Showing posts with label Kenya. Show all posts
Showing posts with label Kenya. Show all posts

September 21, 2017

UCHAGUZI WA KENYA SASA KUFANYIKA OKTOBA 26



NAIROBI, KENYA
 Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya imetangaza tarehe 26 Oktoba kuwa siku ya uchaguzi mpya wa urais nchini humo. Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika  Oktoba 17 mwaka huu ikiwa ni siku chache baada ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya urais kutokana na kukubaliana na pingamizi la Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya, NASA. 

August 24, 2014

BIO CAMP-MBAMBA BAY. NI UFUKWE SAFI KWA KUOGELEA



April 15, 2013

WATOTO WA AFRIKA, AFRIKA NI MOJA

Nimefurahishwa sana na hii picha. Nimefurahia sababu lile dude la ICC ambalo kwangu ni kama genge la majangili, linaona aibu kuu.

Nimependa watoto wa afrika, Uhuru Kenyatta, William Ruto, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wakifurahia katika hali hii.
AFRIKA MOJA, WATOTO WA MAMA MMOJA AFRIKA

March 11, 2013

MAONI YANGU KATIKA MIJADALA YA UHURU KENYATTA VS RAILA ODINGA, SHUKRANI KWA BEN SAANANE KUIBUA HOJA MUHIMU NA NYETI


Nakiri moja ya upumbavu mkubwa ni Barrack Obama kuwa kikaragosi kwake na serikali. Mwanzoni kupitia Hilary Clinton walisema wakenya wasichague watuhumiwa wa ICC yaani Kenyatta na Ruto. Baadaye akaja Barrack Obama akasema atawaunga mkono wakenya katika chaguo lao. UNAFIKI, na nilishawaambia watu Barrack Obama sio mwafrika kwa vile tunavyotaka kumtafsiri kama akina Jesse Owen, Jesse Jackson ambao ni zao la utumwa.

Obama hakuachagua lakini yeye sio zao la utumwa bali mapenzi tu wa binti na mvulana. hajui madhira ya akina jese jackson. kwa suala la kenya Raila Odinga nampenda harakati zake lakini bado naguswa na UZEMBE aliofanya na kudhani atashinda kirahisi. Nimeandika hili, inshallah itachapishwa wiki ijayo jumanne(TAZAMA). Odinga amejitakia sana, kwa njia zake alizopita tangu 2002, 2007 na 2013 sishangai kushindwa kwake.

Hata wengi walipomshinikiza Jaji Willy mutunga katika kesi ya Uhuru kenyatta na Ruto kutogombea, jaji mutunga alisema wanaopinga hawana hoja. Kimsingi Odinga alikuwa na timu dhaifu mno, wala hata CHADEMA sijui kupeleka nini au nini sijui bado Odinga alikuwa na timu dhaifu sana kuliko ile ya mwaka 2007 iliyojaa wababe wa siasa na wenye ushawishi. Hivi nani pale alikuwa na msaada kwa Odinga mwaka huu?

Sioni hata mmoja. Kwahiyo kuwalazimisha wakenya wamchague Odinga ni ukosefu wa heshima tu. wakenya sio wajinga, na wanaolalamika ni watu wa Kisumu tu. Ujinga aliofanya Odinga ahata akiongea na mimi nitamwambia ulifanya makosa haya na haya. kwahiyo CHADEMA kumsaidia Odinga ni kawaida na tunawaheshimu kwa hilo, lakini uamuzi wa mwisho ulikuwa mikoni mwa wakenya.

Sio Obama ambaye sio raia wa kenya. ....... sio mpiga kura wa kenya. kama alitaka Odinga ashinde alipaswa kuwa na adabu sasa. Marekani kutomtaja sio issue kabisa, haitabadilisha kitu, ni ujuha tu. wala Marekani ikitaja jina la kenyatta haina maana ndio inahalalisha. Marekani sio wakenya. 

Hayo mataifa yaliyowapongeza WAKENYA, na WAKENYA wamemchagua nani? Je, kupingwa matokeo mahakamani kunazuia kupongezwa kwa Uhuru Kenyatta ambaye ametangazwa na TUME? ....
na kama Raila Odinga akishinda hiyo kesi, kuna sheria inayozuia kutompongeza Raila Odinga? mimi nadhani USA kutotaja jina la kenyatta ni woga na udhaifu kiakili, sababu ilibidi hata pongezi wasitoe wasubiri hatima ya majibu ya mahakama. ... vilevile, mataifa ya magharibi kutotaja jina kenyatta au kutompongeza bado hakumanishi wao wana uhalali wa kuwamrisha wakenya wamchague nani. .....kwa upande mwingine kisiasa Odinga amejitakia ANGUKO.

March 09, 2013

GEOPOLITICS: ODINGA ALIJITAKIA KUSHINDWA


MTAZAMO WANGU KWA UFUPI; 
Odinga amefanya makosa kisiasa. Timu ya Odinga mwaka huu ilikuwa dhaifu kupindukia. Haikuwa na ushawishi wowote wenye maana. Kalonzo Musyoka anastahili kuheshimiwa lakini naye tumwambie hana ushawishi wowote ambao ungemsaidia Odinga. 
Hebu angalia timu ya zamani; Najib Balala, Charity Ngilu, Mudavadi, William Ruto, na wengine wengi. Odinga amejitakia kushindwa kwanza kabla ya kuangalia kwamba amekuwa kibaraka wa ubeberu. Angalia njia zake, angalia timu yake; AMEJITAKIA KUSHINDWA kabla ya kuwa kibaraka. Kama mtu anakumbuka timu ya NARC ilivyokuwa mwaka 2002, kisha ile ODM ya mwaka 2007, kisha kilichotokea katikati na kusambaratika kabisa kwa timu yenyewe kisiasa, basi hakuna shaka kabisa Odinga alijitakia kushindwa uchaguzi kabla ya kulalamika.

Loading .........

KWA BARRACK OBAMA, MAREKANI

kwamba Obama mwanzoni alimzodoa Uhuru Kenyatta, lakini baadaye nadhani alisoma upepo wa kisiasa na nguvu ya Wiiliam Ruto ilivyokaa vema na Uhuru. kwanza Obama sio raia wa Kenya hata kama mzazi wake anatokea Kenya. Obama akumbuke swali alilowahi kuulizwa na marehemu Hugo Chavez, "Mwanangu Obama unataka kupata kura za uchaguzi nchini kwako kwa kuwashambulia raia wangu wa Venezuela?" Lilikuwa swali zuri sana. Sasa Obama anatakiwa kutambua yeye sio Mkenya, na wakenya wameamua kile kinachofaa kwao bila kujali mashtaka ya Uhuru kule ICC. Na Obama hana sababu za kushinikiza suala la ICC, kwanza aifanye Marekani kuwa mwanachama wa ICC halafu tumkamate Geprge W. Bush. Kama akishindwa kuiingiza nchi yake kuwa mwanachama wa ICC, basi hana mamlaka pia ya kuwachagulia wakenya rais wao.

MATOKEO YA UCHAGUZI NCHINI KENYA: NI UHURU KENYATTA


Dorine Otinga
Na Dorine Otinga, Eldoret, Kenya

Matokeo ya uchaguzi yameshatangazwa huku Uhuru Kenyatta kutoka muungano wa vyama vya Jubilee akitawazwa kuwa rais mpya wa Kenya baada kumshinda Raila Odinga wa muungano wa CORD. Uhuru amepata 50.1% na Raila Odinga 44.3%.

Bila shaka tarehe 4 Machi ni siku ambayo itasalia katika kumbukumbu za wakenya. Ni siku ambayo Wakenya walijitokeza kupiga kura kwa wingi. Kulikuwa na foleni ndefu katika kila kituo, ambayo ni dhibitisho la kutosha kwamba walitaka yule watakae mchagua awe mshindi.

Tume ya IEBC nayo ilifanya mipango kabambe kuhakikisha kwamba inatoa matokeo ya kweli. Korti za Kenya zilifunguliwa masaa ishirini na nne ili kukabiliana na yeyote atakaye vunja sheria. Wasimamizi wote wa IEBC walilala katika vituo vya kupiga kura. Kuna karani mmoja kutoka maeneo ya Kitui ambaye alitiwa mbaroni kutokana na kupeana karatasi mbili za kupiga kura kwa mtu mmoja.

Wale walioenda kinyume na sheria walichukuliwa hatua kali. Shughuli hii ya kupiga kura ilifanywa kwa amani na hali ya usalama ilikuwa shwari. Kura hizi zìlihitajika kuhesabiwa katika kila kituo na matokeo yake kuwasilishwa kupitia njia ya kielektroniki. Shughuli hii ya kuhesabu kura ilikuwa imeanza kupitia njia ya kielektroniki,ambayo ilikuwa ya haraka lakini ikafutiliwa mbali na mkurugenzi wa tume ya IEBC, huku akidai ilikuwa na mushkil kidogo.
    
Ilibidi wasimamizi wa kila eneo bunge kupeleka matokeo ya eneo lao katika kituo kikuu cha kuhesabu kura cha Bomas of Kenya. Ilibidi maafisa wa tume huru ya IEBC kufanya kazi hii kupitia njia ya dijitali.Vyombo vya habari vilifanya kazi kubwa ya kuwasilisha matokeo yaliyokuwa tayari. Matokeo haya tangia mwanzo yalionyesha kuwa Uhuru Kenyatta alikuwa akiongoza  huku Raila Odinga akimfuata kwa karibu. 
          
Kulingana na takwimu za IEBC, Uhuru Kenyatta alipata kura nyingi kutoka maeneo ya Rift Valley na Central Kenya , miongoni mwa maeneo mengine. Raila Odinga naye alipata kura nyingi kutoka maeneo ya Nyanza, Western, na Pwani.Hii ni taashira kwamba  ukabila bado upo. Mgombea kiti mwingine Musalia Mudavadi alikubali kwamba ameshindwa na kuahidi kwamba yuko tayari kumpongeza yule atakayeshinda. Peter Keneth vile vile alisalimu amri.

Kulikuwa na tetesi kutoka upande wa Raila kuhusu jinsi kura hizi zilihesabiwa. Aliyekuwa Makamu wa Rais Kalönzo Musyoka alisema kuwa kuna sehemu ambazo zilisomwa ambapo idadi ya wapiga kura lilipita idadi ya waliojisajili. Jambo hili lilipingwa vikali na Bwana Isaac Hassan,mkurugenzi wa IEBC, ambaye alisema kuwa hajaona suala hilo, na iwapo kutakuwa, angefutilia matokeo hayo mbali.  
          
Uhuru Kenyatta
Hapo jana, kuna kundi kutoka utumishi wa umma, ambacho kiliwasilisha malalamishi yake Mahakamani, huku likitaka matokeo ya uchaguzi kufutiliwa mbali na waanze upya.

Waliweza kuambiwa wapeleke malalamishi yao katika mahakama ya juu kulingana na katiba. Kwa upande mwingine, mgombea mwenza Uhuru, ambaye ni Wiliam Ruto, alipongeza na kushukuru tume huru ya IEBC kwa kazi nzuri. Licha ya tetesi hizi zote Wakenya walionekana watulivu na kuwa tayari kumkaribisha Rais mpya. Walifurahishwa na uwazi ambao ulikuwa katika tume hii. 

Mnamo usiku wa tarehe nane, tume hii iliweza kudhibitisha kwamba Uhuru Kenyatta alitimiza asilimia hamsini ukiongeza moja, ya kura zote, jambo ambalo mgombea urais anafaa kutimiza ili kuwa Rais kulingana na katiba ya Kenya.  ingawa hakuwa amefikisha asilimia hamsini ya kura zote.

Uhuru Kenyatta alipata kura milioni sita nukta moja  huku Raila akipata kura milioni tano nukta tatu. Kura zote zilizopigwa ni milioni kumi na mbili nukta tatu. 

Tume ya IEBC, iliahidi kuwasilisha matokeo yake pindi tu watakapokuwa tayari kupitia mkurugenzi wao. Kwa upande wake,Uhuru Kenyatta aliandaa jukwa lake,katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, mjini Nairobi huku akisubiri matokeo haya yasomwe rasmi, ndipo atoe hotuba yake.
Katika ukumbi huu,aliwaalika wagombea wengine walioshinda. Asubuhi ya kuamkia leo, imekuwa ni shangwe na hoi hoi kutoka kwa wafuasi wa Uhuru. Licha ya hayo, wakenya wameonywa kutokana na matamshi ya chuki na uchokozi miongoni mwao.

Kwa upande mwingine, Raila Odinga akitoa hotuba yake baada ya kutangazwa kushindwa uchaguzi dhidi ya Uhuru Kenyatta, alisema anakusudia kupeleka malalamishi kuhusu Tume ya IEBC na anasema ataenda supreme court. Pia alisema kuwa kuharibika kwa vyombo siku ya uchaguzi ilikuwa mpango na anasema ana imani na mahakama ya juu. Raila anasema  kuwa ajenti wake walitolewa nje wakati wa kuhesabu kura jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Odinga, amesema kuwa atakubali uamuzi wa mahakama ya juu na kuwa ana ushahidi wa kutosha katika malalamiko yake. Lakini amewaomba wafuasi wake kutulia kwani hangependa ya 2007 kutokea tena.amemaliza kwa kusema kuwa haki itatendeka.

Dorine Otinga ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton nchini kenya, akisomea Shahada ya Elimu katika lugha ya Kiswahili.

March 02, 2013

SHAMRASHAMRA ZA KISIASA NA UCHAGUZI MKUU KENYA


Dorine Otinga
Na Dorine Otinga, Eldoret, Kenya
BILA shaka, zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa kihistoria nchini Kenya ambao utafanyika Machi, 4 mwaka huu ikishuhudiwa wagombea nane wakichuana kuwania nafasi ya urais. Maandalizi kati ya wakenya dhidi ya uchaguzi yanafanywa kwa udi na ambari. Wanasiasa wanajaribu kushindani kila siku kwa kumwaga sera za kuwezeshwa kupata kura.
Kama nilivyoelezea juma lililokwishapita juu ya kura za maoni ya wananchi wa Kenya wanaosadiki wagombea wao. Nikumbushe tu, wakenya 328 walioulizwa kwenye zoezi la kura za maoni juu ya uchaguzi walikuwa na mitazamo mbalimbali.
Watu 92% wamekubali kuwa mdahalo kwa njia ya runinga ulisaidia kujua mbinu na uwezo wa kujieleza wa wagombea wao. Wengine 24% walilazimika kubadili mawazo yao kwa ajili ya wagombea waliodhani watawachagua. Wapigakura hawa 34% ina maana wamebadili mawazo kutoka kwa mgombea mmoja kwenda kwa mwingine. Wakenya 27% wanadhani Uhuru Kenyatta atashinda uchaguzi.
Wakenya 26% wanaamini Peter Kenneth atashinda kutokana na kufanya vizuri kwenye mdahalo. Vilevile 22% ya wakenya wanaamini Raila Odinga atashinda uchaguzi na yeye ndiye bingwa wa ushawishi hadi sasa akiwa na mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka. Halafu kuna 12% wanapenda kuona Martha Karua akishinda kuchukua uongozi. Hata hivyo, kuna baadhi ya wakenya ambao hawajaamua iwapo watapiga kura au la. Waangalizi wa kimaitaifa wameshaanza kuwasilia hapa Kenya na wanatahadharisha ongozeko la watu watakaoacha kupiga kura.
Sababu zinazotolewa juu ya baadhi ya wakenya kuacha kupiga kura ni kutokana na yale machafuko ambayo yalitendeka mwaka wa 2007 na kusababisha maafa makubwa kwa wakenya. Wengi wao ni walioathiriwa na ghasia baada ya uchaguzi ambao wamekuwa na uchungu kutokana na mambo yaliyotokea baadaye, huku Uhuru Kenyatta na William Ruto wakifunguliwa mashtaka huko The Hague, nchini Uholanzi.
‘’Sisi tulifukuzwa shambani kwetu kule Molo, na tumeishi katika hema kwa muda wa miaka mitano.Tulijuta sana. Bado sijaamua iwapo nitapiga kura’’, alisema mwanamke mmoja aliyekuwa katika kambi ya wakimbizi. Ingawa serikali ilifanya juhudi ya kuwapa wakimbizi hawa mahali pa kuishi kwa muda na kukabiliana na maisha mapya yenye changamoto kubwa kuliko hali ile waliyozoea kabla ya machafuko.
Raila Odinga
Nje ya Kenya wetu wanadhani shamrashamra za siasa katika uchaguzi mkuu zimekuwa kwenye sura ya mdahalo na upigaji kura pekee. Lakini ukweli ni kwamba watpo watu wenye uchungu kwa hali iliyotokea.
Mpaka sasa hivi, bado wengi wao hawajaamua iwapo watapiga kura tena ifikapo Machi 4, licha ya wapigakura milioni 14.3 kuandikishwa na kupata sifa zote za kuchagua viongozi. Hili limekuwa kero kubwa kwa Tume huru ya Uchaguzi, na inaelekea Mkuu wa Tume hiyo, Isaac Hassan atakuwa na jukumu lingine kuwaelezea wakenya umuhimu wa kushiriki kikamilifu zoezi la kupiga kura.
Baadhi ya vituo vya habari vimeungana kwa nguvu kubwa sana na kuanzisha midahalo isaidiayo wakenya kujua ni kiongozi yupi atakayefaa kuchaguliwa ifikapo Machi 4. Juhudi hizi zimeongeza usikivu mkubwa sana kwa vituo vya habari, kwani vimefanya kazi ya kueneza uzalendo wa wakenya. Kulingana na mdahalo wa kwanza ambao ulihusishwa na runinga ya Citizen na vituo vingine, mgombea Mohamed Abduba  Dida, ambaye ni mgeni katika ulingo wa siasa aliweza kuinua umaarufu wake kutokana na uwezo wake wa kujieleza, kipaji chake cha kushawishi hadhira na vile vile ucheshi wake ambao uliamsha hisia za wananchi.

Raila odinga na Uhuru Kenyata walisalia maarufu zaidi kutokana na kuwa kwenye ulingo wa siasa. Mpaka sasa Odinga na Uhuru wanachuana vikali, huku taasisi za utafiti zikionyesha wanakaribiana sana kwa kujipatia ushindi. Mathalani, duru za kisiasa zinasema kwamba Uhuru Kenyatta na William Ruto hawatahudhuria mdahalo wa mwisho utakaofanyika kabla ya uchaguzi. Jambo hili limezua mjadala mkubwa hapa Kenya, ambapo wengi wanajiuliza kulikoni wasiweze kupanga njia za kufanikisha mdahalo badala yake wanakataa kuhudhuria?

Lakini kwa upande wao Uhuru na Ruto wanasema licha ya Changamoto ambazo zimewakumba, ikiwemo kesi katika mahakama ya ICC, wao wanaendeleza kampeni zao bila wasi wasi. Ilikuwa ni afueni kwao, baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kusema kwamba, haiwezi kuwazuia kugombea kiti cha Urais, na kwamba uamuzi huo ungeweza kuamuliwa na Mahakama ya rufaa.    Akielezea sababu za kujitoa kwenye mdahalo wa mwisho, Uhuru Kenyatta alisema kuwa katika mdahalo uliomalizika hakutendewa haki hivyo haoni sababu za kushiriki tena.

Uhuru akielezea hilo amesema kitendo cha kuingizwa kesi iliyoko ICC kiliudhi kambi nzima ya Jubilee hivyo anastahiki kufuata ushauri wa kambi hiyo kujiondoa kwenye mdahalo wa mwisho kabla ya uchaguzi. Aidha, kumekuwa na tetesi kutoka kwa wanachama wa ODM, ambacho kinaongozwa na Raila Odinga, kwamba wanachama wa Jubilee wana mpango wa kuhakikisha mgombea wao Uhuru Kenyatta anashinda kiti cha urais kwa hali yoyote ile.

Suala hili limewatia wakenya tumbo joto kwani hawataki ghasia, wanaona kitendo cha wanachama wa Jubilee kung’ang’ania kupata ushindi kwa namna yoyote ile ni kutaka kuchochea ghasia miongoni mwa wakenya ambao wanataka utulivu. Wanachama wa ODM wanadai kuwa Jubilee wanataka kuiba kura ili mgombea wa Jubilee, Uhuru Kenyatta ashinde kiti hicho, jambo ambalo hawajathibitisha hadi sasa.
Hii imekuwa kashfa ya kwanza kutolewa kwenye kampeni za uchaguzi zinaoendelea hapa Kenya. Aidha, hawa ODM hawasemi ni namna gani Jubilee ya Uhuru Kenyatta watakavyoiba hizo kura, bali wanaendelea kushutumu na kuchochea matumbo moto kwa wapigakura. Chama cha Jubilee ambacho kinaongozwa na Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza Wiliam Rutto, kimejaribu kufanya kila njia kupinga tetesi za  wanachama wa ODM wanaoongozwa na Raila Odinga kwamba walitaka kuiba kura.
Wengi wanasema haifai kwa ODM na Odinga kueneza fitina kama hii ambayo haina chembe ya ukweli. Wanasema kama Odinga hakujifunza kwa Uhuru Kenyatta na Ruto juu ya mashtaka yao kule ICC, ni vema akachunga kauli zake uchwara ambazo zinachochea uharibifu wa amani kwa wapigakura.
Kulingana na utafiti ambao umefanywa na baadhi ya kampuni nchini Kenya, Raila Odinga anamshinda Uhuru Kenyatta kwa asilimia chache sana, huku wakifuatwa na wagombea wengine. Wagombea hawa wawili wanafuatana uso kwa uso na wakenya wanatarajia mmoja wao kuibuka mshindi baada ya uchaguzi wa Machi 4, mwaka huu.
Huku uchaguzi ukikaribia, serikali iliamua kuunda Tume ya Taifa ya Uwiano na Utangamano, ikiwa na lengo  la kuwaunganisha Wakenya na kuwachukulia hatua wakali wanasiasa na wananchi wanaotoa matamshi ya kichochezi. Mwenyekiti wa tume hiyi ni Mzalendo Kibunja, ambaye amesema Tume yake haitamuonea aibu mwanasiasa na mwananchi yeyote atakayeleta uchochezi kwa wakenya. Wengi wanakumbusha ikwemo hatua ya ODM, kusema Jubilee wataiba kura, kuwa inabidi Mzalendo Kibunja achukue hatua kali zaidi dhidi yao.
Katika mahojiano na mwanahabari Jimmy Gathu wa kituo cha Citizen hapa Kenya, Mzalendo Kibunja, alisema kuwa wale wote wanaoeneza matamshi ya kichochezi na chuki watachukuliwa hatua kali.
Hatua ya tume ya Uwiano na utangamano, imekwenda mbali zaidi na imewaonya wanaotumia mtandao wa facebook na Twitter kuwa makini kwa maandishi yao wanayowaeleza wenzao kuhusu uchaguzi mkuu wa hapa Kenya.
Uhuru Kenyatta
Jaji mkuu wa Kenya Dk. Willy Mutunga ametangaza kuwa anatishwa na baadhi ya wanasiasa, hali ambayo inamfanya asiwe na amani na kukisia kuwa huenda uchaguzi huu unaweza kuwa na machafuko pia. Jaji Mutunga anadai kuwa vitisho hivi vinamshinikiza kutekeleza maslahi yao badala ya kujali uamuzi wa wakenya kwenye uchaguzi.

Hata hivyo, Jaji huyo alisema kwamba vitisho dhidi ya Idara ya Mahakama havitawafanya majaji kutekeleza maslahi ya kundi fulani la watu. Jaji alisema kwamba alipokea vitisho hivi karibuni wakati wa kesi iliyowahusisha Uhuru Kenyatta na William Rutto ilipokuwa ikisikilizwa huko nchini Uholanzi.
Alieleza jinsi ujumbe wa barua aliyoipokea ilivyokuwa ikimtisha, na kwamba angetendewa jambo baya na kundi haramu la Mungiki, iwapo angetoa uamuzi wasioupendelea katika kesi ya wawili hao. 

Mwaka wa 2007, ilisemekana kwamba Uhuru  Kenyatta alitumia kundi hili kuwaangamiza Wakalenjin Mkoani Rift Valley. Jaji Mutunga analaumu serikali kwa kumdhulumu baada ya kuamrishwa na afisa mmoja wa uhamaji, kusafiri kwenda Dar es Salaam kwani hakuwa na idhini ya mkuu wa Umma, Francis Kimemia.
Jaji mkuu ameeleza hofu yake ya majaji kutishwa kisiasa huku uchaguzi ukikaribia kwani inahatarisha usalama wao na kuiweka nchi kwenye hatari ya machafuko. Jaji huyo alitangaza msimamo wake kuwa hatatishika na kama mmoja wa wapiganaji wa demokrasia, yuko tayari kwa lolote.
Jambo jingine ambalo linafanyika katika uchaguzi huu ni matayarisho ya karatasi za kupigia kura yanayofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC). Pia IEBC imeamua kuachana na majaribio ya uchaguzi yaliyopangwa kufanyika mapema Februari 24. Katibu wa IEBC, James Oswago alisema kuna kazi ngumu kufanya majaribio badala ya uchaguzi kamili. Hivyo mashauriano yalifanyika kwamba majaribio yafanyike Februari 18 yaani Jumatatu iliyopita ili kuwaruhusu wananchi kupigakura kwa ufasaha ifikapo Machi 4.
Naye meneja wa Elimu kwa wapigakura IEBC, Nixon Ng’ang’a alisema kwa mara ya kwanza katika historia ya hapa Kenya, wapigakura watakuwa wanpiga kura kwa nafasi za uchaguzi sita na siyo tatu, hivyo watahakikisha zoezi linakwenda vema. Kwingineko ni shamrashamra zinazoendelea hapa, kwani IEBC imesema wagombea wote nane wanatakiwa kufanya kampeni za amani ili kuwalinda wakenya dhidi ya machafuko.

Dorine Otinga ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton nchini Kenya na atakuwa miongoni mwa wasimamizi wa uchaguzi huo.