazania yale yanayoficha mwili wa mwanamke ujue wana matatizo yao wamelishwa kasumba ya wageni. Dhana ya kuficha mwili ni kweli haina Uafrika wowote ndani yake. Mwafrika katika asili yake haangaiki kuficha mwili wa mwanamke. Hauoni kama chombo cha kumfurahisha mwanaume bali kiungo muhimu kumruhusu mwanamke kutimiza wajibu wake.

Kwa mfano wakati mwanamke wa kizungu anahangaika kujificha kunyonyesha mtoto Mwafrika asili anatoa ziwa mtoto ananyonya hadharani. Hapa titi ni mali ya mtoto siyo ya mume.

Kwa hiyo kabla ya wakoloni kufika na wamisionari walioandamana nao wakiwa wamevaa nguo ndefu watoto walikuwa uchi wasichana walipewa ngozi kujisitiri sehemu za siri wakivunja ungo na wanawake nao yalikuwa hayo hayo. Kulikuwa hakuna ubakaji kwa sababu hiyo. 

Ni kweli utasema jamii ilikuwa haijaendelea na maskini. Unaweza pia kusema hali ya maendeleo ilikuwa duni.Nguo hakuna. Lakini hoja hapa ninayolenga kupangua ni ile kwamba wanawake wakijifunua kwa kuonyesha uso au mikono au matiti au miguu yao au mapaja wanawakwaza wanaume. Sio kweli. Mbona mababu zetu hawakukwazika hizo enzi nilizoelezea? Mbona hawakubaka watoto na wasichana kama ilivyo sasa?

December 30, 2017

PUGU HADI PERAMIHO; Kijiji cha Dar, Utemi wa Wangoni na kumbukizi maridhawa.

Katika kitabu cha "PUGU HADI PERAMIHO" kuna masimulizi ya kutoka mwaka 1888-1988 na ujio wa Wamisionari wa kijerumani kupitia Shirika lao la Benedictine Fathers lenye makao yale mjini Peramiho kwa sasa.  
Kitabu hiki ni mkusanyiko wa barua na kumbukizi binafsi (Diaries) zilizoandikwa na Mapadre, Mabruda, Masista wakielezea masuala ya ukoloni wa Kijerumani, Injili, Umisionari, Wapagazi, Wangoni na kupenda vita na starehe pamoja na mahusiano ya kibadamu kati ya wazungu na waafrika.

PADRE ANDREAS AMRHREIN
Kitabu hiki kinaanza kwa maandiko ya Abate Lambert Doerr, OSB. Kwanza "Abate" ni wadhifa waliopewa wakuu wa mashirika ya Benedictine Fathers. Lambert anafungua pazia la masimulizi ya Wamisionari Wabenediktine kusini mwa Tanzania. 

December 06, 2017

“NYASA INAWEZA KUJENGA KIWANDA CHA MATUNDA. HOTELI NAZO ZINATUDAI MAHITAJI MENGI WANYASA”

NA MARKUS MPANGALA

MAELFU ya vijana waliotokea Wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma wamesoma elimu ya Sekondari  katika shule ya Lundo iliyopo Kata ya Lipingo wilayani humo. Hata hivyo sio vijana wote wamepata elimu ya sekondari ndani ya Wilaya ya Nyasa au shule hiyo pekee, lakini idadi kubwa wamesoma hapo. Katika kipindi cha miaka 2000 kumekuwa na ongezeko la shule za sekondari, ambapo nyingi sasa hivi ni za Kata tofauti na awali. 

Miongoni mwao ni ALPHONCE KWENDE ambaye ni mwanazuoni wa masuala ya Kilimo hapa nchini.  Yeye ni mzaliwa wa kijiji cha Chinula, tukiwa tumehitimu pamoja shuleni.  Amejikita katika fani ya Kilimo na anaitazama wilaya Nyasa ikiwa na uwezo wa kujenga Kiwanda pamoja na watu kubadilika kuwa na mawazo ya kibiashara kupitia kilimo. 
SOMA MAHOJIANO KAMILI…..

SWALI:  Habari za mchana mtumishi. Hebu tueleze baada ya  elimu ya Sekondari  Lundo ulichaguwa kwenda shule gani?
ALPHONCE KWENDE: Yes, nilijiunga na Kibiti High School, iliyopo mkoani Pwani kusoma masomo ya kidato cha tano na sita.
Mwanazuoni KWENDE akiwa kwenye shughuli za Kilimo.

SWALI: Umewahi kujiunga na Chuo chochote baada ya kuhitimua ‘High School’?
KWENDE: Sikujiunga na Chuo Kikuu kingine zaidi ya SUA. Hiki ni Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, kipo mkoani Morogoro. Hapo ndipo nilihitimu Shahada yangu ya Kilimo kwa ujumla wake.

SWALI: Aaah! Ndiyo maana kilimo kimekushika sana? Nadhani ni msingi wa Lundo katika somo hilo. Nililipenda sana ila likafutwa. 
KWENDE: Ni kweli kabisa. Kabisa, Lundo walitengeneza msingi mzuri sana kwenye somo la Kilimo, ndiyo matunda yake niliyonayo sasa. Nilimalizana na elimua ye sekondari ya juu  High School, mwaka 2004. Kisha mwaka 2009 nilifanikiwa kuhitimu shahada yangu ya Kilimo pale SUA.

SWALI: Tutajie mambo muhimu ambayo unadhani yanaweza kuipaisha Wilaya ya Nyasa kiuchumi, Afya na Mengine.

KWENDE: Kujibu hilo inatakiwa akili iwe imetulia kidogo. Mimi ningependa sana kuzungumzia sekta yangu ya Kilimo na Ufugaji. Ujio wa Wilaya ya Nyasa unaibua hitaji kubwa sana la kuanza kufanya kilimo chenye tija na cha kibiashara maana mpaka sasa bado wilaya ya Nyasa inategemea Muhogo kama zao kwa chakula na biashara. Ingawaje jitihada zinaendelea kufanyika kuendeleza uzalishaji wa zao hilo ili lilete kipato cha kutosha kwa wakulima hao. Ujio wa Wilaya mpya unakuja na ujenzi wa Mahoteli ambako hakuna uzalishaji wa kutosha mpaka sasa wa mazao ya bustani ya uhakika kukidhi hitaji hilo hivyo kutakuwa na uhitaji wa mboga hizo na matunda kama Mananasi,Parachichi,Matango,Matikiti maji na kadhalika.
Mojawapo ya Hoteli iliyopo wilaya ya Nyasa.
SWALI: Bwana Kwende hapa unatudhihirishia kuwa fursa hii inawahitaji waliosomea fani ya Horticulture (kilimo cha mboga mboga na matunda), kwamba wanahitajika sana Nyasa?

November 12, 2017

NANA YAA ASANTEWAA: MALKIA WA MILKI YA ASHANTI ALIYEWAKINGIA KIFUA WAKOLONI WAINGEREZA.

Na Kizito Mpangala

Alizaliwa mwaka 1863 katika mji wa Besease katika jamii ya Ashanti yenye dhahabu nyingi, Ghana ya sasa, magharibi mwa Afrika. Kaka yake Nana Akwasi Afrane alikuwa ndiye Edweso (kiongozi, au chifu) wa milki ya Ashanti wakati huo. Nana Yaa Asantewaa akiwa bado binti alijishughulisha sana na kilimo. 

Kaka yake (chifu Akwasi) alipokuwa Edweso (kiongozi) alituma askari wake kwenda mapiganoni dhidi ya wakoloni. Baadae aliwekwa kizuizini na wakoloni katika visiwa vya Ushelisheli pamoja na mfalme Prempeh I. Akiwa kizuizini, Nana Akwasi Afrane alimteua dada yake NANA YAA ASANTEWAA kuwa malkia wa milki ya Asante. 

Mwaka 1899 gavana wa wakoloni Waingereza Frederick Hodgson aliitisha mkutano mjini Kumasi ili kulazimisha apewe kiti kilichotengenezwa kwa dhahabu tupu ambacho ni alama takatifu ya Ashanti ambapo askari wa kikoloni walishindwa kukipata kiti hicho, hii ni baada ya kufikiri kwamba ugumu wa kuwatawala Waashanti ungeisha baada ya kupata kiti hicho cha dhahabu. Nana Yaa Asantewaa alimteua mjukuu wake mkubwa kuwa mkuu wa miliki ya Ashanti mara baada ya kufariki kaka yake. 

November 10, 2017

SOKA LA WACHINA, LIKABORESHWA UINGEREZA

NA.HONORIUS MPANGALA

INASADIKIKA Polisi wa China walikuwa wanacheza mchezo uliitwa 'Tsh-u' ikiwa na maana ya piga mpira. Mchezo huo ulipenyeza Japan na maeneo mengine ya Roma. 

Soka lilingia Uingereza mwaka 1066 wakati wa utawala wa Mfalme William. Kutokana na wachezajj wengi kupata matatizo ya vifo mfalme Edward na wengine kama Richard walipiga marufuku na kutoka kauli ambayo Kwa yoyote atakayehusika au kuonekana anacheza soka atenda jela.

November 03, 2017

UCHAMBUZI WA KITABU: IT CAN'T BE TRUE



KITABU: IT CAN’T BE TRUE
MWANDISHI: JOHN MWAKYUSA
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA

HII ni mara yangu ya kwanza kusoma riwaya ya mwandishi John R.P. Mwakyusa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Riwaya inaitwa “It Can’t Be True: A Story from Uganda-the Pearl of Africa”, na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na kampuni ya Partridge Publishing ya India.

October 30, 2017

TAARIFA YA KUNG’ATUKA LAZARO NYALANDU, MBUNGE WA SINGIDA KASKAZINI



NIMEAMUA kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017.

October 27, 2017

WAAMUZI WA SOKA KATIKA JICHO LA JAMII.

NA HONORIUS MPANGALA
 
WAAMUZI wa soka wamekuwa wakitazamwa tofauti kulingana na wao wenyewe wanavyojiweka katika jamii ya wapenda soka. Wako ambao wameifanya fani hiyo kuwa moja ya vitu ambavyo vinaweza kuwapatia nafasi ya kucheza matangazo. Pia wapo ambao jamii imewachukulia tofauti kutokana na mitazamo yao.
Jonasia Rukyaa.
Kuna mitazamo hasi kwa baadhi ya wapenda soka waonapo waamuzi wa kike wakichezesha mchezo. Mitazamo hiyo inatokana na asili ya mchezo wenyewe unavyochukuliwa kama ni wa wanaume. Licha ya wanawake kuucheza lakini bado mitazamo hiyo imekuwa ngumu kuwatoka baadhi ya wapenda soka. Ndo maana hata wale wanawake wanaocheza soka ukiwatazama utafikiri wanaume Kwa baadhi yao.

Tanzania ina Mwamuzi wa kati maarufu Jonasia Rukyaa ambaye anafanya vizuri sana. Alikuwepo katika mashindano ya Afcon ya wanawake ikiyofanyika Kameruni. Pia baada ya kushiriki katika kliniki ya waamuzi Kule Ureno mwaka huu amekuwa na mwaliko 'appointment' ya uwepo katika kombe la dunia. Na yupo katika mshindano ya kombe la dunia la vijana wa chini ya miaka 17 Iliyofanyika India. 

FELA ANIKULAPO KUTI: MWANAMUZIKI ALIYEASISI MTINDO WA PIJINI KATIKA MUZIKI NCHINI NIGERIA NA KUOA WANAWAKE 27.

NA KIZITO MPANGALA

TUNASIKILIZA muziki wa Nigeria mara kwa mara na pengine huenda uliwahi kujihoji aina lugha wanayotumia kuimba na hata katika mazungumzo ya kwaida ya wananchi wa Nigeria. Mtindo huo umejaa pijini kwa kiasi kikubwa hali iliyopelekea kuitwa NIGERIAN ENGLISH.

Fela Anikulapo Kuti alizaliwa  mjini Abeokuta nchini Nigeria mwaka 1938. Alipewa majina OLUFELA OLUSEGUN OLUDOTUM RANSOME ANIKULAPO KUTI lakini alifupisha na kuwa FELA ANIKULAPO KUTI. Mama yake alikuwa ni mwanaharakati wa haki za wanawake katika utawala wa kikoloni wakati huo, na baba yake alikuwa ni mwalimu na vilevile alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza mweusi wa chama cha walimu nchini Nigeria. Fela ni binamu ya Akimwande Oluwole Babatubde Soyinka maarufu kama Wole Soyinka.

Fela alisoma nchini Nigeria na baadae mwaka 1958 alikwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kusoma Udakitari wa Dawa lakini alipofika huko alivutiwa na masomo ya muziki hivyo akasoma masomo hayo ya muziki katika chuo cha Trinity. Fela alikuwa mjuzi wa kupiga tarumbeta na Saxophone.

Alianzisha bendi yake iliyoitwa Koola Labitos ambayo ilipiga muziki aina ya jazz.  Huko alimuoa mwanamke aliyeitwa Remilekun Taylor na wakawa na watoto watatu. Mwaka 1963 alirudi nchini Nigeria na kuendelea na bendi yake aliyoianzisha na pia utangazaji katika shirika la utangazaji redioni la Nigeria.
Mwaka 1967 alihamia nchini Ghana na kuanzisha mtindo mpya wa muziki ambao uliitwa Afrobeat. Mwaka 1979 alisafiri kwenda Marekani na alikaa kwa muda wa miezi 10 jijini Los Angels, huko alibadili jina la bendi yake na kuitwa NIGERIA 70. Baadae alitimuliwa nchini humo pamoja na waimbaji wenzake kwa kutokuwa na kibali cha kufanya kazi nchini humo.